Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WATU 571 hawana mahali pa kuishi baada ya nyumba 391 kuathiriwa na
mafuriko yaliyotokana na mvua zinazoendelea kunyesha mkoani hapa.
Akizungumza katika ziara ya kutathmini athari ya mvua hizo katika
Kijiji cha Mpunguzi wilayani Dodoma jana, mkuu wa wilaya hiyo, Jasmine
Tiseku, alisema nyumba zilizobomoka kabisa ni 164 na jitihada za kuwapa
misaada zinaendelea.
“Vijiji vilivyoathirika ni Mpunguzi A na B, Mkulabi na Makumbulu.
Mvua hii ilianza Januari mosi na kuleta maafa halafu ikarudia tena
Januari 18 hadi sasa. Tunaomba wananchi waondoke kwenye maeneo
hatarishi,” alisema mkuu huyo wa wilaya.
Akizungumza katika eneo hilo, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri
Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Vijana, Jenister Mhagama, alisema
Serikali imetenga msaada wa chakula tani 700 kwa ajili ya walioathirika
na mafuriko katika mkoa huo.
“Tumepanga kuleta chakula cha kutosha kwa walioathirika na mafuriko.
Tutaleta tani 700 na pia tutaleta chakula kingine kiuzwe masokoni kwa
bei nafuu ili kusaidia kupunguza bei ya chakula wakati huu wa mvua,”
alisema Mhagama.
Mbali na chakula, Waziri Mhagama alisema watagawa magodoro kwa familia zilizoathiriwa na mafuriko hayo.
Aliwataka wananchi kuchukua tahadhari na mvua hizo kwa kuhama kwenye
maeneo hatarishi, hasa ya bondeni, huku akisema tayari Kamati ya Maafa
ya Wilaya imeshaanza kufanya tathmini ya uharibifu uliojitokeza.
“Taarifa zilizotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) imesema mwaka
huu kutakuwa na mvua za El-nino, kila mkoa umeathirika na hali hii,
hivyo kila mwananchi ajihadhari kwa kuhama kwenye maeneo hatarishi,”
alisema Mhagama.
Akizungumzia chanzo cha mafuriko hayo, Mhandishi wa Kampuni ya
Technics Construction Group inayojenga daraja la Mto Mpunguzi, Thobias
Kiwando, alisema maji yalikuwa mengi kiasi cha kushindwa kupita kwenye
daraja la mto huo na kupasua tuta linaloyazuia kwenda kwenye makazi ya
watu.
“Hapa kuna makutano ya mikondo mitatu, baada ya kuhamishwa kwa
barabara hii maji yote yanakutana kwenye daraja hili, hivyo yakizidi
ndiyo yanapaswa tuta kama hivi,” alisema Kiwando na kuongeza:
“Ujenzi huu utatumia siku 14 au chini ya hapo na utarudisha tuta kwenye hali yake na kuilinda barabara isiendelee kulika.”
Ziara hiyo pia ilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya
Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Vijana ambaye pia ni Mbunge wa
Dodoma Mjini, Anton Mavunde na mbunge wa viti maalumu wa mkoa huo,
Felister Bula.
CHANZO: MTANZANIA.
0 comments:
Post a Comment