Home » » HUVISA, CHIPAKA WAKWAMA KUREJESHA FOMU

HUVISA, CHIPAKA WAKWAMA KUREJESHA FOMU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
John Chipaka
 
Wajumbe wawili wa Bunge Maalum la Katiba ambao waliomba nafasi za kugombea uenyekiti, wameshindwa kurudisha fomu za kugombea nafasi hiyo na hivyo kukosa sifa za kugombea.
 Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi yake mjini Dodoma, Katibu wa bunge Dk. Thomas Kashililah aliwataja waliojitoa ni Dk Terezya Huvisa na John Chipaka.

Alisema kanuni za Bunge zilitaka hadi  leo (jana) majira ya saa 4 asubuhi wote wawe wamerejesha fomu zao, lakini wajumbe hao  walishindwa kufanya hivyo.
 Aliwataja wajumbe ambao wamerudisha kwa wakati fomu hizo na kuwa na sifa ya kugombea ni Samuel Sitta na Hashimu Rungwe Sipunda ambao ndio waliokuwa wakiendelea na kampeni.

Alisema baada ya kukamilika kwa zoezi hilo kwao, iliwapasa makatibu kuandika majina yao na kuyabandika ili wajumbe waweze kutambua majina na idadi ya wagombea.

Kwa mujibu wa kanuni za bunge hilo, baada kuteuliwa kuwa mgombea, mjumbe haruhusiwi kujitoa tena badala yake wataingia moja kwa moja kwenye uchaguzi.
Alisema fomu za makamu Mwenyekiti zinatarajio kutolewa leo (jana) jioni ambapo uchaguzi wake unatarajia kufanyika leo.

“Tukimpata kesho (leo) Makamu Mwenyekiti, tayari utaratibu wa kumpata Katibu utakuwa umejulikana na ndipo tutajua ni lini hasa Rais atakuja kuzindua bunge,”alisema.

 Hata hivyo, akizungumzia nafasi yake ambayo dhahiri inaonekana atakuwa ni Naibu Katibu, alisema hana shida kwani kazi zote wanafanya kwa ushirikiano mkubwa.

Kanuni za bunge hilo, zinaeleza kuwa ikiwa Mwenyekiti atatoka upande mmoja wa Muungano, Katibu atatoka upande wa pili.
Wajumbe waliojitokeza katika kuwania nafasi ya Mwenyekiti wote wanatoka Tanzania Bara hivyo Naibu Katibu atatoka Bara pia ambako Zanzibar itatoa Katibu.

Wakati huo huo Kashililah alisema kwa uzoefu wake kuwa idadi ya wajumbe waliopo ndani ya bunge hilo, watachukua zaidi ya siku mbili na nusu kwa ajili ya kiapo.

Alisema kuwa dakika alizopewa kila mjumbe kuzitumia na baadhi kusoma kwa taratibu, itakuwa wastani wa siku mbili au mbili na nusu kukamilisha kila kitu.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa