Home » » HATI YA MUUNGANO MOTO

HATI YA MUUNGANO MOTO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
  Msekwa,AG Z�bar waitwa,watoa maelezo
  Wajumbe kupewa nakala iliyoko makahamani
Aliyekuwa Katibu wa Bunge la Tanganyika wakati huo,Pius Msekwa.
Utata uliojitokeza kwenye Hati ya Muungano na kusababisha baadhi ya wajumbe kugoma kujadili Rasimu ya Katiba kutokana na kutoonekana kwa ushahidi wa kisheria wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar kuridhia makubaliano ya Muungano, umesababisha kuitwa na kuhojiwa kwa aliyekuwa Katibu wa Bunge la Tanganyika wakati huo, Pius Msekwa, na Mwanasheria wa Zanzibar Othuman Masoud Othuman. Msekwa na Masoud jana waliitwa na kuhojiwa na Kamati Na. 2 ya Bunge Maalum la Katiba ambayo Mwenyekiti wake ni Shamsi Vuai Nahodha.
Walitakiwa kutoa maelezo juu ya utata uliopo kwenye Sheria ya Makubaliano ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Nahodha alisema kuwa wajumbe wa kamati yake ambao walikuwa wakijadili sura ya kwanza na ya sita za Rasimu ya Katiba zinazohusu muundo wa Muungano, walitilia shaka na kuzua mabishano makali juu ya mambo matano ambayo ndiyo yalisababisha kuitwa kwa Msekwa na Masoud kwenye Kamati yake.

Aliyataja mambo hayo kuwa ni kusainiwa kwa mkataba wa Muungano baina ya Hayati Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume, kuridhiwa kwa Mkataba wa Muungano na Baraza la Mapinduzi, Muundo wa Muungano uliopendekezwa kwenye Mkataba wa Muungano, namna jina la Tanzania lilivyopatikana wakati sheria ya kuridhia Muungano imetaja jina la Tanganyika na Zanzibar na utata wa saini ya Nyerere na Msekwa kwenye hati ya Muungano.

Akifafanua zaidi, Nahodha alisema kuwa baadhi ya wajumbe walidai kuwa saini ya Msekwa aliyosaini kwenye Sheria ya Makubaliano ya Muungano iliyotungwa na Bunge la Tanganyika wakati akiwa Katibu wa Bunge la Tanganyika mwaka 1964, haikuwa ya Msekwa kwa kuwa inatofautiana na saini zake nyingine alizosaini kwenye nyaraka nyingine.

Alisema kuwa baadhi ya wajumbe walipinga kuwa saini iliyokuwa kwenye nakala ya sheria hiyo iliyopelekwa kwenye kamati yake haikuwa ya Msekwa huku pia sheria hiyo ikidaiwa kuchapwa kwa kompyuta ambazo hazikuwapo wakati nchi hizo zikiungana mwaka 1964.

Nahodha alisema mbali na suala la saini ya Msekwa, wajumbe wa kamati yake pia walidai kuwa hakuna ushahidi wowote wa kisheria unaoonyesha kwamba Baraza la Mapinduzi Zanzibar liliridhia makubaliano ya Muungano na hivyo wakahitaji ufafanuzi zaidi wa kisheria juu ya jambo hilo, huku wakitaka waonyeshwe nakala halisi ya sheria iliyotungwa na Baraza la Mapinduzi iliyoridhia makubaliano ya Muungano.
Alisema kuwa katika mabishano hayo, wajumbe wa kamati yake pia walihoji namna lilivyojitokeza jina la Tanzania wakati kwenye sheria ya makubaliano ya Muungano yametajwa majina ya Tanganyika na Zanzibar.

Alisema suala jingine lililotakiwa kufafanuliwa ni aina ya muundo wa Muungano uliopendekezwa wakati wa makubaliano kuwa ni wa shirikisho la nchi mbili au Muungano wa Serikali mbili.

“Hoja hizi ndizo zilizosababisha kamati yangu ione umuhimu wa kuwaalika wageni wetu Msekwa na Mwanasheria wa Zanzibar ili watoe ufafanuzi kwa wajumbe na kujibu maswali yaliyoulizwa,” alisema Nahodha.

Alisema aliyekuwa wa kwanza kuhojiwa alikuwa ni Mwanasheria wa Zanzibar ambaye katika majibu yake alikiri kuwa hata yeye hajawahi kuiona sheria ya makubaliano ya Muungano, ingawa ana amini kuwa sheria hiyo ipo.

Alisema Mwanasheria wa Zanzibar aliieleza kamati kuwa hajawahi kuiona sheria hiyo kwa sababu hakuna mamlaka yoyote iliyowahi kuihoji wala kudai na kwamba ikitokea sheria hiyo ikahitajika ataingia kazini kuitafuta na anao uhakika wa kuipata.

“Mwanasheria ametuthibitishia kuwa hicho kitu ingawa hajakiona, lakini kipo, endapo kitahitajika anaweza akakitafuta na kutuonyesha,” alisema Nahodha.

Kwa mujibu wa Nahodha, Mwanasheria wa Zanzibar alipoulizwa kuhusu mahali ilipo Hati ya Muungano, alisema kuwa hati hiyo ilipelekwa kwenye Umoja wa Mataifa ambako ndiko iliko hadi hivi leo.

Akifafanua zaidi, Nahodha alisema kuwa wakati ule Tanganyika na Zanzibar zilipopata Uhuru, kila moja ilitambuliwa na Umoja wa Mataifa, lakini baada ya kuungana Umoja wa Mataifa ulisimamisha unachama wao ukidai mpaka upate ushahidi wa kisheria ndipo zitambuliwe.

Alisema ili kuuthibitishia Umoja wa Mataifa kuwa nchi hizo zimeungana ilibidi wapelekewe nyaraka ya kisheria, ambayo ni Hati ya Muungano, huku akisema kuwa hati hiyo inapatikana Umoja wa Mataifa na kwamba Mtanzania yeyote anayehitaji kuiona anaweza kwenda huko atapewa.

Akizungumzia majibu ya Msekwa kwenye Kamati hiyo, Nahodha alisema kuwa baada ya kuhojiwa Msekwa alisema kuwa hana wasiwasi na maandishi ya sheria hiyo na kukiri kuwa saini iliyokuwa kwenye sheria hiyo ya makubaliano ya Muungano iliyotungwa na Bunge la Tanganyika wakati huo ilikuwa ni yake.

Akizungumzia jinsi jina la Tanzania lilivyopatikana, Nahodha alisema kuwa sheria ya jina jipya la Tanzania ilipitishwa Desemba 10, 1964 baada ya Serikali kutangaza shindano la kutafuta jina na aliyebuni jina hilo kuibuka mshindi.

Nahodha alisema kuwa baada ya kupata maelezo kutoka kwa Msekwa na Mwanasheria wa Zanzibar, wajumbe waliridhika na kuendelea na majadiliano, na kwamba ana amini kufikia jana saa mbili usiku kamati yake itakuwa imekamilisha kazi ya majadiliano ya sura hizo mbili za Rasimu ya Katiba.

Nahodha alipoulizwa kama na yeye hajawahi kuiona Sheria ya makubaliano ya Muungano iliyotungwa na Baraza la Mapinduzi Zanzibar wakati alishawahi kuwa Waziri  Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, alisema kuwa hata yeye hajawahi kuiona kwa vile wakati huo hapakuwapo na malumbano kama yaliyopo sasa, hivyo hakuona sababu ya kuitafuta.

“Wewe kama wazazi wako hawajafarakana, huna sababu ya kuanza kutafuta cheti chao cha ndoa, wakati ule hayakuwapo malumbano kama yaliyopo hivi leo hivyo na mimi sijawahi kuiona sheria hiyo,” alisema Nahodha.

Kuhusu saini ya Msekwa, Nahodha alisema kwa maoni yake anakubaliana na maudhui yaliyo kwenye sheria hiyo, lakini uhalali wa saini ya Msekwa alidai hana hakika kwa sababu yeye sio mtaalam wa masuala ya saini.

Alisema kama kuna mtu ataendelea kuwa na shaka na saini hiyo anayo haki ya kuichukua na kuipeleka kwa wataalam ili ajiridhishe.
 
WABUNGE KUONYESHWA HATI HALISI
Katika hatua nyingine,  mvutano  mkubwa  wa wajumbe wa Kamati ya Bunge la Maalum la Katiba kudai Hati ya Muungano iliyopelekwa kwenye vikao vilivyoanza juzi, Bunge hilo linafikiria kutoa nakala ya hati hiyo ambayo kwa sasa iko Mahakama Kuu Dar es Salaam.

Baadhi Kamati juzi ziligoma kuanza mjadala wa Rasimu ya Katiba mpya wakidai kuwa hati zilizowasilishwa hazikuwa nakala halisi.
Kwa mujibu wa wajumbe hao hati hizo zilikuwa na saini ya hayati Julius Nyerere pekee bila saini ya muasisi mwingine wa Muungano, hayati Abeid Amani Karume.

Katibu wa Bunge Maalum la Katiba, Yahaya Khamis Hamad, alipoulizwa kuhusu utata huo, alisema kuna changamoto zinazojitokeza kuhusu suala hilo kwa kuwa nakala ya hati hiyo ni moja tu.

Alisema  kitendo cha kuitoa mahakamani na kuileta Dodoma kunaweza kuusababisha kupotea njiani na kuleta balaa zaidi.

“Kuna challenge (changamoto) nyingi kwa sababu hata hiyo copy (nakala) ni iko moja kuitoa mahakamani na kuileta huku, ikipotea njiani itakuwaje,” alisema.

Hata hivyo, alisema kinachofikiriwa kwa sasa ni kuitoa nakala na kwenda kuithibitisha mahakamani au kwa mwanasheria kwa kuwa hakuna namna nyingine.

Juzi wakati wajumbe wa kamati za Bunge hilo wakiwa kwenye vikao vya kujadili Rasimu, baadhi waligoma kuanza kujadili wakidai wapatiwe nakala halisi ya hati ya Muungano.

Katika baadhi ya kamati, ikiwemo Na. 11, Mwenyekiti wake, Anne Kilango, alisema kuwa kamati hiyo ilikuwa na mwanasheria ambaye alitolea ufafanuzi wa hati hiyo na wajumbe wote waliridhika na kuendelea na kikao chao.

Akizungumzia kuhusu muda ulioombwa na wajumbe wa kuongezewa muda wa kujadili sura mbili walizopangiwa kwa siku moja, Hamad alisema kuwa suala hilo haliwezi kuamuliwa na yeye wala kamati.

Alisema kanuni zinaweza kuwekwa kando kuhusu suala la muda mpaka hapo watakaporejea bungeni kwani si katibu wala kamati zinazoweza kuongeza muda.

Imeandikwa na Beatrice Bandawe, Emmanuel Lengwa na Ashton Balaigwa, Dodoma
SOURCE: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa