Home » » Ukawa watishia kujiondoa Bunge la Katiba

Ukawa watishia kujiondoa Bunge la Katiba

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta akiwa katika tafakuri nzito wakati mjumbe wa Bunge hilo, Prof. Ibrahim Lipumba alipokuwa akitoa maelezo ya kukataa kuteuliwa kuwa mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya Bunge hilo, mjini Dodoma jana. Picha/Khalfan Said
Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wametishia kujiondoa kwenye Bunge hilo leo, wakilalamikia muundo wa Kamati za Bunge hilo kuwa  na wenyeviti wengi wanaotoka CCM na upendeleo wa Mwenyekiti kwa chama hicho.
Mtafaruku huo miongoni mwa wabunge unatokana na uchaguzi pamoja na uteuzi wa wenyeviti wa Kamati 12 za Bunge hilo, uliosababisha manung’uniko kutoka kwa wajumbe baada ya Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta, kutangaza majina ya washindi wa uchaguzi wa Wenyeviti na Makamu wenyeviti uliofanyika juzi.

Baada ya uchaguzi pamoja na uteuzi wa Mwenyekiti, wajumbe 16 kati ya 19 wanaounda Kamati ya Uongozi ya Bunge Maalum la Katiba ni wanachama wa CCM, huku watatu waliobaki mmoja akiwakilisha watu wa makundi ya watu wenye mahitaji Maalum na wawili pekee wakiwakilisha vyama vya upinzani.

Sitta alitangaza majina ya wenyeviti wa Kamati za Bunge ambao walichaguliwa kwenye uchaguzi ulofanyika juzi mjini hapa kuwa ni Andrew Chenge, Pandu Ameri Kificho Ummy Mwalimu, Hamad Rashid, Shamsi Vuai Nahodha, Dk. Francis Michael, Christopher Ole Sendeka, Steven Wasira, Brigedia Mstaafu Hassan Ngwilizi, Job Ndugai, Kidawa Hamis Salehe, Anna Abdallah, Anne Kilango Malechela na Paulo Kimiti.

Aidha, ili kukamilisha idadi ya wajumbe 19 wa kamati ya Uongozi ya Bunge, Sitta aliwateua Fakaria Hamis Shomari, Mary Chatanda, Prof. Ibrahim Lipumba, Amon Mpanji na Abuu Juma.

Kati ya wajumbe hao, wanaowakilisha vyama vya upinzani walikuwa ni Hamad Rashid na Prof. Ibrahim Lipumba wote kutoka CUF, licha ya kuwa chama hicho kilishamfukuza uanachama Hamad Rashid.

Baada ya kuahirishwa kwa kikao hicho cha Bunge, Wajumbe wa Ukawa walikutana katika ukumbi wa Pius Msekwa, na kuteua kamati yao ya Uongozi yenye wajumbe 20 kwa ajili ya kujadili suala hilo kwa kina.

Kamati hiyo ilihamia katika moja ya ukumbi ndani ya Jengo la Utawala la Bunge na kufanya kikao kilichochukua takriban saa tano, huku baadhi yao wakiitwa kwenye Kamati ya Kanuni ya Bunge hilo kwa lengo la kutafuta maridhiano juu ya suala hilo.

Wajumbe waliokwenda kwenye Kamati ya Kanuni za Bunge hilo ni James Mbatia na John Mnyika.

Akizungumza na NIPASHE kabla ya kuingia kwenye kikao hicho cha Kamti ya Kanuni, Mbatia alisema kuwa Ukawa inatarajia kutoa uamuzi wa nini kifanyike juu ya suala hilo baada ya kuunganisha mawazo atakayoyapata kwenye Kamati ya Kanuni pamoja na maoni ya kikao cha Ukawa kilichokuwa kikiendelea kwenye Jengo la Utawala.

“Nimewaacha wenzangu wakiendelea na kikao, mimi nakwenda kwenye Kamati ya Kanuni, yale nitakayoyapata huko tutaunganisha na mawazo ya wengu na ndipo tutatoa tamko letu,” alisema Mbatia

Hata hivyo taarifa kutoka kwenye chanzo chetu ndani ya kikao cha Kamati ya Ukawa, zilieleza kuwa Kamati hiyo imeamua wajumbe wake kujitoa kushiriki kwenye Bunge Maalum na kuondoka mjini Dodoma endapo hakutafanyika mabadiliko ya kanuni kwa ajili ya kuwezesha wapinzani kupata uwakilishi kwenye Kamati ya Uongozi wa Bunge.

“Subirini kwa sasa siwezi kuzungumza chochote, lakini kaeni tayari kesho (leo) kuna kitu kikubwa kitatokea kwa wajumbe wanaounda Ukawa kufanya maamuzi magumu baada ya kumaliza kikao cha Kamati ya Kanuni kumalizika na kutueleza walichoazimia,” kilisema chanzo hicho.

Katibu wa Ukawa, Julius Mtatiro, alipoulizwa kuhusiana na maamuzi ya kikao hicho aliwataka waandishi wa habari kuvuta subira ili viongozi wa Ukawa watoe taarifa kwa wajumbe wake na baadaye kutoa taarifa ya uamuzi wa wajumbe kwa waandishi wa habari.

Kwa upande wake Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, Prof. Lipumba aliliambia NIPASHE kuwa baada ya majadiliano ya muda mrefu wamekubaliana kusubiri maamuzi ya Kamati ya Uongozi ya Bunge na ajenda zitakazoletwa leo bungeni ili watoe uamuzi wao.

Hadi gazeti hili linakwenda mitamboni kikao cha Ukawa na kile cha Kamati ya Kanuni za Bunge vilikuwa vikiendelea kwenye kumbi tofauti bungeni mjini Dodoma.
 
CHANZO: NIPASHI

1 comments:

Unknown said...

Kama mambo yanafanyika kiccm bas wapinzan waachieni bunge lao. Halafu wananchi tutawaonyesha. Sita amekuwa hovyo kabisa. Sina iman nae tena!!!

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa