Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema tamko la
katazo la mikutano ya kisiasa nchini, lilitafsiriwa vibaya kwa kuwa
alizungumzia hali ya jimbo lake alipokwenda kuwashukuru wananchi, ingawa
alikataa kulifuta na kuvitaka vyama kufuata sheria.
Kauli ya Majaliwa ilitokana na swali aliloulizwa na Kiongozi wa
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, kwenye kipindi cha
maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu.
Katika swali lake, Mbowe alisema kauli hiyo ya Waziri Mkuu,
aliyoitoa akiwa jimboni kwake Ruangwa, inalenga kufifisha demokrasia na
kuzuia vyama vya siasa kutimiza majukumu yao.
Akijibu swali hilo, Majaliwa alisema uongozi wa serikali ya awamu
ya tano unafuata misingi ya kidemokrasia, sheria, kanuni na katiba.
“Suala la katazo kwa vyama vya siasa kufanya mikutano, msemaji wa
kwanza hakufanya kazi yake vizuri. Hii kauli niliitolea jimboni kwangu
nikiwa Mbunge na nilikuwa sijavaa koti la uwaziri mkuu.
“Nilikutana na makundi mengi, polisi, watumishi wa halmashauri na
madiwani wakiwamo wa vyama vya upinzani, ambaao walisema sasa tufanye
kazi na siasa pembeni na mimi nikasema ni kweli walioshinda ndio wafanye
kazi wakutane na wananchi,” alisema.
Aliongeza kuwa: “Kauli yangu ilitokana na mazingira yale, lakini
likichukuliwa na maeneo mengine si vibaya, kwa hiyo kama mwandishi
aliyeandika ile habari ya kwanza angeendelea kufuatilia niliyoyasema
kwenye ziara yangu yote ile jimboni, mkanganyiko huu usingekuwapo,”
alisema Majaliwa.
Baada ya jibu hilo, Mbowe alimtaka Majaliwa kubatilisha kauli yake
ya awali kwa maelezo kwamba yeye ni kiongozi kwa hiyo chochote
anachozungumza kinachukuliwa kama amri halali.
Hata hivyo, Majaliwa hakuikanusha kauli yake ya awali licha ya
kusema nchi inaongozwa na Katiba, kuna sheria zinazoiongoza hivyo kama
chama cha siasa kinataka kufanya mikutano, kifuate sheria.
Pia Mbowe alitaka Majaliwa afafanue kauli ya serikali juu ya
Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), kutorusha moja kwa moja
majadiliano bungeni.
Kuhusu swali hilo, Majaliwa alisema TBC ilichofanya ni kubadilisha
ratiba ambapo sasa itakuwa ikirusha kipindi cha maswali na majibu
asubuhi na kisha majadiliano kurekodiwa na kuonyeshwa usiku.
Kwa upande wake, Mbunge wa Babati Mjini (Chadema), Pauline Gekul,
alimwuliza Waziri Mkuu juu ya mkanganyiko wa elimu bure ambapo wanafunzi
wa bweni wanalipiwa fedha ya chakula shuleni lakini wale wa kutwa
waambiwa walipie chakula.
Majaliwa alikiri kuwapo kwa mkanganyiko kwenye suala la elimu bure
na kuwa hivi karibuni serikali itatoa mwongozo unaojitosheleza juu ya
utekelezaji wake.
Alisema baadhi ya mambo ambayo serikali itagharimia kwenye elimu
bure ni Sh. 20,000 ya ada kwa shule za sekondari za kutwa, Sh. 70,000 za
ada kwa shule za bweni, fedha za mitihani za darasa la nne na kidato
cha pili pamoja na gharama za chakula kwa shule za bweni.
Naye Mbunge wa Ilala (CCM), Mussa Zungu, alitaka serikali
itofautishe viwango vya kodi ya ongezeko la thamani (VAT), kufuatana na
ukubwa wa biashara, jambo ambalo litasaidia kuwafanya walio wengi kulipa
kodi hiyo na kuinua pato la taifa.
Alisema moja za nchi jirani, ambayo hakuitaja, ilipunguza VAT kwa
biashara zisizo rasmi mwaka 2009 na ikafanikiwa kukusanya Sh. trilioni
nane.
Akijibu swali hilo, Majaliwa alisema ombi kama hilo amewahi
kulipata tena alipokutana na wafanyabishara, lakini linahitaji utafiti
wa kina kwa sababu linaweza kuleta usumbufu wakati wa utekelezaji wake.
Alisema wasiwasi mkubwa uko kwenye tathmini ambapo ni rahisi
maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kuingia kwenye mitego ya
rushwa na kuwasumbua wananchi.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment