WANASAYANSI nchini wamemtaka Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
(Mazingira), Theresia Huvinza, kupunguza masharti ya kanuni ya usalama
wa mimea ya mwaka 2009 ambayo imekuwa ikiwabana watafiti na washiriki
kutumia Jene kuweza kuifanya mbegu kustahimili ukame.
Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa mwishoni mwa wiki na mwanasayansi
mwanamke wa kwanza Tanzania, Roshen Abdallah kwa niaba ya wanasayansi,
alipozungumza na waandishi wa habari kwenye ziara ya kutembelea kituo
cha utafiti wa kilimo Makutupora mkoani hapa.
Alisema lengo lao ni kuwapatia wakulima teknolojia mpya na ya kisasa
zaidi kupata mbegu sahihi na bora inayostahimili hali ya hewa ya aina
yoyote.
Alieleza kama waziri huyo atakubali kubadilisha kanuni hiyo na
wakulima kutumia mbegu za mazao yaliyoboreshwa kutumia viini tete kwa
njia ya uandisi, Jeni (GMO), taifa halitayumba tena kwa uhaba wa
chakula.
Kanuni hiyo ya mimea ya mwaka 2009 inasema kukiwepo madhara yoyote ya
kimazingira yatakayosababishwa na mbegu, atawajibishwa kuanzia mwenye
kiwanda, aliyesambaza mbegu, aliyefanya utafiti na walioshirikiana nao.
“Kiukweli watafiti kutoka nchi za wenzetu wanaogopa kuja kushirikiana
na sisi kutokana na kanuni hii kuwa ngumu, na utafiti kama huu huwezi
kuufanya wewe mwenyewe, lazima kupata ushirikiano na watu kutoka nje,”
alisema.
Pia alisema nchi zinazoendelea wanatumia Jeni hiyo ambayo imeshafanyiwa utafiti kwa miaka 30 iliyopita.
Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima, alisema
wizara yake inataka kuona kilimo nchini kinakuwa cha ajira ya kudumu
kwa wakulima.
Aliwataka watafiti kuendelea na uchunguzi wa kina, ili kupata mbegu bora ya kilimo kwa taifa la Tanzania.
Naye Mratibu wa Water Efficient Maize For Africa (WEMA), Dk. Aloice
Kullaya, alisema kama waziri hataiondoa kanuni hiyo ya usalama kwa
mimea, utafiti hautofanyika na itasababisha Tanzania kupata gharama
kununua mbegu nchi jirani.
Chanzo;Tanzania Daima
|
0 comments:
Post a Comment