Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Baadhi ya wabunge wa upinzani ambao jana walisusia
kikao cha Bunge, wamesema kashfa tano zilizotikisa serikali ya awamu ya
nne na hali ya kisiasa Zanzibar, ndio msingi wa serikali kukataza
matangazo ya moja kwa moja kurushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania
(TBC).
Mbali na TBC ambayo kutokana sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania (TCRA), inayolazimisha kampuni za ving’amuzi kurusha matangazo
ya televisheni hiyo bure, hali inayofanya ionekane eneo kubwa la nchi,
wabunge hao walisema hata vituo binafsi vya televisheni vinavyorusha
matangazo hayo moja kwa moja, zitazuiwa hivi karibuni.
Vituo vingine vya televisheni vinazorusha matangazo hayo moja kwa moja ni Azam na Star.
Jana, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisisitiza kwamba TBC
haitoonyesha majadiliano ya moja kwa moja ya Bunge kuanzia mkutano huu
wa pili wa Bunge la 11 na badala yake yatarekodiwa na kuonyeshwa usiku.
Juzi Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye,
alisema kipindi hicho kitaonyesha matukio muhimu yaliyojiri bungeni kwa
saa moja licha ya kwamba kuanzia kukatishwa kwa maswali na majibu saa
tano mpaka saa saba mchana kinapoisha kipindi cha asubuhi kabla ya
kuingia tena saa 10:00 jioni mpaka saa 1:45 jioni ni takribani saa saba.
Baadhi ya wabunge wa upinzani waliozungumzia suala hilo, walisema
serikali kusema inakatisha matangazo hayo kwa sababu ya kuongezeka kwa
gharama na kufikia Sh. bilioni 4.2, hazina msingi.
Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT- Wazalendo), Zitto Kabwe, ambaye
aliianzisha hoja hiyo, alisema tangu akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya
Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), amekuwa akilishauri shirika hilo
namna ya kuongeza gharama lakini hakuna walichokifanya.
“Kila Waziri anayeingia ninamshauri. Kwa mfano, sasa hivi kuna
ving’amuzi, tukisema kila mtu mwenye king’amuzi tumuwekee Sh. 500 kwa
ajili ya kuisaidia TBC na yenyewe ijiendeshe kama shirika la umma bila
matangazo, kwa mwaka watakuwa na zaidi ya Sh. bilioni 40.
“Sehemu kama Uingereza, kila mtu analipa fedha kwa ajili ya BBC
(Shirika la Utangazaji la Uingereza) ndiyo maana wao hawana matangazo,”
alisema Zitto.
Alisema hoja nyingine kama za watu kuacha kazi na kuhangaikia
televisheni, hazina msingi kwa sababu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Ibara ya 18 inatoa uhuru kwa wananchi kupata habari.
“Kwa hiyo ukiangalia mambo yote hapa utaona kuna kitu kimejificha
ndiyo maana mimi hata kwenye kamati ya uongozi nilisimamia msingi wa
katiba,” alisema Zitto.
Kutokana na hali hiyo, Zitto alisema ni dhairi kwamba matokeo ya
vipindi vya Bunge kurushwa moja kwa moja, viliigharimu CCM haswa kwenye
kashfa ya Escrow iliyosababisha wapoteze viti vingi kwenye serikali za
mitaa.
Katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Desemba 14, 2014 CCM ilikiri kuporomoka kwa asilimia 12 kwenye uchaguzi huo.
Mbunge wa Simanjiro, James ole Millya, alisema serikali inataka
kujigeuzi kuwa ya kidikteta baada ya kuona athari ilizopata kwenye Bunge
la 10 kwa wabunge kuiangusha serikali mara kadhaa.
“Kwenye matangazo ya moja kwa moja wananchi wanaona kila kitu. Huko
tunakokwenda watasitisha mambo mengi tu ili kinachojadiliwa bungeni
kisijulikane. Sote tunajua walichoambulia baada ya kashfa ya Escrow
kujadiliwa bungeni huku wananchi kwa ukaribu sana wakiwa wanafuatilia
mjadala ule,” alisema.
Alisema serikali kubana vyombo vya habari na kuwanyima wananchi
haki ya kupata habari, haitakuwa njia nzuri ndiyo maana wao wanahangaika
kuonyesha hawakubaliani na njia hiyo ya serikali kuficha udhaifu wao.
Kwa upande wa Mbunge wa Malindi, Ali Saleh Ali, alisema serikali
ilijua suala la Zanzibar litatikisa kwenye Bunge hili ndiyo maana
ikapanga mapema kulidhibiti Bunge.
“Serikali wanapata taarifa mapema ndiyo maana hata leo kuanzia
asubuhi umeona askari wamejaa hapa kwa sababu walijua tutatoka wakadhani
labda kutakuwa na fujo. Vivyo hivyo walijua kuwa tutasema ukweli wa
suala la Zanzibar hapa na hali yake ya kisiasa ndiyo maana wameamua
kukata matangazo ili wananchi wasione,” alisema.
Alisema kauli ya Nape ni utekelezaji wa matamanio yake ya tangu
mwaka 2013 na kwamba aliona serikali na chama chake kinabanwa kutokana
na Bunge kuonekana moja kwa moja.
“Februari 25, 2013, aliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook kuwa
ni vyema utaratibu wa kurusha mikutano ya Bunge moja kwa moja
ukasitishwa,” alisema Saleh.
Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya, alisema serikali inaendeleza mpango
wake wa kuhakikisha hakuna hata chombo kimoja kinachorusha moja kwa moja
matangazo hayo ndiyo maana imeanza na TBC.
“Eti wanasema watu hawafanyi kazi wanaangalia TV, kuna kazi gani
walizowapa? Hebu wawape kazi uone kama hawatafanya,” alisema Bulaya.
WABUNGE CCM WALONGA
Mbunge wa Jimbo la Donge, Sadifa Khamis Juma, aliiambia Nipashe
kwamba hoja iliyotolewa na serikali ililenga ilijikita kwenye msingi wa
gharama ambazo shirika limekumbwa nazo.
“Unajua siasa za bara ni tofauti na za Zanzibar. Kule ili uwe
maarufu inategemea ni jinsi gani unatoa huduma lakini bara wengi
wanakuwa maarufu kwa sababu ya vyombo vya habari.
“Yote hayo si mabaya, lakini kama gharama imekuwa kubwa ni bora au
zinatakiwa kupelekwa kwingine si vibaya kwa sababu wananchi kupata
huduma ni muhimu kuliko umaarufu kwa sababu hata mimi umaarufu wangu
umechangiwa na vyombo vya habari,” alisema Sadifa.
Naye Mbunge wa Shinyanga Mjini, Stephen Masele, alisema kwa sababu
hoja iliyowasilishwa na waziri ilijikita kwenye gharama, ni vyema
wapinzani wangekaa ndani ya chombo hicho cha kutunga sheria waangalie
namna ya kupata fedha za kugharamia matangazo hayo.
“Hili suala haliathiri wabunge wa upinzani tu, hata wa CCM pia. Kwa
hiyo ni vyema wangekaa hapa ili tuone namna ya kupata fedha ya
kugharimia TBC,” alisema.
NAPE ANENA
Usiku wa kuamkoa jana, Nape alifanya mkutano na waandishi wa habari
na kueleza kwamba wapinzani hawana sababu ya kuwa na wasiwasi kwa kuwa
lengo la serikali si baya na wala haiwahofii hata kidogo.
“Mimi tena nawaambia waikosoe serikali iwezavyo ili ifanye kazi na
si hao tu. Hata wa CCM wafanye hivyo. Hivi kweli kwa baraza lile
(Baraza la Mawaziri) kuna mtu wa kumhofia?,” alihoji.
Alisema Wabunge wa CCM ni zaidi ya asilimia 70 ndani ya chombo
hicho cha kutunga sheria, hivyo ni wazi kwamba hawana jambo lolote la
kuhofia.
Mbunge wa Bukoba Mjini (Chadema), Wilfred Lwakatare, alisema ni
jambo lisiloingia akilini kusema kipindi cha Bunge kitakachorushwa kwa
saa saba kinaweza kurushwa tena kwa saa moja na kutenda haki kwa watu
wote.
“Wataenda kuchuja na kupitisha kile ambacho kinawapendezesha wao.
kama wanasema watu hawafanyi kazi kwa sababu ya kuangalia televisheni
kuanzia saa sita, basi wafute vipindi vyote kuanzia muda huo mpaka
usiku,” alisema.
Alisema ni wazi kwamba wana wasiwasi ambao unachagizwa na nguvu ya wingi wa upinzani Bungeni.
KASHFA ZILIZOLITIKISA BUNGE
Kashfa kubwa iliyotikisa nchi katika kipindi cha awali cha Rais
Kikwete ilikuwa ni Richmond ya mwaka 2008. Hii ilitokana na tatizo kubwa
la uhaba wa umeme na serikali kulazimika kutafuta njia za dharura za
kutatua tatizo hilo, zikiwamo zilizodaiwa kukiuka taratibu na sheria.
Baada ya kashfa hiyo kuchunguzwa na taarifa kutolewa bungeni,
aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, alilazimika kujiuzulu baada ya
kutakiwa ajipime kutokana na mazingira ya kashfa hiyo.
Wengine waliong’oka madarakani kwa kujiuzulu ni mawaziri wa Nishati
na Madini kwa vipindi tofauti, Nazir Karamagi na Dk. Ibrahim Msabaha.
EPA
Mwaka 2008 iliibuka kashfa nyingine ya wizi wa mabilioni katika
Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania
(Bot) ambapo vigogo kadhaa walitumia mbinu chafu kuchota zaidi ya Sh.
bilioni 133 katika akaunti hiyo.
Katika wizi huo ulioitikisa nchi, wahusika walitajwa kutumia vivuli
vya siasa kupitisha nyaraka bila kufanyiwa uhakiki. Ilimalizika kwa
baadhi yao kufikishwa mahakamani na wengine ambao hawakutajwa kusamehewa
na Rais Kikwete wakidaiwa kurejesha fedha walizoiba.
Katika kipindi hicho, yalipofanyika mabadiliko ndani ya Baraza la
Mawaziri aliyekuwa Waziri wa Fedha, Zakia Meghji, hakurudi huku Gavana
wa BoT, Dk. Daudi Balalli akitimuliwa.
RIPOTI YA CAG 2012
Mwaka 2012, ilipotolewa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG) na kujadiliwa bungeni, ulitokea mtikisiko
mkubwa uliowang’oa mawaziri sita na manaibu wawili.
Waliong’olewa ni Dk. Cyril Chami (Viwanda na Biashara), Omary Nundu
(Uchukuzi), Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii), Dk. Hadji Mponda (Afya
na Ustawi wa Jamii), Mustafa Mkulo (Fedha) na William Ngeleja (Nishati
na Madini) na manaibu waziri wawili; Athumani Mfutakamba (Uchukuzi) na
Dk. Lucy Nkya (Afya na Ustawi wa Jamii).
OPERESHENI TOKOMEZA UJANGILI
Desemba 2013, Operesheni Tokomeza Ujangili (Otu), iliyoanzishwa na
serikali nayo ilizua mtikisiko mwingine uliowang’oa madarakani mawaziri
wanne ambao wizara zao zilielezwa kushindwa kusimamia vizuri utekelezaji
wake.
Mawaziri waliong’olewa ni Dk. Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani ya
Nchi), Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) na Waziri
wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Mathayo David Mathayo. Balozi
Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii), aliamua kujiuzulu kwa kile
alichokiita kupima uzito wa matokeo ya operesheni hiyo.
AKAUNTI YA TEGETA ESCROW
Novemba 2014, ripoti 0ya PAC bungeni baada ya kuchambua ile ya CAG,
iliyochunguza Akaunti ya Tegeta Escrow, ilisababisha mawaziri
kung’olewa.
Mawaziri hao ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Prof.
Sospeter Muhongo na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Prof. Anna Tibaijuka.
Watumishi wengine walioguswa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
Frederick Werema, Wenyeviti wa Kamati ya Nishati na Madini, Victor
Mwambalaswa, Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, William Ngeleja na
Kamati ya Bajeti, Andrew Chenge na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na
Madini, Eliakim Maswi.
CCM KUPOTEZA SERIKALI ZA MITAA
Katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika mwaka 2014, ingawa
CCM iliingia kwenye uchaguzi huo ikiwa na faida ya kupita bila kupingwa
katika vijiji 2,708, mitaa 644 na vitongoji 26,300, kupitia operesheni
za Movement For Change (M4C), Vua Gamba Vaa Gwanda, Delete CCM na
Mkachamchaka Kuelekea mwaka 2015 (V4C), upinzani ulinyakua viti vingi
kuliko wakati mwingine wowote.
Hali hiyo inadaiwa kuchangiwa kwa kiasi kikubwa na kashfa ya
Escrow ambayo ilikuwa imepamba moto kipindi hicho. CCM ilikiri kuwa
imeporomoka kwa asilimia 12 katika matokeo ya uchaguzi huo.
Chama hicho kilisema, kimeporomoka kutoka asilimia 96 mwaka 2009 hadi asilimia 84 mwaka 2014.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, aliwaambia
waandishi wa habari kwamba asilimia 16 ya viti walivyopata wapinzani
bado ni ndogo ikilinganishwa na miaka 22 tangu kurejea kwa mfumo wa
vyama vingi vya siasa nchini.
UPINZANI WAWATOLEA UVIVU POLISI
Baada ya juzi wabunge wa upinzani kutolewa nje ya ukumbi wa bunge
kwa kichapo kutoka kwa polisi, jana walitoka tena kimya kimya na
kuwatolea hasira zao askari waliokuwa nje ya jengo la kutokea ukumbini.
Tangu asubuhi jana, kabla ya kuanza kwa kikao cha Bunge, kulikuwa
na idadi kubwa ya askari wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU), ambao
walikuwa wamevalia mavazi maalumu ya kuzuia risasi.
Wabunge wa upinzani walipotoka nje ya ukumbi wa Bunge, baada ya
kipindi cha maswali na majibu kwisha, askari hao walisogelea eneo la
mlango wa kutoka kwenye ukumbi huo.
Kitendo hicho kiliwafanya baadhi ya wabunge hao kuanza kuwazomea polisi hao na kila mmoja kusema alilojisikia.
Baadhi ya maneno yaliyokuwa yakitamkwa dhidi ya polisi hao ni
pamoja na “leo cheni hamuibi” , ‘ingieni tena leo Bungeni mkachangie na
nyie” ‘leo hampati wa kumpiga”, “nendeni mkachangie ndani huko, kikao
cha familia kinaendelea”, “leo hamuibi tumewa-time”, “Ingieni ndani
kwenye kikao cha NEC kinaendelea huko” “Hebu waangalieni, watoto wa
maskini mnakubali kutumiwa”.
Wengine walikuwa wanasema, “leo mmekuja wapya ili muibe vizuri, hamuambulii kitu, mtaendelea kutumiwa hivyo hivyo".
Naye Zuberi Kuchauka wa Liwale (CUF), anayedaiwa kupigwa na askari
hao juzi na kuachwa na fulana, alikuwa akinyoosha juu kidole chake
kilichokuwa kimefungwa kitambaa akidai aliumizwa na askari hao.
“Nawaambieni hii damu mliyoimwaga mtailipa. leo hamumpigi mtu hapa nawaambia,” alisema.
Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bunge, Freeman Mbowe, alipozungumza
na waandishi wa habari jana, alisema kuna wabunge wa upinzani
wamelalamika kwamba wameibiwa vitu mbalimbali vikiwamo mikufu, simu na
pochi.
Kwenye maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu, Mbowe alitaka
serikali itoe tamko juu ya polisi kutumia nguvu kupita kiasi ikiwa ni
pamoja na lilivyotumia kuwatoa wabunge juzi na hali ilivyo Zanzibar kwa
sasa.
Baada ya swali hilo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema polisi
kazi yake ni kuhakikisha amani na utulivu vinakuwapo wakati wote na
kwamba watu wafanye kazi zao kama ilivyopangwa.
Alisema kuna mazingira yanayofanya polisi watumie nguvu na kwamba jambo la msingi ni kuwasaidia polisi kwa kutii sheria.
CHADEMA WATOA TAMKO
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimepinga hatua ya
serikali ya kufuta urushaji moja kwa moja matangazo ya bunge kupitia
TBC, na kwamba serikali ya awamu ya tano inaonyesha kuwa na hofu katika
kujibu na kutekeleza shughuli zake kwa vitendo.
Chadema, kupitia Kaimu Ktibu Mkuu wake, Salum Mwalimu, jana
iliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa hatua hiyo ni
dalili ya uendeshaji nchi kidikteta na kuondoa haki ya Watanzania
kufahamu kinachojadiliwa bungeni kupitia televisheni ya umma.
Aliomba kimelitaka Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Wamiliki wa
Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), kutokubali kuminywa kwa vyombo vya
habari katika kutekeleza majukumu yao.
Mwalimu alisema katiba ya nchi imevunjwa kwa kuwanyima haki
Watanzania kupata, kutafuta habari na kuzisambaza kwa kuwa sababu
zilizotolewa na serikali kwamba matangazo hayo ni gharama kubwa hazina
msingi na wala ukweli wowote.
Mwalimu alisema madai ya Waziri wa Waziri Nape kwamba urushaji
matangazo hayo ni ghali na yanafikia Sh. bilioni 4.2 kwa mwaka si ya
kweli, kutokana na ukokotozi wa gharama hizo kutowekwa hadharani.
“Haiwezekani kuondoa matangazo ya bunge ambayo hufuatiliwa na
Watanzania wengi, kwa walio vijijini hawawezi kuangalia marudio ya
matangazo ya bunge saa nne hadi saa tano usiku kwani wanakuwa wamelala
na gharama si kubwa kama ilivyoelezwa. Ziwekwe wazi Watanzania
tutalipia,” alisema Mwalimu.
Alisema kwamba mapato ya serikali yaliyoongezeka katika awamu ya
tano, yatumike katika kulipia matangazo hayo kwa kuwa suala hilo ni la
kitaifa.
Alisema tangu mkutano wa pili wa Bunge la 11 uanze mjini Dodoma,
uundwaji wa kamati za kudumu za bunge kwa ajili ya kuisimamia serikali,
uteuzi wa wenyeviti na wajumbe wa kamati hizo haukuzingatia uzoefu wa
watu.
Alisema uzoefu wa nchi zingine duniani ni kwamba matangazo ya bunge
au shughuli za kitaifa, huwa na chaneli maalumu ambayo muda wote
hurusha, tofauti na televisheni za watu binafsi ambazo haziwezi kumudu
gharama hizo.
WADAU WAZUNGUMZA
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika lisilo la kiserikali la Sikika,
Irenei Kiria, akizungumzia suala hilo la TBC kutorusha matangazo moja
kwa moja, alisema kilicho nyuma ya pazia ni mkakati wa kupunguza
uwajibikaji ndani ya Bunge hilo kwa visingizio tofauti.
Alisema vizuizi hivyo vilianza kuonekana tangu kwenye Kamati za
Bunge kwa kutoweka wabunge wenye uwezo wa kuibua mambo mbalimbali, jambo
ambalo linaonyesha wanakwepa kuwapo kwa uwajibikaji.
“Tunachoona kuna nguvu inaogopa mambo fulani ambayo hawataki
yaonekane au kusikika kwa wananchi kupitia luninga ya serikali ambayo
inaonekana sehemu kubwa nchini,” alisema.
Alisema kurusha kipindi cha Bunge si jukumu la serikali bali ni
Bunge lingepaswa kuhakikisha vipindi vyake vinaonekana kwa wananchi.
Kuhusu kuzuiwa kwa waandishi wa habari kufanya kazi zao, alisema ni
kuweka vizuizi ili kuhakikisha wananchi hawapati habari zinazotakiwa
jambo ambalo si sahihi.
Alisema wananchi wana haki ya kujua kinachojadiliwa na wawakilishi
wao na siyo kusubiri vipunguzwe na kwamba kuwaeleza kuwa walikuwa
wanaangalia TV muda mwingi halina mashiko kwa kuwa wanaweza kuangalia
vipindi vingine kwa muda huo.
Imeandaliwa na Fredy Azzah, Dodoma, Mwinyi Sadallah, Zanzibar, Christina Mwakangale na Salome Kitomari, Dar
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment