Home » » Pinda:Mshahara wangu huu hapa

Pinda:Mshahara wangu huu hapa

Waziri Mkuu,Mizengo Pinda
 
Waziri  Mkuu, Mizengo Pinda, ametangaza bungeni mshahara anaoupata wa Sh. milioni sita kwa mwezi na kusema pia amekuwa ‘fundi mkubwa’ wa kukopa benki na alipozidiwa na benki moja alihamia benki nyingine.
“Kama kuna fundi wa kukopa benki, mimi ni nimekuwa mmoja fundi mkubwa Nimekopa NMB na nilipozidiwa sasa hivi nimehamia Benki ya CRDB…pia nimechukua asilimia 50 ya kiinua mgongo changu baada ya utaratibu kuturuhusu kufanya hivyo. Yote hayo yanatuweka katika unafuu,” alisema.

Alitangaza mshahara wake wakati akijibu swali la nyongeza lililoulizwa na Mbunge wa Mkanyageni, Mohamed Habib Mnyaa (CUF), akitaka kauli ya Pinda kuhusu taarifa za kwenye mitandao ya kijamii zinazodai analipwa kiasi hicho cha fedha na kwamba Rais analipwa Sh. milioni 32.

Awali, katika swali lake la msingi, Mnyaa alitaka kujua kama taarifa hizo ni za kweli na lini Bunge lilipitisha mishahara ya Rais na wa Waziri Mkuu.

Mnyaa alisema Ibara ya 43 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inazungumzia pamoja na mambo mengine masharti ya kazi ya Rais na malipo ya mshahara wake.

Katika majibu yake, Pinda alisema: “Siwezi kujibu vizuri sana. Lakini sijaona mambo haya ya mishahara ya viongozi yanajadiliwa.”

Alisema baada ya sheria hiyo (Ibara 43 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania), kuna sheria nyingine, ambayo ina waratibu wake na pia kuna kanuni zinazotungwa na Menejimenti ya Utumishi wa Umma.

“Kwa kuwa mitandao ya kijamii imesema Rais analipwa Sh. milioni 32 na Waziri Mkuu analipwa Sh. milioni 26, utakubaliana na mimi jambo hili linaenezwa tu bila ukweli wowote.

Labda ni njama tu kutaka kuchafua watu kwa sababu wanazozijua wenyewe,” alisema Pinda.
Aliongeza: “Wapo baada ya kupata taarifa hizo wameanzakusema sasa huyu mbona alisema kuwa ni mtoto wa mkulima, inakuwaje mambo haya?…mshahara wangu ni fedha taslimu za Sh. milioni sita kwa mwezi pamoja na posho ya mke wangu.

Nasema kwa maana ya mimi kiasi ninachokipata…sitamsemea Makamu wa Rais na Rais. Lakini tofauti kati yetu na Makamu wa Rais haizidi Sh. milioni moja.”

Alisema anashukuru serikali kwa kuweka utaratibu mzuri wa kuwapa nyumba na chakula bure ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa vizuri zaidi.

Pia alisema anapata posho ya utekelezaji wa shughuli za kazi zake kama Waziri Mkuu ya Sh. 500,000 na posho ya jimbo kama ambavyo wanapata wabunge wengine.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa