MASHINDANO ya Wizara na Idara za Serikali
(SHIMIWI), yameanza mjini hapa huku baadhi ya timu zikilalamika kutolipwa fedha
zao na kununuliwa vifaa vya michezo hivyo kukosa ari ya kushiriki michezo hiyo
kikamilifu.
Wakizungumza na Tanzania daima,
baadhi ya wachezaji wa timu shiriki, wameeleza kushiriki michuano hiyo bila ya
kuwa na amani na kusababisha wengine kuwa na tamaa ya kujiunga na timu nyingine
na hata kucheza kwa mgomo wa chini chini.
Wakizungumza kwa kuomba kutotajwa majina yao,
wafanyakazi hao ambao wengine wanatoka timu zenye majina, walibaniasha kuwa,
hawajalipwa zao hadi sasa na wakikosa vifaa kama suti za michezo na vinginevyo.
Akifungua mashindano hayo juzi, Naibu Waziri wa
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makala, amezitaka Wizara, Idara na
Taasisi za Serikali, kuacha tabia ya kushindwa kuleta timu kushiriki kwa
kisingizio cha ukosefu wa bajeti, kwani Bunge limekuwa likipitisha bajeti hizo
bila vipingamizi.
“Kumekuwepo na visingizo vingi vya kushindwa kuleta
timu kushiriki katika michezo hii ambayo ni muhimu, kwa kudai kuwa hakuna
bajeti, wakati bunge limekuwa likipitisha bajeti kwa ajili ya michezo hiyo kila
wakati,” alisema na kuongeza;
Sasa natumia mamlaka yangu kuwaagiza, mhakikishe
mnatenga bajeti ya kutosha ya michezo ili timu zenu ziweze kushiriki katika
mashindano mbalimbali hapa nchini.
Naibu Waziri huyo, alifafanua kuwa, Wizara, Idara
na Taasisi za Serikali zina uwezo wa kuweka bajeti ya kutosha na kuwawezesha
watumishi wake kushiriki michezo, hivyo ni wajibu wao kutekeleza.
Pia, aliwataka washiriki kuonyesha nidhamu pamoja
na kuzingatia ratiba na sheria kwa kuwa wote ni watumishi wa serikali na pia ni
kioo cha jamii.
Awali, akisoma taarifa fupi kwenye ufunguzi huo,
Mwenyekiti wa Shimiwi, Daniel Mwalusamba, aliwataka waajiri kutenga bajeti ya
fedha za kutosha kwa ajili ya kuwawezesha watumishi wao kushiriki kikamilifu
katika michezo na mazoezi, kwani ni sehemu zao za kazi.
Mashindano hayo yanashirikisha timu 43 katika
michezo ya soka, netiboli, kuvuta kamba, baiskeli, drafti, bao na vishale.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment