HALMASHAURI ya Wilaya ya Mpwapwa, mkoani hapa ipo
hatarini kukumbwa na ukame na kuwa jangwa kutokana na kukithiri kwa vitendo vya
uharibifu wa mazingira.
Hali hiyo imedhihirishwa juzi na wataalamu
mbalimbali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Christopher Kangoye aliyeeleza
namna ambavyo wakazi wa wilaya hiyo wamekuwa wakifanya uharibifu wa mazingira
ikiwamo kuchoma miti, kufyeka misitu pamoja na kuharibu vyanzo vya maji.
Akifungua mdahalo kuhusu mabadiliko ya tabia nchi
na athari zake ulioandaliwa na mtandao wa mashirika ya asasi za kiraia wilayani
hapa (Nngomnet), Kangoye alisema hivi sasa suala la uharibifu wa mazingira
limekuwa ni tatizo kubwa na linamuumiza kichwa kutokana na kuwepo kwa
watu wachache wenye ubinafsi.
Alibainisha mazingira ya Mpwapwa hivi sasa
yamekuwa tofauti na awali kutokana na kupoteza asili yake, hasa ukiilinganisha
na enzi za Shaaban Robert (marehemu) ambaye alikuwa akiishi wilayani hapa kwani
mazingira yalikuwa ya kijani na ya kuvutia.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kukithiri kwa vitendo
vya uharibifu wa mazingira, hasa katika maeneo ya milimani kunaweza kusababisha
wilaya hiyo kuwa jangwa.
Ofisa ardhi wa wilaya, Devis Mlowe, alisema
shughuli za kibinadamu hasa kilimo cha kuhamahama, ufugaji holela na uharibifu
wa misitu zimekuwa zikichangia mabadiliko ya tabia nchi ikiwemo kubadilika kwa
misimu ya mvua hali ambayo ni hatari.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment