Home » » WAJUMBE WANAWAKEKULALAMIKA KWA SITTA

WAJUMBE WANAWAKEKULALAMIKA KWA SITTA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Mwenyekiti umoja wa Wabunge Wanawake Tanzania (TWGP),Anna Abdallah
Umoja  wa Wabunge Wanawake Tanzania (TWGP)  unakusudia kumwandikia Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta, kupinga lugha za udhalilishaji dhini ya  wanawake ndani ya Bunge hilo.
Mwenyekiti wa Umoja huo, Anna Abdallah, alisema hayo jana kwenye semina ya wanawake wa Bunge hilo kuhusu mambo ya Katiba, iliyofanyika mjini hapa.

Alisema juzi alifuatwa na mtu mmoja na kumuuliza wanawake ndani ya Bunge wanafanya nini wakati wanawake wenzao wanaposimama kuchangia na kutolewa lugha za kudhalilisha, wanakaa kimya.

“Mimi sikusikia, lakini kuna watu wengi wamesema wamesikia, tena ilikuwa sauti ya mwanaume, kwa kweli hatuwezi kukaa kimya lazima tumuombe akemee,” alisema.
Alisema kuwa Umoja huo utamwandikia barua Mwenyekiti kumuomba akemee lugha za udhalilishaji dhidi ya wanawake.

Baadhi ya Wajumbe wa semina hiyo walisema kuwa walisikia sauti ya mjumbe mwanaume ikimwambia mjumbe aliyekuwa akichangia mjadala ndani ya ukumbi huo kuwa aende kuolewa.

Naye Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Anne Makinda, aliwataka wanawake kuacha tabia ya kuzomea wanapokuwa kwenye kamati za kujadili Rasimu,
“Zile tabia ya kuzomea zomea wakati tukiwa kwenye ukumbi tuziache, tuingie kazini na watuone tuko kazini,” alisema.

Dk  Zainab Gama, aliwataka wanawake wasitetereke wanapotukanwa ndani ya ukumbi na kutoa mfano wa yeye na mjumbe mwingine Dk. Ave Maria Semakafu, kutukanwa matusi ya nguoni, lakini hawakutetereka na wale waliowatukana hivi sasa wanawaheshimu.

Lucy Nkya, alisema lugha za matusi kwenye magari ya umma ziangaliwe zinawekwaje kwenye Katiba  ili kuzikomesha.

Mwishoni mwa wiki mmoja wa Wajumbe hao, Teddy Ladslaus Patrick, aliyekuwa akichangia mjadala na baadaye kutaja umri wake, sauti ya kiume ya mjumbe mmoja ilisikika katika kipaza sauti ikisema “Unafaa kuolewa”.

Anna, alisema lugha hizo zinaweza kuwasababishia wajumbe wengine wanawake kuwa na hofu ya kuchangia kwa sababu ya kudhalilishwa.

Awali akifungua semina hiyo, Anna aliwataka Wajumbe wanawake wa bunge hilo  kuwa na sauti moja na kuhakikisha haki zao zinapatikana.

“Sauti ya wanawake iwe moja katika masuala yanayohusu wanawake Kwenye Katiba,” alisema. Anna Kilango, alisema, wanawake walio kwenye majimbo wameanza kupata upinzani, na kwamba kuna wanawake wameenda kujikita kwenye majimbo ya wanawake wenzao na kudhoofisha nia ya kupata idadi ya kupata majimbo mengi kwa wanawake kwa asilimia ya 50/50.
 
SOURCE: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa