Home » » WANANCHI WATAKA KATIBA MPYA IWAFUTE WAKURUGENZI NA MAKATIBU TAWALA

WANANCHI WATAKA KATIBA MPYA IWAFUTE WAKURUGENZI NA MAKATIBU TAWALA

Masoud Masasi, Dodoma Yetu
BAADHI ya wananchi wa tarafa ya Hombolo katika Manispaa ya Dodoma wamependekeza katika katiba ijayo wakurugenzi pamoja na makatibu tawala wa mikoa na Wilaya kutokuwepo badala yake kazi zao zifanywe na wakuu wa mikoa na wilaya ili kupunguza mlundukano wa viongozi ambao wanaigharimu serikali fedha nyingi za kuwalipa.

Pia wametaka kuwepo kwa utaratibu wa wakuu wa mikoa na  wilaya kuteuliwa kufanya kazi katika maeneo wanayotoka ili kuweza kuleta ufanisi mkubwa wa kazi kwa kuwa wanajua changamoto za eneo hilo.

Wanakijiji hao waliyasema hayo juzi wakati wa mjadala wa mchakato wa kupata katiba mpya ulioandaliwa na Mtandao wa Asasi zisizo za serikali wa DUNGONET iliyofanyika katika  ukumbi wa chuo cha serikali za mitaa cha Hombolo.

Yonadi Mtagwa amesema serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kuwalipa mishahara wakurugenzi na makatibu tawala hao ambapo amesema wakuu wa mikoa na wilaya wanatosha kufanya kazi za watumishi hao.

Mkazi mwingine David Meshack amesema majukumu ya mkuu wa mkoa na wilaya ni madogo hivyo wanao nafasi ya kuweza kufanya kazi za watumishi hao.

Meshack amesema hilo liende sambamba na wakuu hao kupelekwa kwenye vituo vya kazi ambavyo wamezaliwa kwa kuwa wataweza kufanya kazi kwa ufanisi kutokana na kujua mambo mengi katika maeneo hayo.

Katika hatua nyingine wanakijiji hao pia wametaka wakuu wa mikoa na wilaya wateuliwe wale ambao si wanachama wa chama cha siasa chochote ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi pasipo kuogopa  wala kutetea mabaya ya chama chake.

Blogzamikoa

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa