- I. UTANGULIZI:
a) Maswali
- Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kutekeleza na kukamilisha majukumu yetu katika muda uliopangwa. Katika Mkutano huu Maswali 120 ya Msingi na 305 ya Nyongeza ya Waheshimiwa Wabunge yalijibiwa na Serikali. Aidha, jumla ya Maswali 12 ya Msingi ya Papo kwa Papo na 11 ya Nyongeza yalijibiwa na Waziri Mkuu.
b) Miswada
- Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu, Bunge lako Tukufu lilijadili na kupitisha Miswada Mitatu (3). Miswada hiyo ni:
i) Muswada wa Sheria ya Taifa ya Umwagiliaji wa Mwaka 2013 [The National Irrigation Bill, 2013];
ii) Muswada wa Sheria wa Vyama vya Ushirika wa Mwaka 2013 [The Cooperative Societies Bill, 2013]; na
iii) Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2013 [The Constitutional Review (Amendment) Bill, 2013].
- Mheshimiwa Spika, napenda nitumie nafasi hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa kujadili na kukubali kupitisha Miswada hiyo kwa umahiri mkubwa. Aidha, niwapongeze Mawaziri na Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Wataalam wote waliohusika na Maandalizi ya Miswada hiyo. Kipekee niwashukuru Wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge kwa kupitia Miswada yote na kutoa maoni yao, ambayo sehemu kubwa yamezingatiwa na Serikali katika kuboresha Miswada hiyo.
- Mheshimiwa Spika, asubuhi ya leo Bunge lako Tukufu lilipokea Kauli za Mawaziri wa Fedha na Uchukuzi. Wote tunawashukuru kwa maelezo yao.
- II. UTEKELEZAJI WA MFUMO WA MATOKEO MAKUBWA SASA “BIG RESULTS NOW”
- Mheshimiwa Spika, katika Mkutano wa Kumi na Moja wa Bunge uliomalizika mwezi Juni, 2013 Serikali iliahidi kwamba, katika Bajeti ya mwaka 2013/2014 itaanza kutekeleza Mfumo Mpya wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo ambao unajulikana kwa dhana mpya ya ‘Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa’ (Big Results Now-BRN). Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, Mfumo huo mpya umeanza kutekelezwa kama ilivyokusudiwa.Utekelezaji wa Mfumo huu mpya umekuwa unatekelezwa katika mikondo (streams) mikuu miwili, inayoenda sambamba. Mkondo wa Kwanza ni kujenga na kuimarisha mfumo utakaohakikisha kuwa matokeo Makubwa tarajiwa katika mikakati yetu ya kuleta maendeleo endelevu Nchini yanapatikana (Strengthening the Delivery System). Mkondo wa Pili ni kusimamia, kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa mikakati iliyoainishwa katika Awamu ya Kwanza ya uchambuzi wa Kimaabara (LABs).
- Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Juni, 2013 maandalizi muhimu ya Awamu ya Kwanza ya uchambuzi wa kina wa kimaabara wa maeneo sita (6) yaliyochaguliwa Kitaalam ulikuwa umekamilika. Napenda kuwakumbusha kuwa, maeneo hayo sita ni: Nishati ya Umeme, Uchukuzi, Kilimo, Elimu, Maji na Ukusanyaji wa Mapato. Kazi zilizotekelezwa katika kipindi hiki kifupi cha kuanzia Julai 2013 hadi sasa ni pamoja na zifuatazo:
a) Serikali imemteua Mtendaji Mkuu wa Taasisi Mpya ya President’s Delivery Bureau (PDB)
na amekwishaanza kazi tayari. Vilevile, Naibu Mtendaji Mkuu wa Taasisi
hiyo anayehusika na masuala ya Mageuzi ya Kilimo ameteuliwa hivi
karibuni;
b)
Watendaji wa Wizara husika pamoja na Wakuu wa Mikoa wote, Makatibu
Tawala wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya zote Nchini wamepata mafunzo kuhusu
Mfumo Mpya wa Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa;
c) Mawaziri wa Wizara Sita zilizoanza kutekeleza Mfumo Mpya wa ‘Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa’ (Big Results Now) wameingia Mikataba ya Utendaji na Mheshimiwa Rais (Performance Contract) yenye Viashiria vya Utekelezaji (Key Performance Indicators).
Aidha, Makatibu Wakuu wa Wizara Sita pamoja na Watendaji wao, Wakuu wa
Mikoa yote, Makatibu Tawala wa Mikoa, pamoja na Watendaji wao, wote
wameingia Mikataba hiyo ya utendaji kazi ili kufikia malengo
yaliyowekwa;
d) Muundo wa Taasisi ya President’s Delivery Bureau na ule wa Vitengo vya Kusimamia Utekelezaji katika Wizara (Ministerial Delivery Units – (MDUs))
umeidhinishwa tangu mwanzoni mwa mwezi Agosti, 2013. Aidha, tangu mwezi
Julai 2013 Wizara zinazohusika na matokeo ya awali zimeunda timu za
muda za kusimamia na kufuatilia utekelezaji ili usimamizi stahiki wa
utekelezaji uweze kuendelea wakati taratibu za kupatikana kwa watumishi
wa kudumu zikiendelea;
e) Wizara zote sita zenye Miradi ya Kipaumbele chini ya Mfumo wa ‘Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa’ (Big Results Now) ambazo ni Nishati, Kilimo, Maji, Elimu, pamoja na Uchukuzi zimeanza utekelezaji wa Miradi husika; na
f) Wizara zote Sita zimeanza kuandaa ripoti za utekelezaji za kila wiki na kuziwasilisha kwenye President’s Delivery Bureau kama mfumo unavyoainisha.
- Mheshimiwa Spika, kazi nyingine zilizofanyika ni kuundwa na kuanza kazi kwa Kamati Maalum za Kuratibu na Kusimamia Utekelezaji wa Miradi ya ‘Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa’ (Big Results Now) zinazojulikana kama National Key Results Areas (NKRA) Steering Committees. Kamati hizi zimeundwa na Wawakilishi wa Wadau muhimu katika kuhakikisha mikakati ya utekelezaji inatekelezwa na matokeo tarajiwa yanapatikana kwa wakati. Kamati hizi zinaongozwa na Mawaziri husika na zinakutana mara moja kila mwezi kujadili mwenendo wa utekelezaji, ili kutatua vikwazo na kushughulikia changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika utekelezaji.
- Mheshimiwa Spika, vilevile, Kamati ya Kitaifa ya Kusimamia Mageuzi na Utekelezaji (Transformation and Delivery Council – (TDC)) imeundwa na kuanza kazi. Kamati hii ambayo Mwenyekiti wake ni Mheshimiwa Rais ndiyo yenye mamlaka ya kusimamia utekelezaji katika Mfumo wa ‘Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa’ (Big Results Now).
- Kamati hii itakuwa inakutana mara moja kila mwezi kutathmini maendeleo ya utekelezaji na vilevile kuzipatia ufumbuzi changamoto na vikwazo ambavyo vitakuwa vimeshindwa kupatiwa suluhisho stahiki katika ngazi za Wizara.
- Kamati hiyo itafanya kikao chake cha kwanza baadaye mwezi huu ambapo itapokea muhtasari wa taarifa ya utekelezaji wa ‘Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa’ (Big Results Now) na kisha kutoa maamuzi na muongozo stahiki wa hatua za utekelezaji zinazofuata pale itakapohitajika.
- Katika maandalizi ya Kikao hicho, nilikutana na Mawaziri wote Sita wanaohusika tarehe 21 Agosti, 2013 kujadili hatua za utekelezaji na changamoto zilizopo na mikakati ya kuzipatia ufumbuzi. Aidha, kuanzia tarehe 7 hadi 8 Septemba, 2013 Ofisi yangu inatarajia kukutana na Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa kupitia na kujadili Taarifa za Utekelezaji katika kipindi cha miezi miwili iliyopita.
- Mheshimiwa Spika, muda ambao utekelezaji wa mfumo wa ‘Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa’ (Big Results Now) umeanza kutekelezwa rasmi ni mfupi mno, lakini dalili zinaonesha kuwa, matokeo mazuri yataanza kuonekana muda si mrefu kuanzia sasa na yatakuwa yakianishwa kadri yanavyojitokeza.
- Serikali kwa ujumla imejipanga kuhakisha Miradi ya ‘Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa’ (Big Results Now) inatekelezwa kwa wakati na kwa ukamilifu kwa kuzingatia Viashiria vya Utekelezaji (Key Performance Indicators - KPIs) vilivyoainishwa wakati wa uchambuzi wa kimaabara kwa mwaka huu wa fedha.
- III. KILIMO
a) Hali ya Chakula
- Mheshimiwa Spika, tathmini ya awali ya uzalishaji wa mazao ya chakula katika msimu wa 2012/2013 iliyofanyika kati ya Mwezi Julai na Agosti 2013 kwa Mikoa 25 imeonesha kuwa Mikoa 8 ya Rukwa, Katavi, Mbeya, Ruvuma, Iringa, Kagera, Geita na Njombe itazalisha ziada ya chakula. Aidha, Mikoa 8 ya Kigoma, Simiyu, Morogoro, Lindi, Mtwara, Pwani, Manyara, na Tanga itajitosheleza kwa chakula. Aidha, Mikoa 9 ya Dar es Salaam, Dodoma, Tabora, Arusha, Mwanza, Shinyanga, Singida, Kilimanjaro na Mara itakuwa na uhaba wa chakula na kwamba Halmashauri 60 katika Mikoa 19 zitakuwa na maeneo tete yatakayokabiliwa na uhaba wa chakula.
- Mheshimiwa Spika, kwa ujumla hali ya uzalishaji na upatikanaji wa Chakula Nchini hadi kufikia Mwezi Agosti 2013 ni ya kuridhisha katika maeneo mengi kufuatia mavuno ya msimu wa 2012/2013 kuanza kuingia sokoni. Bei za wastani za vyakula sasa hasa kwa mazao ya mahindi na mchele zimeanza na zinaendelea kushuka kufuatia uvunaji wa mazao hayo katika maeneo mbalimbali ya Nchi.
- Uchambuzi unaonesha kuwa bei ya wastani ya Mahindi Kitaifa imeshuka kutoka bei ya kilele ya Shilingi 774 kwa Kilo mwezi Februari, 2013 hadi Shilingi 513 kwa Kilo mwezi Agosti, 2013. Aidha, bei ya wastani ya mchele Kitaifa imeendelea kushuka kutoka Shilingi 1,825 kwa Kilo mwezi Februari, 2013 na kufikia Shilingi 1,215 kwa Kilo mwezi Agosti, 2013.
- Mheshimiwa Spika, Wakala wa Hifadhi ya Chakula ilianza kazi ya ununuzi wa Nafaka (Mahindi na Mtama) Mwezi Julai, 2013 katika Vijiji kwa Shilingi 450 kwa kilo na katika Miji kwa Shilingi 480 kwa kilo.
- Aidha, ili kuufanya Wakala kupata chakula cha kutosha kinyume na ilivyokuwa mwaka jana 2012/2013, na kuwawezesha kushindana na wafanyabiashara, Serikali iliamua kuongeza bei watakayotumia Wakala kununulia nafaka hiyo hadi kufikia Shilingi 500 kwa Kilo katika vituo vyote vya ununuzi.
- Hali ya ununuzi na akiba ya chakula kupitia Wakala wa Hifadhi ya Chakula ya Taifa (NFRA) inaendelea vizuri, na kwamba katika msimu wa mwaka 2013/2014, Wakala umepanga kununua Tani 200,000 za nafaka kupitia kanda zake kama ifuatavyo: Makambako (Tani 40,000); Sumbawanga (Tani 50,000); Songea (Tani 50,000); Dodoma (Tani 15,000); Arusha (Tani 20,000); Dar es Salaam (Tani 10,000); na Shinyanga (Tani 15,000).
- Hadi kufikia tarehe 03 Septemba, 2013 Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula umenunua kiasi cha Tani 159,602 za Nafaka ambapo Tani 159,421 ni Mahindi na Tani 181 ni Mtama. Akiba ya nafaka katika Maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula kwa sasa ni Tani 182,587 zikiwemo Tani 182,406 za Mahindi na Tani 181 za Mtama.
- Kiasi hiki kinajumuisha Tani 22,985 zilizokuwepo katika Maghala kabla ya kufanyika kwa manunuzi hayo.
- Napenda kuwahakikishia Wananchi wote kupitia Bunge lako Tukufu kwamba Serikali imejipanga vizuri.
- Chakula cha kutosha kipo kwa maeneo yanayoelezwa kuwa na uhaba wa chakula; na hakuna Mwananchi atakayepoteza maisha yake kutokana na kukosa chakula. Nitumie fursa hii kuwaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya zenye chakula cha ziada kuwahimiza Wakulima kuhifadhi chakula cha kutosha kwa mahitaji ya Kaya zao.
- Aidha, Halmashauri za Wilaya ziweke Mikakati madhubuti ya kuzuia ununuzi holela wa chakula kutoka katika mashamba ya Wakulima.
b) Maandalizi ya Pembejeo za Kilimo kwa Msimu wa 2013/2014
- Mheshimiwa Spika, tutakumbuka kuwa katika Mkutano wa 11 wa Bunge nilieleza changamoto zilizoukumba Mfumo wa kusambaza Pembejeo kwa njia ya Vocha. Serikali iliamua kutafuta Mfumo tofauti ili kuondokana na changamoto hizo.
- Moja ya hatua zilizochukuliwa ni kuweka utaratibu na uwiano wa Asilimia 80 kwa Vocha na Asilimia 20 kwa mikopo. Aidha, Serikali imeidhinisha Bajeti ya Shilingi Bilioni 112.46 kati ya kiasi hicho Shilingi Bilioni 19.97 za ufadhili wa Benki ya Dunia na Shilingi Bilioni 92.49 za Serikali kwa ajili hiyo.
0 comments:
Post a Comment