Home » » Tusigeuzwe watumwa wa vyama-Mbunge

Tusigeuzwe watumwa wa vyama-Mbunge

MBUNGE wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), amesema siasa za hapa nchini zimejaa utumwa wa vyama vya siasa, badala ya kuangalia uwezo wa mwanasiasa mmoja mmoja.
Machali alitoa kauli hiyo jana mjini Dodoma, wakati wa kongamano la kuadhimisha miaka 52 ya Uhuru lililoandaliwa na Umoja wa Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOMASA).

Alisema umefika wakati wa Watanzania kuacha kuangalia majina ya vyama, badala yake waangalie uwezo wa mwanasiasa hasa vijana wakati wa uchaguzi.

Machali ambaye alikuwa anatoa mada kuhusu vijana na harakati za siasa na maendeleo ya Taifa, aliwataka vijana walioingia katika siasa kuepuka tabia hiyo ya utumwa wa vyama.

“Vijana na wazee wa Tanzania nani katuroga hadi tunakuwa watumwa wa majina ya vyama vyetu bila kusimamia ukweli.

“Tunaona majina ya vyama vyetu ndiyo suluhisho ya matatizo yetu badala ya kuangalia uwezo wa kusimamia hoja,” alisema.

“Wapo wabunge wa CCM ambao ni bora kuliko wa Chadema, wapo wabunge wa Chadema ambao ni bora kuliko wa NCCR-Mageuzi,” alisema.

Alisema utumwa wa siasa ni hatari kuliko wa kidini, hivyo kiongozi achaguliwe kwa kuangalia uwezo wake na sio kuangalia chama chake.

Katika mdahalo huo, Machali alianika wazi mshahara wake kuwa Sh milioni 3.5, ambapo baada ya makato yote anapata Sh milioni 1.6 kwa mwezi.

Kwa upande wake, Rais wa Jopo la Wanataaluma (UDOMASA), Profesa Kalafunja Osaki aliwataka vijana kuwa mashujaa kwa kuipigania nchi yao na kuiga mfano wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela.

Chanzo;Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa