Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Baadhi ya wajumbe wa Bunge la Katiba wakishangilia wakati mjumbe
mwenzao, Joshua Nassari alipounga mkono kimakosa hoja ya kura ya wazi
wakati anatoka upande unaoipinga
Hali ya hewa jana ilichafuka kwenye Bunge la Katiba baada ya
mjumbe Ezekiel Wenje kuwatuhumu Waziri Mkuu Mizengo Pinda na baadhi ya
mawaziri kuwa waliwahonga baadhi ya wajumbe wa kundi la 201.
Katika tuhuma hizo, Wenje alimtaja Waziri Profesa
Jumanne Maghembe, Dk. Shukuru Kawambwa na Gaudensia Kabaka akisema kuwa
walitoa rushwa ya vyakula, maji na vinywaji kwa wajumbe hao ili waunge
mkono msimamo wa serikali mbili.
Kauli hiyo, iliyotolewa katika mjadala wa
mabadiliko ya kanuni, ilisababisha mawaziri hao kunyanyuka kujibu tuhuma
hizo, huku Wenje akisisitiza kuwa aliyoyasema ni kweli tupu.
Vilevile baadhi ya wajumbe wanaotoka katika kundi
hilo walicharuka na kujaribu kujitetea huku mmojawapo akitishia kuwa
iwapo Wenje asingeomba radhi, asingetoka ndani ya Bunge hilo.
Hoja ilipoanzia
Wenje, ambaye pia ni mbunge wa Nyamagana
(Chadema), alianza kwa kueleza kwamba wapinzani “walilia” sana kuwa
Bunge la Katiba lisingekuwa na usawa kutokana na Chama cha Mapinduzi
kuwa na wajumbe wengi, ndipo ikaonekana wapatikane wajumbe wengine 201,
lakini jambo la ajabu ni kwamba walioteuliwa katika kundi hilo asilimia
80 ni makada wa CCM akiwamo mzee maarufu ambaye ameingizwa kama mganga
wa jadi.
Ingawa hakumtaja jina, Wenje alikuwa anamaanisha
kada mkongwe wa CCM, Kingunge Ngombale-Mwiru aliyeteuliwa kupitia kundi
la waganga wa jadi.
Kuhusu rushwa, Wenje alisema:“…Sasa kuna wajumbe
wa kundi la 201 walipelekwa kwa Profesa Maghembe na Dk. Kawambwa
wamepeana rushwa, vikao vingi vilifanyika usiku. Hii haikubaliki.”
Baada ya kauli hiyo ya Wenje, Profesa Maghembe
alisimama ghafla huku akionekana kutaharuki, ambapo Makamu Mwenyekiti
Samia Suluhu Hassan alimpa nafasi ya kujieleza.
Profesa Maghembe alikiri kuwakaribisha baadhi ya
wajumbe wa kundi hilo, akieleza kwamba ilikuwa ni katika hali ya ukarimu
uliozoeleka miongoni mwa jamii ya Kitanzania.
“Kuna kundi lipo hapa ambalo linafanya kazi ya
kudhalilisha wenzao. Ni kweli niliwaalika kwa chakula wajumbe hao kwa
taratibu za kawaida, lakini hakuna mbunge hapa anayeshindwa kujinunulia
chakula, hakuna anayeweza kupewa rushwa.
“Kwa sababu hiyo ninaomba kiti chako kimtake
mjumbe aliyewasilisha hoja hiyo aniombe radhi. Wenje aniombe radhi,”
alisema Profesa Maghembe akiwa katika hali ya hasira, huku kukiwa na
sauti za kuzomea na kushangilia kutoka kwa wajumbe.
Makamu mwenyekiti pia alifanya jitihada za kuwataka wajumbe kuwa
wavumilivu, huku akitoa nafasi kwa Dk. Kawambwa kujieleza akisisitiza
kwamba ni tuhuma nzito.
Kawambwa alisema: “Ni kweli nilikutana nao; ni
wajumbe ambao wanatoka kwenye taasisi zinazojihusisha na masuala ya
elimu, lakini mbona wameshafanya mikutano yao mingine mingi ambayo mimi
hawakuniita. Kama mtu akiwa hana hoja bora akae chini.”
Makamu Mwenyekiti alimtaka Wenje aombe radhi
kutokana na kauli yake, lakini katika hali ya kushangaza mjumbe huyo
alisisitiza kwamba Profesa Maghembe na Dk. Kawambwa wamekiri.
“Maghembe amekiri aliwaita wafugaji na wavuvi
ndiyo waliokula chakula cha rushwa, pia wapo wengine walienda kwa Waziri
Gaudensia Kabaka, kuna ushahidi mama mmoja siwezi kumtaja jina hapa
alikwenda huko akafukuzwa, nitakupa jina lake mwenyekiti baadaye.
Aliambiwa kwamba anatoa siri… hoja iliyojadiliwa huko ilikuwa ni kwamba
msimamo ni wa serikali mbili… rushwa ya chakula, maji na bahasha
walipewa,” alisema Wenje na kusababisha kulipuka kwa kelele zaidi.
Wenje aliongeza kuwa kuna wajumbe wengine walikwenda hadi kwa waziri mkuu ambako walikula, walikunywa hadi saa 7:00 usiku.
Alisema wengine walikwenda kwa Gaudensia Kabaka (Waziri wa Kazi na Ajira) na walikula na kunywa na kupewa bahasha.
Baada ya Wenje kukaa, baadhi ya wajumbe wa kundi
la 201 walichachamaa wakitaka kutetea hadhi yao, akiwamo mjumbe kutoka
kundi la wafugaji, Esther Juma aliyesema hawatendewi haki kama kundi
kusema kwamba walihongwa.
Alisema yeye ana ng’ombe 3,000 na asingeweza
kwenda kupokea rushwa ya chakula na kumtaka mbunge huyo kuwaomba radhi
la sivyo asingetoka mlangoni.
Wakati mjadala huo ukiendelea, mwenyekiti wa
Bunge, Samuel Sitta aliyekuwa ametoka kwa udhuru, alirejea kimya kimya,
na kumtaka Wenje kueleza iwapo anadhani kauli yake haikuwaudhi baadhi ya
wajumbe.
Wenje alikiri kuwa ni kweli baadhi ya wajumbe wameudhika kutokana na ukweli aliosema dhidi yao na kuwaomba radhi kwa ukweli huo.
Kauli hiyo ilimfanya Sitta kutangaza kuwa
anapeleka suala hilo kwenye Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge na uamuzi
utakaotolewa atautangaza bungeni.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment