Home » » WAJUMBE WAVUTANA MBUNGE ASIWE WAZIRI

WAJUMBE WAVUTANA MBUNGE ASIWE WAZIRI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Mwenyekiti wa Kamati namba nane, Job Ndugai
 
Kamati mbili kati ya kumi za Bunge Maalum la Katiba, zimeshindwa kuhimili kishindo cha mvutano kuhusu mbunge kutokuwa waziri.
Hatua hiyo imezilazimu kamati hizo kushindwa kufikia maamuzi na badala yake hoja hiyo itapigiwa kura na maamuzi yake kupelekwa kwenye Bunge kwa ajili ya maamuzi ya mwisho.

Mwenyekiti wa Kamati namba nane, Job Ndugai, akizungumza na waandishi wa habari, jana mjini Dodoma, alisema suala hilo limetikisa kamati yake na linasubiri maamuzi Agosti 21, mwaka huu.

“Wapo wenye msimamo tuendelee kuwa na mawaziri wanaotokana na wabunge na wengine wanapinga kabisa, tutaamua kama kuwa na mgawanyo wa madaraka ikiwamo rais asiwe sehemu ya bunge,” alifafanua.

Sura ya saba, ibara ya 101 (1) ya Rasimu ya Katiba, inasema mtu atateuliwa kuwa waziri au naibu waziri wa serikali ya jamhuri ya muungano ikiwa: (a) ni raia wa kuzaliwa wa jamuhuri ya muungano; (b) awe na shahada ya chuo cha elimu ya juu kinachotambulika kwa mujibu wa sheria za nchi na ana weledi na uzoefu.

Ibara ndogo ya pili inasema watu wafuatao hawatakuwa na sifa ya kuteuliwa kuwa mawaziri au naibu waziri katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano (a) Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Wabunge wa Bunge la Tanganyika, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar au madiwani katika nchi Washirika.

Ndugai ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Uongozi, alisema suala hilo limewekwa kiporo kusubiri upigaji kura na kwamba ni moja ya maeneo yatakayokuwa na maoni ya wengi na wachache.

Mwenyekiti wa Kamati namba 10, Salmin Awadhi Salmin, alisema wajumbe wengi wanapinga wabunge kuwa mawaziri na kutaka mgawanyo wa madaraka kwa kila muhimili ujitegemee na kufanya kazi katika maeneo yao.

“Wanasema mawaziri wengi wanapokuwa ndani ya bunge wanakuwa na msimamo wa serikali zaidi kuliko kwenye majimbo wanayowakilisha, na hivyo wajibu wa serikali kumvuta zaidi na kuwasahau wananchi wake,” alisema.

Alisema wanaotaka mawaziri watokane na wabunge wana hoja kuwa wabunge wanapohitaji ufafanuzi wa jambo kutoka serikalini hukosa kwa kuwa mawaziri wamesafiri au wako kwenye kazi nyingine na hivyo kukosa msaada.

“Wanapokuwa mawaziri ni wabunge, likijitokeza swali lolote anaweza kujibu kwa kuwa wanafanya kazi kwa kushirikiana, lakini kwa mapendekezo ya sasa waziri hatakiwi kushiriki bunge hadi pale atakapohitajika,” alifafanua.

Alisema mahitaji mengi hutokea wakati wa mijadala ya Bunge huku waziri husika akiwa nje ya nchi na Rasimu hiyo ikipendekeza wenyeviti wa kamati kutoa ufafanuzi wakati wanatokana na wabunge.

Mwaka jana, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Shukuru Kawambwa, akitoa maoni yake mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwenye kituo cha kuchukulia maoni cha Soga, wilayani Kibaha, alieleza kuwa Waziri kuwa Mbunge kunanyima wapiga kura uwakilishi.

DENI LA TAIFA
Alisema ibara ya 15 imekuwa na mjadala mkali  kwa kuwa sharti lililopo Serikali ya Zanzibar inapotaka kukopa fedha kwa jambo ambalo siyo la Muungano hadi wapate dhamana ya Serikali ya Muungano.

Ndugai ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya maridhiano, alisema baadhi ya wajumbe walipendekeza kiwango cha mikopo kiwekwe wazi na kupata kibali cha Bunge ambako kuna wawakilishi wa wananchi kwa kuwa deni la taifa litawahusu Watanzania wote.

Alisema kamati hiyo imeangalia uwezekano wa mikopo ya kiasi fulani serikali kulazimika kuomba kibali cha Bunge jambo ambalo litasaidia kuzuia ukuaji wa deni la taifa kwa haraka.

“Badala ya kuruhusu Waziri wa fedha kukopa atakavyo ni lazima kabla lifikishwe Bungeni na kuwekwa wazi zinakopwa kwa sababu gani na zitatumikaje ili kuepusha mikopo kutumika visivyo,” alisema.

Alisema kwa madeni ambayo Jamhuri ndiyo itahesabika mdhamini, inawaweka Watanzania katika madeni makubwa na serikali isipokuwa makini nchi itakuwa katika hali mbaya.

“Mfano leo tumegundua gesi, baadhi ya viongozi wanaweza kwenda kukopa fedha nyingi sana, halafu utakapoanza kuzalisha gesi, unaona wawekezaji wanachukua gesi tu mkihoji mnaelezwa si mlikopa ukifuatilia awamu ya uongozi iliyokopa ilishaondoka madarakani hata namna ya kuulizana inakuwa ngumu,” alisema Ndugai.

MADARAKA YA RAIS
Alisema suala la msingi siyo kumuondolea rais mamlaka ya uteuzi lakini ni kuweka wazi mchakato mzima wa uteuzi kama Katiba ya Kenya inavyotaka mchakato huo kuwa wazi na wananchi kushuhudia aina ya watu wanaoteuliwa.

SURA MPYA
Alisema wamepata mapendekezo ya kuwa na sura mpya ambapo mjumbe Ezekiah Oluochi, amependekeza kuwapo kwa ibara inayozungumzia Tume ya Walimu na nyingine, wengine wakipendekeza kuwapo kwa sura ya ardhi, rasilimali, wakulima na wafugaji..
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa