Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bunge, Freeman Mbowe.
Kivuli cha Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bunge,
Freeman Mbowe, kimedaiwa kuwa moja ya sababu zinazofanya serikali
ipunguze nguvu ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), kutokana na
kubaini kuwa alikuwa awe mwenyekiti wake.
Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bunge, Tundu Lissu, jana alisema ili
Mbowe aweze kuwa mwenyekiti wa PAC ni lazima awe mjumbe wake, jambo
ambalo limekuwa gumu baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, kukataa
kumpeleka huko.
Alisema Ndugai amefanya hivyo kwa madai kwamba amepokea amri kutoka
mamlaka za juu asihamishe mjumbe yeyote wa Kamati za Bunge ambazo
zimeshatangazwa.
“Mwanzo hatukufikiria kumpeleka Mbowe, lakini baada ya kuona kamati
zilizochakachuliwa, moja ya 'possibilities' ni hiyo (kumpelekea
kuongoza PAC) na ili aongoze lazima awe mjumbe (wa PAC) ila Ndugai
anasema ameambiwa asimpeleke huko,” alisema Lissu.
Alisema endapo hawataafikiana na Spika na kufanya marekebisho ya
wajumbe wa kamati kama wanavyotaka, kamwe hawatakuwa tayari kuongoza
kamati hizo.
“Hili bunge litakuwa la kichekesho. Unasema hizi ni kamati za
upinzani halafu unachagua nani ndiye aongoze, watuchagulie? Kwenye
utararatibu wa Jumuiya ya Madola tunaojifanya tunafuata PAC inaongozwa
na kiongozi wa upinzani.
"Ni kwa sababu huo ndio moyo wa serikali. Mapesa yote yako huko na
lazima iendeshwe na mtu imara. Wameumia (serikali) sana kwa miaka 15 PAC
na LAAC (Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa) zimewaumiza. Wanataka
kuiua nguvu ya hizi kamati ili yabaki majina tu,” alisema Lissu.
Alisema wakifanya kile alichosema ndiyo serikali inataka watapeleka watu dhaifu na mambo mengi mabovu yatapita.
“Watakuja kusema mwenyekiti ni wa kwao, sisi tunasema tunataka
mwenyekiti imara, Spika hawezi kutuchagulia viongozi dhaifu. Hizi
kamati hazipaswi kuongozwa na watu dhaifu na hili limefanyika pia
kwenye Kamati ya Katiba na Sheria, daktari wa binadamu amepelekwa huko
na Lissu anapelekwa kupigania sheria za ushuru wa pombe za gongo,
hatuwezi kukubali.
"Ukikubali umekwisha kabisa. Wasipokubali (kubadilisha wajumbe)
hatutakubali uongozi tutaacha. Mimi mwenyewe sheria ndogo siendi, huko
ni kupoteza muda. Nitaenda sheria na katiba na kushiriki mijadala, kura
tu ndiyo sitopiga. Hoja yoyote ya kisheria ikiibuka bungeni nitaibuka na
watashangaa,” alisema Lissu.
Mamlaka ya PAC kupelekwa PIC
Kuhusu Mamlaka ya PAC ya kusimamia mashirika ya umma na badala yake
kupelekwa Kamati ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC), haitatekelezeka
kwa sababu kanuni zinakataa.
“CAG anafanya uchunguzi wa hesabu za serikali kuu, serikali za
mitaa na mashirika ya umma, akimaliza uchunguzi baada ya kupeleka kwa
Rais analeta bungeni. Unapelekwa PAC na LAAC (Kamati ya Hesabu za
Serikali za Mitaa).
"CAG haripoti kwa Kamati ya Uwekezaji, anaripoti kwa PAC, Kamati ya
PIC inapokea taarifa ya msajili wa hazina na taarifa za mwaka za
mashirika ya umma, kama Tanesco (Shirika la Umeme Tanzania) na Tazara
(Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia) na nyingine,” alisema na
kuongeza:
“Taarifa ya CAG inakwenda PAC, huhitaji maneno ya (John) Joel
(Naibu Katibu wa Bunge, anayeshughulikia masuaya ya Bunge). Unahitaji
mambo ya kanuni na kuhoje je, CAG ataendelea kukagua taarifa za
mashirika ya umma? Kama ndiyo taarifa zake zitaenda wapi? Kama unasema
CAG hana tena mamlaka kukagua mashirika ya umma hapo sawa, akindelea
kukagua atazipeleka PAC kwa sababu huko ndiko anaenda kuripoti.
"Wana mawazo kwamba kwenye mashirika ya umma kuna uchafu sana na
huu uchafu umekuwa ukitumiwa na PAC kwa sababu ni ya upinzani na kwamba
upinzani wamekuwa wakiutumia kuwapiga (serikali)."
AWAFAGILIA Zitto, DK.SLAA.
Lissu alisema Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe,
na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, ni baadhi ya
wabunge wenye weledi mkubwa ambao wamewahi kuongoza PAC na LAAC na
kuiumiza serikali, jambo ambalo alisema sasa wanalikimbia.
“Tumekuwa na majadiliano na Spika na yeye amebanwa kweli kweli kwa
sababu anaambiwa na mamlaka za juu hapana. Sisi hatuko tayari kwa
kamati kama PAC na LAAC kuchaaguliwa mwenyekiti na CCM,” alisema.
Dk. Slaa na Zitto, alisema wanajua kuibua uchafu ndiyo maana
kamati hizo zilipata heshima kwa sababu ya kuendeshwa na watu wenye
weledi na watawala wanajua hilo. Alisema wamefanya hivyo ili
wasipatikane tena watu wenye weledi wa aina ya Dk. Slaa na Zitto.
Kwa nyakati tofauti, Zitto aliongoza kamati ya Hesabu za Serikali
Kuu na Mashirika ya Umma (POAC), kabla ya kubadilishwa na kuwa PAC
wakati Dk. Slaa aliongoza LAAC.
Juzi, Joel alisema ni kweli PIC wamepewa jukumu hilo hatua iliyochukuliwa kutokana na Kanuni za Bunge toleo la Januari 2016.
Alisema uamuzi wa kupeleka jukumu hilo PIC, umetokana na pendekezo
la Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), kutokana na PAC iliyopita
kushindwa kutimiza majukumu iliyopewa.
“Ni kweli, kabla hujaniuliza fanya utafiti ujue ni kitu gani
kilikuwa kinaendelea zamani. Ujue ni kwa nini PAC ilipewa hilo jukumu
halafu uniambie PAC walilitekeleza jukumu walilopewa? Kuna majukumu
walipewa na hawakutimiza,” alisema Joel.
Alipoulizwa majukumu ambayo hawakutimiza, Joel alisema “Hayo hayo
ya kukagua mashirika na ndiyo maana CAG akashauri ianzishwe kamati
nyingine.”
Alipofuatwa jana kutoa ufafanuzi wa hoja za Lissu, Joel alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa sababu hatotenda haki kwao.
Zitto afunguka
Ziitto, aliyekuwa Mwenyekiti wa PAC kwenye Bunge la 10, alisema si kweli kwamba kuna jukumu walilopewa na kushindwa kulitimiza.
“Tulitimiza majukumu yetu yote, na ili tufanye kazi yetu kwa
ufanisi, tuliigawa kamati, eneo moja likawa chini ya makamu mwenyekiti
(Deo Filikunjombe- sasa marehemu) na moja chini yangu. Deo mashirika na
mimi serikali.
“Hata hivyo kazi ilikuwa kubwa na muhimu kugawa PAC kuwa na PIC na
PAC. PIC ya sasa haina mamlaka ya kushughulikia hesabu za mashirika ya
umma kwa mujibu wa kanuni. Kamati za hesabu ni mbili tu, PAC na LAAC,’
alisema.
Aliongeza kuwa: “Iwapo Bunge linataka PIC ishughulike na hesabu za
mashirika ya umma itabidi iitwe (Public Investment Accounts Committee)
na itabidi iongozwe na mbunge wa upinzani na si kutoka CCM.
“Kanuni za Bunge za sasa hazielekezi PIC kushughulikia taarifa ya
CAG kuhusu hesabu za mashirika ya umma. Pia kanuni haziipi PAC mamlaka
hayo, kimsingi kikanuni hivi sasa hesabu za mashirika ya umma hazina
kamati.”
Kwa mujibu wa Kanuni za kudumu za Bunge, toleo la Januri 2016,
nyongeza ya nane sehemu ya nne, inasema kanuni za kudumu za Bunge
zinazosimamia matumizi ya fedha za umma zitakuwa PAC na LAAC.
Nipashe ilimtafuta Mbowe kuzungumzia suala hilo, alipokea simu yake
na kusema hayuko eneo zuri anatoka kanisani na akiwa vizuri
atazungumza.
KURUGENZI IKULU
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa, alipoulizwa
kuhusu taarifa zinazodaiwa kuwa zimetoka juu, alisema Kurugenzi yake
haina taarifa yoyote kama Rais John Magufuli alitoa amri ya kutorudiwa
upangaji wa wajumbe wa kamati za Bunge.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment