Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
a “Uvumilivu una mwisho wake, ukifika wakati huo tutawaambia Watanzania
nini kinachoendelea na sisi tunakusudia kufanya kitu gani.
Kuna njama. Maneno haya mawili ndiyo yametumiwa na pande mbili
zinazopingana ndani ya Bunge Maalumu la Katiba, kuelezea hali
iliyojitokeza jana wakati wa kikao cha Bunge hilo kuhusu mvutano wa
mabadiliko ya kanuni.
Njama zinazoelezwa na pande hizo ni za kuvuruga
mchakato wa Katiba Mpya, zikirejea yaliyotokea jana jioni ikiwamo
zomeazomea hali iliyomlazimu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba,
Samuel Sitta kuliahirisha Bunge hadi leo jioni.
Baada ya kuahirisha Bunge hilo, Sitta alikutana na
waandishi wa habari na kusema kwamba kuna njama za baadhi ya wanasiasa
kutumia vurugu kuhujumu mchakato wa upatikanaji wa Katiba, badala ya
kujenga hoja.
Bila kuwataja wanasiasa hao, Sitta alisema ikiwa hawataki kuendelea na mchakato huo, basi waondoke na kuwaacha wenye nia njema.
“Wanasiasa hawa wamedhamiria kuvuruga mchakato wa
Katiba, tuhuma ambazo tumetuhumiwa leo na Lissu (Tundu) ni uongo na
uzushi, mimi sihusiki na kupeleka marekebisho ya kanuni kwenye Kamati ya
Kanuni na Haki za Bunge,” alisema Sitta.
Sitta alikuwa anajibu mchango wa mjumbe wa Bunge,
Tundu Lissu alioutoa mapema kwenye kikao cha jioni, akipinga
kilichoelezwa ni njama za kutaka kubadili kanuni kinyemela ili kumsaidia
mwenyekiti kulidhibiti Bunge.
Sitta alisema kwa kuzingatia kanuni ya 59 (1),
Kamati ya Uongozi ina mamlaka ya kupeleka marekebisho ya kanuni ili
kuliwezesha Bunge kufanya kazi vizuri.
Alisema hoja kwamba haiwezekani kufanyika
mabadiliko hata kabla ya kuanza kutumika kanuni, siyo ya msingi kwani
kila kitu kinabadilika kutokana na mazingira yake.
“Kamati ya Uongozi ndiyo ilipeleka waraka wa
mabadiliko ya kanuni kwa Kamati ya Kanuni na Haki kwa kuzingatia kanuni,
lakini hata kabla ya kujadiliwa na kamati husika inaonekana kuna
wajumbe ndiyo wameichukua na kuifikisha bungeni,” alisema Sitta.
Alisema kwa kiasi kikubwa marekebisho ambayo
yangesomwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Pandu Ameir Kificho, yalilenga
kutoa ufumbuzi wa kanuni ya 37 na 38 juu ya upigaji kura ama uwe wa wazi
au siri.
Sitta alisema pamoja na hilo, kulikuwa na
marekebisho ya msingi kama kuweka utaratibu mzuri wa majadiliano katika
kamati pia kuweka utaratibu wa vikao vya Bunge kuanzia Jumatatu hadi
Jumapili.
“Mengi ambayo alikuwa anayasema Lissu kama ni takataka hayakuwapo katika taarifa ya Kificho,” alisema Sitta.
Kauli ya Lissu
Lissu katika mchango wake alibainisha kile
alichoeleza kama ‘njama’ za kuchakachua kanuni, akihoji inawezekanaje
kasoro zikaanza kuonekana wakati kanuni hazijaanza kutumika.
Alisema kanuni zilipitishwa mapema mwezi huu na kiporo pekee kilikuwa ni ile ya 37 na 38 kuhusu upigaji kura.
“Tumeletewa jedwali la marekebisho ambalo
linaonyesha kuna marekebisho katika kanuni ya 14 (1), 32, 33, 35 na zile
za 37 na 38 pamoja na 58(1) (d) zingine ni 63 (1) na 64 na kufutwa kwa
kanuni ya 85, jambo ambalo ni kinyume kabisa na kanuni zetu,” alisema
Lissu.
Mbunge huyo wa Singida Mashariki, alisema
utaratibu wa kurekebisha kanuni umeelezwa katika kifungu cha 87 (2)
kwamba, mjumbe akiona kuna hitaji la kurekebisha kanuni awasilishe
pendekezo kwa mwenyekiti wa Kamati ya Haki na Kanuni na iwapo Mwenyekiti
akiona inafaa atawasilisha mapendekezo hayo bungeni.
“Kanuni hazina hata wiki tatu, hazijaanza kutumika
tayari mmeanza kuzichakachua hivi, kasoro mmezipataje wakati bado
hazijaanza kutumika,” alihoji.
Huku akionyesha marekebisho hayo, Lissu alisema:
“Hizi ni takataka ambazo hatutakubali ziingizwe ndani ya mabadiliko.”
Alisema Kamati ya Uongozi haina mamlaka yoyote juu ya kanuni za Bunge.
Lissu kushtakiwa
Sitta alisema kutokana na lugha alizotumia Lissu
juu yake, anakusudia kumfikisha kwenye Kamati ya Kanuni na Haki za
Bunge. Alisema atatoa utetezi na wale ambao wanamtuhumu wataeleza ili
ukweli ujulikane.
Alisema vurugu za jana jioni, zilipangwa hata
kabla ya kuanza Bunge hilo, kwani hata wajumbe wanaotokana na Ukawa
walisusia kutoa maoni katika Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge.
“Wajumbe wao hata kwenye kamati walikuwa
hawazungumzi na wakati wanatoka walisikika wakisema wataendelea na
mkakati wao wa kufanya vurugu,” alisema Sitta ambaye pia ni Waziri wa
Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Ilivyokuwa
Dalili za kuvunjika kikao hicho zilionekana mapema baada ya
wajumbe kuingia ukumbi kwani baadhi walikuwa kwenye makundi
yaliyoashiria kujipanga kwa jambo lililokuwa mbele yao.
Kwa muda kidogo ukimya ulitawala bungeni baada ya Sitta kuzungumza, kisha ilisikika sauti ikiomba mwongozo.
Mwenyekiti alitoa nafasi kwa Lissu akitimiza ahadi yake aliyokuwa ameitoa asubuhi kabla ya kuahirisha Bunge hilo.
Mapema jana asubuhi, Sitta alikuwa ameahidi kuwa
angetoa nafasi kwa miongozo hata kama ingekuwa 20 au 30 ili kila mtu
aweze kupata kile alichokuwa akikihitaji.
Baada ya Lissu kueleza tuhuma zake, zomea zomea ilianza bungeni kiasi cha kuvuruga na kuondoa utulivu.
Waziri wa Sheria na Katiba wa Zanzibar, Abubakar
Khamis Bakary baada ya kuruhusiwa alisema Bunge linaendeshwa na kanuni
“haiwezekani huko aliko aandike mambo yake na kuyapeleka kwenye kamati
halafu yaletwe bungeni, jambo hili haliwezi kukubalika.”
Alisema Bunge hilo ni lenye hadhi na heshima kubwa lakini kanuni kukiukwa kwa kanuni na sheria husika kunapunguza hadhi yake.
Kauli za wajumbe hao ziliungwa mkono na mjumbe
mwenzao Ismail Jussa ambaye alisema waliopendekeza mabadiliko ya kanuni
walikaa mafichoni kutekeleza azma hayo.
Kwa upande wake Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji
Frederick Werema, akizungumza huku akikatishwa na makofi
yaliyochanganyika na zomeazomea na yeye akielekeza maneno yake kwa
kelele hizo alisikika akisema, “sijazoea kuzomewa” na wakati mwingine
akisema “sijazoea kupigiwa makofi.”
Baada ya utulivu kukosekana, Sitta aliahirisha Bunge hilo ili kwanza wajadiliane kabla ya kuendelea.
Ukawa: Hatoki mtu
Wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)
wamesema wataendelea kupambana ndani ya Bunge Maalumu hadi ipatikane
Katiba nzuri na watakuwa wa mwisho kujitoa katika mchakato huo.
Pia wamebainisha kuwa kukimbia au kujitoa katika mjadala huo ni
sawa na kuwaachia CCM walio wengi kwenye Bunge Maalumu watunge Katiba
wanayoitaka wenyewe na hivyo kuzima mawazo ya wananchi.
Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman Mbowe alitoa msimamo
huo jana katika mkutano na waandishi wa habari huku akiweka tahadhari
kuwa “Uvumilivu una mwisho wake, ukifika wakati huo tutawaambia
Watanzania nini kinachoendelea na sisi tunakusudia kufanya kitu gani.”
Imeandikwa na Mussa Juma, Habel Chidawali na Editha Majura
Mbowe ambaye ni kiongozi wa Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni, alisema kuna dalili zinavyoonyesha kuwa CCM hakina nia
njema ya kuwafanya wananchi wapate Katiba nzuri.
“Hakuna mwendawazimu ambaye anaweza kufanikiwa
kutugombanisha na kutusambaratisha, lazima katika jambo hili tutashinda
na matakwa ya wananchi yatachukua nafasi ndani ya Katiba.”
Kwa upande wake James Mbatia alisema Ukawa haiwezi
kwenda kinyume na wala haitakuwa tayari kuwasaliti wananchi katika yale
ambayo waliyapendekeza kwenye rasimu.
Hotuba za JK, Warioba kutojadiliwa
Matarajio ya wajumbe wa Bunge Maalumu kujadili
hotuba ya Rais Jakaya Kikwete na ile ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko
ya Katiba, Jaji Joseph Warioba yameyeyuka.
Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta alisema
amechukua uamuzi huo baada ya majadiliano ya kina na kuonekana ni kama
kutanguliza mjadala wa Rasimu ya Katiba kabla ya wakati wake.
“Kumbukeni waheshimiwa Rasimu ya Katiba
tutaijadili kwa mpangilio wa sura mbili kama haitafanyika marekebisho ya
kanuni hivyo, tukijadili hotuba hizi, wabunge watajadili mahala popote
panapowahusu na hivyo itaharibu kabisa utaratibu wa kanuni,” alisema
Sitta.
Awali, ilipangwa hotuba hizo kujadiliwa hasa kutokana na hoja mbalimbali za wajumbe kutaka kujadiliwa hutuba hiyo.
Miongoni mwa wajumbe walioomba kujadiliwa kwa
hotuba hizo ni Julius Mtatiro ambaye pia aliomba kurejeshwa kwa Jaji
Warioba kutoa ufafanuzi kuhusu masuala yaliyoibuliwa na Rais Kikwete
Mjumbe mwingine Tundu Lissu aliwaeleza waandishi wa habari kuwa alikuwa
anakusudia kumjibu neno kwa neno Rais Kikwete katika kila hoja kwani
hotuba yake ilikuwa na upungufu.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment