Dodoma.Kambi ya Rasmi ya Upinzani Bungeni
imetaka Muswada wa Kura ya Maoni uondolewe bungeni hadi hapo Bunge
litakapofanya marekebisho ya Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwa kuwa unapingana nayo.
Awali, muswada huo ulikuwa ujadiliwe katika
Mkutano wa 12 wa Bunge lakini uliahirishwa kutokana na wajumbe wa Kamati
ya Katiba, Sheria na Utawala ya Bunge wanaotoka Zanzibar kupinga vikali
kura ya maoni kupigwa visiwani humo kwa kuwa tayari huko kuna sheria
hiyo.
Akiwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni jana, Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria, Tundu Lissu alisema
katika Katiba ya sasa, hakuna mahali ambako kura ya maoni inatajwa.
Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki
alisema tofauti na Katiba ya Jamhuri, Katiba ya Zanzibar imetambua kura
ya maoni kwa kuitaja rasmi katika Katiba na kuiwekea utaratibu.
“Kwa maoni ya kambi ya upinzani, Serikali ya CCM
inaogopa kufungua mjadala wa marekebisho ya Katiba ili kuruhusu kura ya
maoni kwa hofu kuwa mjadala huo, utapanuliwa kwa kuhoji uhuru wa Tume ya
Uchaguzi katika kuendesha na kusimamia uchaguzi,” alisema.
Alisema hofu ya CCM haiwezi kukubaliwa na Bunge kama sababu ya msingi ya kutunga sheria ambazo zinapingana na Katiba.
“Kwani kwa kufanya hivyo itakuwa sawa na kubariki
ukiukwaji wa Katiba ambao wabunge wote tuliopo ndani ya ukumbi huu
tuliapa kuhifadhi, kuilinda na kuitetea,” alisema Lissu ambaye pia ni
Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani bungeni.
Awali, akiwasilisha muswada huo bungeni kwa niaba
ya Waziri Mkuu, Waziri wa Nchi (Ofisi ya Waziri Mkuu), Sera, Uratibu na
Bunge, William Lukuvi alisema: “Ili kuepuka mkanganyiko unaojitokeza
iwapo sheria za uchaguzi zilizopo zitatumika kusimamia uendeshaji wa
kura ya maoni, Serikali imeona umuhimu wa kutumia kura ya maoni kwenye
mchakato wa kutunga Katiba Mpya.
“Sheria hii si ya kudumu na itafikia ukomo wake,
mara tu baada ya Katiba Mpya kupatikana na haya ndiyo madhumuni makuu ya
kupendekeza kutungwa kwa sheria hii ya kura ya maoni,” alisema.
Alisema mpigakura aliyesajiliwa katika Daftari la
Kudumu la Wapiga Kura la Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), au Daftari la
Kudumu la Wapiga Kura la Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), atakuwa na
haki ya kupiga kura ya maoni.
Kamati
Kwa upande wake, Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria
na Utawala, imeshauri muda wa kukata rufaa kuongezwa hadi siku saba
badala ya tano zilizopendekezwa katika muswada huo. Mwenyekiti wa Kamati
hiyo, Pindi Chana alisema Ibara ya 45 ya muswada huo, inaweka masharti
kwa kamati ya kura ya maoni ambayo haikuridhika na uamuzi wa mahakama ya
chini, kuwasilisha rufaa yake ndani ya siku tano tangu tarehe iliyopata
nakala ya hukumu.
Kamati hiyo pia imeshauri Daftari la Kudumu la Wapiga Kura
lianze kuboreshwa kwa sababu vijana wengi wamefikisha umri wa kupiga
kura na hawajaandikishwa.
Chana alisema kamati inaunga mkono mapendekezo ya
muswada huo kuwa kura zitangazwe ndani ya saa 72 tangu kufungwa kwa
vituo vya kupigia kura.
“Kamati inashauri Serikali kuandaa vifaa vya
kisasa na kuwajengea uwezo watendaji wa tume zote mbili ili waweze
kumudu usimamizi wa mchakato wa upigaji wa kura ya maoni kwa weledi na
umahiri wa hali ya juu,” alisema. Aidha, alisema kamati inaunga mkono
mapendekezo ya muswada huo kuwa matokeo ya kura ya maoni yataamuliwa kwa
kigezo cha asilimia 50 ya kura halali zilizopigwa za kuunga mkono swali
la kura ya maoni kwa pande zote mbili za Muungano.
“Ibara ya 34(2) inaweka sharti la wingi wa kura
halali zilizopigwa katika suala la kura ya maoni kuwa ndilo litakaloamua
kuhusu kukubalika au kutokukubalika kwa katiba inayopendekezwa. Kamati
inaunga mkono masharti haya kwa kuwa uamuzi wa wananchi ndiyo wa mwisho
kuhusu jambo kubwa na nyeti kama la Katiba,” alisema Chana.
Wabunge Z’bar wapinga
Utaratibu wa kuwatumia masheha katika uandikishaji
wa vitambulisho vya ukaazi Zanzibar umezua mjadala mkali bungeni baada
ya wabunge wa CUF, kupinga kutumika katika kuwapata wapiga kura wa
Katiba Mpya.
Akichangia Muswada wa Sheria ya Kura ya Maoni wa
mwaka 2013, Mbunge wa Chakechake, Mussa Haji Kombo alitaka kufutwa kwa
kipengele kinachotaka kutumika kwa Daftari la Wapiga Kura la Zanzibar
katika kupiga kura za maoni kwa kuwa kitawanyima haki Watanzania ambao
hawakuandikishwa kutokana na kunyimwa vitambulisho vya ukaazi na
masheha.
“Msitugawe kwa kutubagua, leo hii mtu
anayeandikishwa Tabora (katika daftari la wapiga kura) haulizwi
kitambulisho cha ukaazi lakini wa Micheweni haandikishwi bila kuwa na
kitambulisho cha ukaazi,” alisema. “Kuna danadana nyingi katika
uandikishaji wa vitambulisho vya ukaazi lakini watoto wa miaka 12 wa
wanachama wa CCM wameshapata vitambulisho… zoezi hili ni muhimu
tutaliharibu kwa kufuata matakwa ya vyama,” alisema Riziki Omary Juma
(Viti Maalumu).
Mbunge wa Mkoani, Ally Khamis Seif, alishauri
kuanzishwa kwa daftari lingine la wapiga kura ambalo halitahusisha
masharti ya kuwa na vitambulisho vya ukaazi ili kuwapa nafasi
Wazanzibari wote kupiga kura katika mchakato huo.
“Kama mimi Sheha wangu wa Konde alininyima
kitambulisho cha ukaazi kama ya Mbunge yamekuwa hayo je, Watanzania wa
kawaida? Hili jambo litatuletea taabu katika maamuzi haya magumu
tunayoyafanya, tuache kutumia daftari la wapiga kura la Zanzibar lile si
daftari lile ni uchochezi litatuletea taabu,” aliongeza Mbunge wa
Konde, Khatibu Said Haji.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment