Home » » CAG kuchunguza kashfa posho za safari za wabunge

CAG kuchunguza kashfa posho za safari za wabunge

Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM), Mwigulu Nchemba, akizungumza bungeni mjini Dodoma jana
 
Kashfa ya baadhi ya wabunge kukatisha safari za kikazi nje ya nchi baada ya kuchukua fedha za safari na posho limewatia aibu na kutikisha bunge jana asubuhi huku Bunge likisema suala hilo limefikishwa ngazi ya utawala na kuwataka waliochukua posho hizo kuzirudisha.
Sakata hilo liliibuliwa bungeni na Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM), Mwigulu Nchemba, wakati akiomba mwongozo kwa mwenyekiti wa kikao hicho, Mussa Zungu Azzan (Ilala – CCM) baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu.

Katika mwongozo wake, Mwigulu alitaka kujua hatua ambazo bunge linachukua dhidi ya wabunge wachache ambao wanachukua fedha bila kwenda safari za kikazi suala ambalo alisema linawadhalilisha wabunge.

“Hivi karibuni kumekuwa na taarifa kwenye magazeti kwamba baadhi ya wabunge waliopewa safari za kikazi nje ya nchi wamechukua fedha lakini wameshindwa kwenda huko na wengine wamekatisha safari hizo.

“Magazeti yameandika kwamba wana mahusiano, mimi sipendi kwenda kwenye uhusiano na badala yake  nataka kwenda kwenye taswira ya Bunge na Taifa,” alisema.

“Hili ni suala binafsi, lakini linachafua taswira ya wabunge na kulidhalilisha bunge. Hatua gani zinachukuliwa dhidi yao,” alisema na kuongeza:
“Jambo hili limechukua taswira kama ni bunge lote na limevunja heshima ya Bunge na linatuvunjia heshima, hata watu ambao tuna maadili ya uongozi tunaoliheshimu taifa letu.”

“Lakini mwongozo ninaotaka kuomba ni kwamba kiti chako kinachukua hatua gani stahiki ya kupambanua kwamba mambo yaliyofanywa na mbunge binafsi na yashughuhulikiwe kwa mbunge binafsi mwenyewe kuliko kupanga taswira bunge zima tuonekane ni wa hovyo,” alisema.

Wakati Mwigulu akizungumza wabunge wengi wa CCM walionekana kupiga makofi hali ambayo iliwamfanya Mbunge wa Mbozi Magharibi (Chadema), David Silinde, kusimama na kusema maelezo ya Mwigulu yanaonyesha kuwa suala hilo ni la  wapinzani peke yake, jambo ambalo siyo kweli.

Alisema wabunge wote wa CCM na Upinzani wanahusika katika kashfa hiyo.

Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Mariam Msabaha, aliwaeleza wabunge wenzake kwamba wakianza kutajana wapenzi humo bungeni hakuna atakayesalimika kwani kila mmoja anaye wa kwake.

Alisema anashangaa kumsikia Mwigulu akisema amesoma kwenye magazeti kashfa ya wabunge kuchukua posho na kutokwenda safari wakati hasemi kuhusu habari za mbunge mmoja wa kike (CCM) ambaye ameandikikwa kwenye magazeti pia kuwa ameiba kidani.

Alisema wizi huo nao unalichafua bunge pia na Mwigulu alipaswa kulilalamikia hilo kwa kuwa nao linawachafua wabunge.

 Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Anna Abdallah, aliunga mkono kauli ya Msabaha, akisema masuala hayo ya binafsi hayapaswi kujadiliwa bungeni.

Kwa upande wake Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Kabwe Zitto, alisema Bunge linataratibu zake za namna gani ya kushughulikia masuala kama hayo.

Alisema Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) ambayo yeye ni mwenyekiti wake, imemwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya uchunguzi kuhusu suala hilo na kuwasilisha ripoti yake kwa Spika.

Alisema kama Spika ataona kuwa inafaa taarifa hiyo iwekwe hadharani basi bunge litataarifiwa.

Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azan Zungu, alisema kuwa mwongozo huo utatolewa baadaye.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa