Home » » Ngombale Mwiru awaasa wahitimu vyuo vikuu nchini

Ngombale Mwiru awaasa wahitimu vyuo vikuu nchini

Mwanasiasa mkongwe nchini,Kingunge Ngombale Mwiru
 
Mwanasiasa mkongwe nchini,  Kingunge Ngombale Mwiru amewaasa wahitimu wa vyuo vikuu nchini kuwa wazalendo kwa kupenda nchi yao na raia wenzao.
Aliitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya mahafali ya 48 ya Chuo cha Biashara (CBE) Kampasi ya Dodoma.

Alisema ni vema wahitimu huko waendako wakatambua umuhimu wa kuwa wazalendo, waipende Tanzania, watu wake na mali zao."Wawe waaminifu na wawapende watu na mali zao...hayo mawili tu kuwa waaminifu na wazalendo na ukiwa mzalendo wa kweli hakika utaipenda nchi yako," alisisitiza Kingunge.

Akizungumza katika mahafali hayo kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya Uongozi wa CBE,Profesa Eliuter Mageni, alisema idadi kubwa ya wahitimu wa vyuo vikuu nchini wanaobaki mijni hukosa ajira.

 Kwa mujibu wa Mageni,  utafiti uliofanywa na Taasisi ya National Demographic & Health Survey,  unaonyesha kijana wa mjini ana asilimia 13 ya kutokuajiriwa ikilinganishwa na asilimia 2 ya wa kijijini.

"Kwa sasa asilimia 8.8 ya vijana wa Tanzania hawana ajira na kwamba wahitimu wa Vyuo vya Elimu ya Juu wamejengewa utamaduni wa kusubiri kuajiriwa, " alisema na kuongeza kuwa:

“Chuo cha Elimu ya Biashara kwa muda mrefu kumekuwa na mpango mahsusi wa kuwapika wahitimu kuwa na uwezo wa kujiajiri.”

Alisema  mitaala yote ya chuo hicho imezingatia utoaji wa mafunzo ya ujasiriamali ambayo dhamira yake ni kufanya utafiti, kutoa huduma za ushauri na mbinu za kutafuta masoko na mitaji kwa wajasiriamali.

Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Emmanuel Mjema, alisema tangu CBE ilipoanza mwaka 1966 kumekuwapo na mafanikio makubwa ikiwamo kuongezeka kwa idadi ya wahitimu katika kampasi zote tatu za Dar es Salaam, Dodoma na Mwanza kwa wahitimu 2,279 kutunukiwa vyeti.

Hata hivyo, alisema chuo hicho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo ukosefu wa  madarasa, maktaba kubwa ya kisasa, ofisi za wafanyakazi, upungufu wa wahadhiri na upungufu wa hosteli unaosababishwa na ongezeko kubwa la wanafunzi wanaojiunga na Kampasi ya Dodoma.

Kwa upande wake mgeni rasmi katika mahafali hayo, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara,

Gregory Teu, aliwaasa wahitimu kuepuka tabia sizioendana na maadili ya kitanzania kama vile wizi, rushwa, ubadhirifu wa  mali za umma na matumizi ya dawa za kulevya.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa