Home » » WARIOBA: SIUNGI MKONO MAANDAMANO

WARIOBA: SIUNGI MKONO MAANDAMANO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, ametoa ufafanuzi wa kauli yake ya kukutana mtaani, kwamba haimaanishi kuunga mkono maandamano. Akizungumza na gazeti hili jana kwa simu, Warioba alisema kauli yake aliyotoa juzi katika maadhimisho ya miaka 19 tangu kuanzishwa kwa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Dar es Salaam, kwamba ‘tutakutana mtaani’, imetafsiriwa vibaya kwamba anaunga mkono maandamano.
“Imeonekana kwamba nitaungana na watu kwenye maandamano lakini ni vyema ieleweke mimi siamini katika maandamano,” alisema Jaji Warioba.
Alisema kauli yake kwamba ‘tutakutana mtaani’ alimaanisha kutoa ushauri kwa Bunge Maalumu la Katiba, lipeleke Katiba inayopendekezwa kwa wananchi kupitia njia za kutoa elimu.
“Maana yake ni Katiba Inayopendekezwa ipelekwe katika semina, makongamano na vyombo vya habari ili wananchi waielewe kama Tume (ya Marekebisho ya Katiba), ilivyofanya,” alisema.
Katika maadhimisho hayo, Jaji Warioba alisema Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalumu la Katiba imeondoa mambo manne muhimu yaliyokuwa kiini cha kupata Katiba ya mageuzi. Mambo hayo aliyataja ni maadili ya viongozi wa umma, madaraka ya wananchi, mgawanyo wa madaraka na Muungano.
“Bunge Maalumu limeondoa uadilifu, uzalendo, umoja, uwazi, na uwajibikaji kutoka kwenye orodha ya tunu za taifa na kuziweka kwenye misingi ya utawala bora. Kila Mtanzania anatakiwa awe mzalendo, kila Mtanzania anatakiwa kuwa mwadilifu, kila Mtanzania anatakiwa kuuenzi umoja. Inakuwaje mambo haya yahusu utawala tu?” alikaririwa akihoji Warioba.
Pia Warioba alikosoa kuondolewa kwa miiko ya uongozi kwenye Katiba, wakati kila siku viongozi wanalalamika juu ya rushwa na ufisadi, pamoja na fedha za umma kuwekwa kwenye akaunti za benki nje ya nchi.
Hata hivyo moja ya vipengele vinavyotarajiwa kurekebishwa katika Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa, inayotarajiwa kuwasilishwa kesho na kuanza kupigiwa kura, ni suala hilo la miiko ya uongozi na kutajwa kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa na Uhujumu Uchumi.
Marekebisho hayo yanatokana na matakwa ya kamati karibu zote 12 za Bunge Maalumu la Katiba, ambao walitaka yarejeshwe katika Rasimu ya Katiba inayopendekezwa, badala ya kuachiwa katika sheria.
Wamjibu Warioba Kama alivyotarajia Jaji Warioba, kwamba dhana ya kauli yake kwamba ‘tukutane mtaani’ ingetafsiriwa vibaya, baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba waliamua kutumia muda wa kuzungumza machache, kumjibu.
Mjumbe wa Bunge hilo, John Komba, alilalamika kwamba Warioba kila mara amekuwa akiwaingilia wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba katika kazi yao, wakati yeye alipopewa kazi ya kuongoza Tume, aliomba asiingiliwe na ombi hilo likaheshimika.
Komba alisema kwa kuwa Warioba amesema ataingia mtaani na kuwa upande mmoja na wajumbe wa bunge hilo upande mwingine, basi aende ili wakutane. Cheyo Mjumbe John Cheyo, alisema Warioba amefanya kazi nzuri.
Hata hivyo alimwomba akisema kama mzee mwenzake, apumzike ili kazi nzuri aliyoifanya, isiharibike mwishoni.
Katika kuonesha kuwa kuna tafsiri kwamba Warioba amekusudia kuingia katika maandamano, Cheyo alimsihi pia Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ambaye ameitisha maandamano yasiyo na kikomo kupinga Bunge Maalumu la Katiba, afanye mambo mengine na aendelee kupumzika Afrika Kusini, badala ya kuhamasisha maandamano hayo.
Cheyo aliyezungumza katika kundi maalumu la wajumbe wazee, alisisitiza umuhimu wa Mbowe kuacha kuhamasisha wanawake kwa kile alichosema, wakakatwe miguu kwa kuwa hakuna duka la viungo hivyo.
“Acha kuhamasisha vijana ili kutoa kafara ya urais, hakuna kafara hapa...tulisema tuzungumze na Rais Kikwete (Jakaya), anapenda mazungumzo, ni mtu mwenye moyo, mtu wa Mungu pamoja na kumdharau dharau, tukimwendea atatufungulia mlango,” alisema Cheyo.
Wassira, Chenge Mjumbe Stephen Wassira, ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Uhusiano na Uratibu, bila kumtaja Warioba, alisema; “wengine wanasema wanataka kwenda mtaani, mimi nasema sina haja ya kwenda mtaani, ninaishi huko huko.”
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalumu la Katiba, Andrew Chenge, ingawa pia hakutaja jina, alisema hataki malumbano na watu wengine ambao wamemlea katika taaluma ya sheria.
Alitaka Watanzania wasome Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa na Rasimu ya pili ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba mpya na kupima ukweli uko wapi.
Chanzo:Habari Leo 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa