Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
CHAMA
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema propaganda za Katibu
Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bw. Abdulrahman Kinana juu ya mjadala
wa Katiba Mpya unaoendelea bungeni mjini Dodoma, una dhamira ya
kuvuruga mwelekeo wa Bunge hilo na kwenye hatua ya kamati.
Mkurugenzi
wa Habari na Uenezi wa chama hicho, Bw. John Mnyika, aliyasema hayo
jana mjini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya kile
alichokisema Bw. Kinana kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika juzi Dar
es Salaam.
Alisema Rais Jakaya Kikwete alipolihutubia Bunge hilo,
aliharibu mwelekeo wa mjadala huo kwa kuzungumzia mambo yaliyohusu
masilahi ya CCM lakini hali ikapoa baada ya wadau mbalimbali kujadili
hotuba hiyo na kutofautiana na Rais kwenye mambo yanayohusu mchakato
mzima wa katiba.
“CCM imeamua kufanya propaganda nje ya Bunge hili
kwa kuitisha mkutano wenye lengo la kumpongeza Rais Kikwete kwa hotuba
yake jambo ambalo ni sawa na kuurudisha tena mjadala kuhusu msimamo wa
Rais bungeni.
“Ifahamike kuwa, ule haukuwa msimamo binafsi wa Rais
bali wa CCM na ushahidi upo katika waraka wao wa siri uliowasilishwa
kwenye Kikao cha Halmashauri Kuu,” alisema Bw. Mnyika.
Aliongeza
kuwa, katika waraka huo CCM imesema muundo wa Muungano ndio moyo wa
rasimu na ndio unaoamua ibara nyingine ambapo chama hicho kinafahamu
ukubwa wa muundo kwenye mjadala wa Katiba, lakini bado wanawadangaya
wananchi.
“Maoni ya Watanzania yanataka kubadilishwa ili yaendane na
sera ya CCM...sisi tutaendelea kusimamia msimamo na maoni ya wananchi,
mkutano wa Kinana aliofanya juzi, umeonesha wazi kuwa chama chake
kimeanza kuiponda Tume ya Mabadiliko ya Katiba,” alisema.
Bw. Mnyika
alisema tume hiyo ilikusanya maoni ya muundo wa Serikali tatu hivyo CCM
imeishiwa hoja kwa kuona kuwa Rasimu ya Pili ya Katiba imezingatia
msimamo walioutoa wananchi si vinginevyo.
Aliwataka Watanzania
kufahamu kuwa, rasimu hiyo ni matokeo ya uchambuzi wa wataalamu na
wananchi wenyewe hivyo CHADEMA haitakuwa tayari kukwamisha mchakato huo
ikitambua kuwa tume hiyo haikuwa ya mtu mmoja na maoni waliyotoa yapo
sahihi.
Aliwahadharisha wajumbe wa Bunge hilo kutoka CCM,
kuhakikisha hawaligeuzi kuwa sehemu ya kuwajadili waliotoa hoja zao juu
ya Rasimu ya Katiba na kutopeleka katika kamati zao agenda iliyosemwa na
Kinana.
“CCM isiseme maoni ya Jaji mstaafu Joseph Warioba yawekwe
pembeni kwa kuwa hayakuzingatia maoni ya mabaraza huku ni kuvuruga
mjadala mzima wa katiba,” alisema.
Bw. Mnyika alisema, katika
mkutano huo Bw. Kinana alidai haoni umuhimu wa Katiba Mpya kwani Katiba
ya zamani watu wengi hawaijui na kusisitiza hata ikiandikwa itaishia
kabatini jambo ambalo ni baya kusemwa na kiongozi wa CCM.
Alisema
kauli hiyo ni ishara tosha kuwa kuna tatizo kubwa nchini ambalo
linashuhudiwa na waraka wa chama hicho ambao unakiri kuwa kuna tatizo la
kuvunjwa kwa matakwa ya katiba hivyo kukiri wazi kuwa hakiheshimu
utawala wa kikatiba.
Chanzo;Majira
0 comments:
Post a Comment