Home » » Asakwa kwa kutorosha,kubaka mwanafunzi

Asakwa kwa kutorosha,kubaka mwanafunzi

Wakati Tanzania ikiungana na mataifa mengine kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili na unyayasaji wa kijinsia, mtoto mwenye umri wa miaka 14 (jina linahifadhiwa) mkazi kijiji cha Chinangali mpakani mwa Kibaigwa, Wilaya ya Kongwa, Mkoa wa Dodoma, amebakwa na kulawitiwa kwa muda wa wiki mbili.

Akizungumza jana na NIPASHE, Mhudumu wa Shirika la lisilo la Kiserikali linalopinga ukatili wa kijinsia na watoto (Afnet) kwa kushirikiana na Tunajali, Mnemelwa Simba, alisema tukio hilo lilitokea katika kijiji hicho hivi karibuni.

Simba alisema wazazi wa mtoto huyo walifika kwa mhudumu huyo kuomba ushauri baada ya kuona mtuhumiwa wa ukatili huo akiwa hajachukuliwa hatua stahiki za kisheria na vyombo husika.

Alisema mtoto huyo, ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule ya sekondari iliyopo Kibaigwa, amelazimika kusitisha masomo ili kupata matibabu kutokana na kufanyiwa ukatili huo.

Alisema mtoto huyo alifungiwa ndani ya nyumba kwa muda huo na mtuhumiwa aliyetambulika kwa jina la Hassan, ambaye ni mgeni katika kijiji hicho anayefanya vibarua vya ujenzi.

 “Mimi namjua huyu. Anatambulika kwa jina la Hassan. Na ni mgeni. Hata mwaka hajamaliza. Na mpaka sasa yupo, ni mtu na akili zake, aliyefanya kitendo hiki,” alisema Simba.

 Alisema wazazi wa mtoto huyo baada ya kumtafuta kwa muda mrefu, walitoa taarifa kwa ulinzi shirikishi ili kumtafuta.Simba alisema baadaye iligundulika kijana huyo akiwa na binti huyo, alimuhamishia katika Kijiji cha Ndurugumi.Alisema walipofika katika kijiji hicho walisikia amehama naye tena.

 Simba alisema mtoto huyo alikutwa katika Kijiji cha Ngomai kwa kaka yake na Hassan. Alisema Hassan alidai kuwa mtoto huyo alipelekwa na mdogo wake.

 Mama mzazi wa mtoto huyo, Suzan Fugusa, alisema ilikuwa siku ya Jumapili mtoto wake alimuaga anaenda kanisani kama ilivyo kawaida.
Alisema baada ya kuona muda umepita na mtoto huyo hajarudi kutoka kanisani walianza kumtafuta.

Fugusa alisema baada ya siku kadhaa kupita, walikwenda kutoa taarifa kwa ulinzi shirikishi na kwa mwenyekiti wa serikali ya mtaa.

“Baada ya kumtafuta katika hivi vijiji na kufanikiwa kumpata mkuu wa mtaa alisema suala hilo ni kubwa na kutuambia twende polisi ambako tulihojiwa na mtuhumiwa alikubali kuwa alimtorosha mtoto huyo,” alisema Fugusa.Alisema polisi waliwataka kwenda hospitali kufanyiwa vipimo.

Fugusa alisema walimpeleka, lakini kulingana na woga wa mtoto huyo, alishindwa kueleza ukweli kuhusu vitendo alivyokuwa akifanyiwa.

 “Baada ya kumpima ukimwi na mimba tukarudi nyumbani. Na mara baada ya kurudi akiwa na bibi yake, alienda kujisaidia.
Ndipo haja zote zikawa zinatoka kwa pamoja. Tukarudi hospitali tena. Tulipoona mambo tofauti, alipimwa akagundulika kweli aliingiliwa kinyume cha maumbile na kuanza matibabu ambayo anaendelea mpaka sasa,” alisema Suzan na kuongeza:

 “Tumetumia gharama nyingi kumtafuta mtoto wetu mpaka kumfuata. Na hii kesi ilishafika mahakamani isipokuwa hukumu imetolewa haraka kabla hatujapeleka ripoti ya pili ya daktari iliyogundua ameingiliwa na mtuhumiwa yupo nje hata hatuelewi tuanzie wapi. ”

Kwa upande wake, mtoto huyo alisema siku ya tukio alikuwa akitoka kanisani na kukutana na kijana huyo, ambaye alimwambia waende nyumbani.
Alisema baada ya kufika nyumbani kwa Hassan, alimzuia kurudi  nyumbani kwao na kumfungia ndani na kuanza kumuingilia kinyume cha maumbile kila kijiji walichokuwa wakienda.

“Kwa sasa naendelea na matibabu. Nimesitisha masomo mpaka nitakapopona. Maana niliumizwa. Bado nasikia maumivu makali,” alisema mtoto huyo.

Akizungumza kwa njia ya simu na NIPASHE,  Mkuu wa Kituo cha Polisi Kibaigwa, Inspekta Beda Msoma, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
 Msoma alisema jalada lilifunguliwa kituoni hapo kwa hati ya mashitaka ya kubaka KBG/247/2013.

Alisema kesi hiyo ilikuwa na ushahidi wa kutosha na haelewi kwa nini mtuhumiwa ameachiwa huru, hivyo ataifuatilia kwa mpelelezi wake kuona kwa nini iliamuliwa hivyo.
“Hii kesi naijua ilivyokuja kuripotiwa. Nilifanya jitihada zote. Nikafanikiwa kuifikisha mahakamani ikiwa na ushahidi wa kutosha. Sasa nashangaa kusikia eti yupo huru. 

Iliamuliwa vipi wakati ilikuwa na vithibitisho… Huyu binti nilimpeleka akafanyiwa councelling (ushauri) kwa madaktari wakishirikiana na ustawi wa jamii,” alisema Inspekta Msoma.

Alisema mtoto huyo alipimwa na kugundulika kuwa alibakwa.

Msoma alisema baada ya siku mbili, bibi ya mtoto huyo alirudi polisi na kudai kuwa ameona hali tofauti ndipo akapimwa tena na kubainika aliingiliwa pia kinyume cha maumbile.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa