Home » » MAPAMBANO MJADALA WA RASIMU LEO

MAPAMBANO MJADALA WA RASIMU LEO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Kaimu Mwenyekiti wa Ukawa,John Mnyika.
Kamati  12 zilizoundwa na Bunge Maalum la Katiba leo zinatarajiwa kuanza kujadili Rasimu ya Katiba kwa kuanza na Sura ya Kwanza na  Sita, huku Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ukidai kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinataka kupenyeza maoni yake na kwamba watapambana na njama hizo.

Makamu Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samia Suluhu Hassan, alisema kuwa leo asubuhi Wajumbe wa Bunge hilo watakutana Bungeni kwa ajili ya kupangiwa utaratibu kabla ya kwenda kwenye kumbi walizopangiwa kukaa kama kamati.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta, alisema baada ya Bunge kuridhia Kanuni ya 37 na 38 ya upigaji kura, leo Kamati hizo zitaanza kujadili Sura ya kwanza na sura ya sita ya Rasimu ya Katiba.

Sura ya Kwanza ya Rasimu inazungumzia Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo kipengele 1(1) kinasema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi shirikishi lenye mamlaka kamili ambalo limetokana na Muungano wa nchi mbili za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya watu wa Zanzibar, ambazo kabla ya Hati ya Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964, zilikuwa nchi huru.

Aidha, Sura ya Sita, inazungumzia Muundo wa Jamhuri ya Muungano  ambapo kipengele 60(1) kinasema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakuwa na muundao wa shirikisho lenye serikali tatu ambazo ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Tanganyka.

Kwa mujibu wa Sitta, Kamati hizo zitajadili mapendekezo yaliyomo kwenye sura hizo na mapendekezo hayo yatawasilishwa Bungeni kwa ajili ya kupigiwa kura za “Ndiyo” na “Hapana” kwa kuitwa majina au kwa kura ya Siri kama ilivyokubaliwa katika Kamati ya Maridhiano na kupitishwa na Bunge hilo mwishoni mwa wiki.

Suala la Muundo wa Serikali tatu na Muungano, limekuwa likileta mjadala mkubwa katika kuamua namna ya kupigia kura wakati Wajumbe wakitunga Kanuni, hatua iliyosababisha Kanuni hiyo kuwekwa kiporo na hatimaye kufikia maridhiano ya kutumia kura zote mbili za Wazi na Siri baada ya kutokea mvutano mkubwa.

Maridhiano yaliyofikiwa mwishoni mwa wiki yamesaidia Bunge hilo kupiga hatua mbele na kufanikisha kuanza kuijadili Rasimu hiyo.

 Wakati Bunge hilo linaanza kujadili sura za Rasimu ya Katiba mpya, Ukawa umedai kunasa waraka wa siri kutoka CCM  uliopangwa kupenyezwa ili uweze kujadiliwa katika kamati badala ya maoni ya wananchi, mabaraza na Taasisi mbalimbali.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Mwenyekiti wa Ukawa, John Mnyika, alisema kuwa waraka huo umenaswa na Wajumbe wa Bunge hilo la Katiba kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ukiweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha maoni ya CCM yanapewa nafasi na kujadiliwa katika kamati ya kuchambua rasimu hiyo.

Mnyika alidai kuwa waraka huo waliunasa juzi ukiwa na lengo kuingiza maoni ya CCM kama ndio maoni ya wananchi na Taasisi  katika sura ya kwanza hadi ya sita ambazo alisema ndizo moyo wa Katiba hiyo.

Mnyika ambaye alisema lengo la waraka huo ni kutaka kufanya njama kuhusu maoni ya mabaraza mengine yaonekane hayana uzito isipokuwa maoni ya Kamati za  kata ambazo ziliundwa na wenyeviti wa kamati za vijiji na madiwani  ambao wajumbe wake kwa asilimia 80  wanatoka CCM  kinyume na maoni yaliyotolewa na wananchi kwa iliyokuwa tume ya Mabadiliko ya Katiba wakati wa kukusanya maoni nchi nzima.

“Ni vizuri nikawaeleza Watanzania wakafahamu  tutakapoanza kuingia katika kamati na hatua za Bunge lenyewe, CCM  wanataka kuingiza maoni yao na kuacha maoni ya mabaraza mengine  ndio yawe  maoni ya wananchi ili waweze kuingiza katika kujadili rasimu hiyo kinyume na rasimu aliyoleta Jaji Warioba,” alidai Mnyika.

Alidai kuwa hivi sasa tayari pilikapilika zimeanza za kuwatafuta  baadhi ya Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba ili kuwashawishi kwa chochote waweze kukubali kupitisha mapendekezo ya CCM wakati wa kujadili sura ya kwanza na sita katika rasimu inayoanza kujadiliwa leo.

Alisema kuwa Waraka huo una lengo la  kuupuuza maoni yaliyotolewa na wananchi kwa tume ilipopita kukusanya maoni na kutoa mapendekezo liliwamo la kuundwa kwa serikali tatu.

Mnyika alidai miongoni mwa mambo yaliyomo kwenye wa waraka huo ni  CCM imependekeza kuwa mfumo wa Serikali mbili ufanyiwe marekebisho ambayo yatashughulikia changamato zilizopo, marekebisho hayo katika sura ya nne (4) ni pamoja na iwepo tume ya usimamizi na uratibu wa mambo Muungano kikatiba na uendeshaji wake ulingane na mwenendo wa sasa wa vikao vya pamoja vya kero, uratibu na usimamizi wa masuala ya Muungano uweke kisheria na tume ipewe mamlaka ya kuzisimamia taasisi zote za Muungano katika makubaliano yatakayofikiwa na pande zote mbili.

Kwa upande wa Mawaziri katika Serikali ya Muungano, waraka huo wa CCM imependekeza Wajumbe wa Bunge la Muungano wanaweza kuwa Mawaziri wa Wizara za mambo ya Muungano tu, wizara zisizo za muungano ziongozwe na wabunge wanaotoka Tanzania bara.

Alisema kuwa wajumbe hao kutoka upinzani wamejipanga kusimamia maoni ya wananchi kuhakikisha wanapata Katiba bora huku akitaka wananchi kuwahoji Wabunge wao kuwa wapo katika kutea wananchi au kusimamia maslahi ya vyama vyao.

Mnyika ambaye alisema kuwa iwapo CCM kupitia Wajumbe wake walio wengi watalazimisha kuingiza mapendekezo hayo yanayotokana na maelekezo ya Chama chao Wajumbe kutoka kambi ya Upinzani watafanya maamuzi magumu ambayo hata hivyo, hakuyaeleza.

Akizungumzia kuhusu hotuba ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, kuhusu amepata taarifa kuwa kuna Baadhi ya Wajumbe wa Katiba wamepanga kuvuruga amani ya nchi, alisema hizo ni propaganda zake na anapaswa kuwataja hao watu na iwapo hatawataja kutakuwa na muelekeo kuwa CCM ina  mipango ya kuvuruga mchakato wa Katiba kwa  kuandaa mazingira yake.

Hakuna kiongozi wa CCM aliyepatikana jana jioni kuzungumzia madai hayo kwa kuwa  simu za Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye na Kinana zilikuwa zinaita bila majibu.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa