Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa.
Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
wamegawanyika kwa kiasi kikubwa kuhusiana na Sh. milioni 90 za mikopo ya
magari walizoanza kulipwa mwishoni mwa wiki.
Baadhi yao wameafiki kwa shingo upande huku wengine wakipinga kwa
maelezo kuwa fedha hizo haziendani na bei ya soko ya magari yanayoweza
kuhimili changamoto za miundombinu ya barabara kwenye majimbo yao.
Nipashe ilithibitishiwa kuwa kuanzia juzi, wabunge walianza
kuingiziwa fedha hizo kwenye akaunti zao huku baadhi wakikiri kukuta
kiasi hicho badala ya Sh. milioni 130 kilichokuwa kikitarajiwa na wengi
wao.
Kundi la kwanza lililojumuisha wabunge 160 ndilo lililoingiziwa
fedha hizo juzi akiwamo Mbunge wa Donge (CCM), Juma Sadifa, aliyekiri
kuingiziwa Sh. milioni 90 lakini akakuta Sh. milioni 89, kiasi kingine
kikikatwa kwa ajili ya gharama za bima. Wengine wanatarajiwa kupata
fedha hizo kati ya leo na kesho.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Nipashe jana, baadhi ya wabunge
walisema kiasi hicho hakitoshi kwa kuwa kimetokana na makadirio ya
mwaka 2010 wakati wa Bunge la 10 na kwamba hivi sasa fedha hizo hazina
nguvu ya kununulia magari madhubuti ya kuwasaidia katika kutekeleza
majukumu yao majimboni.
Aidha, wapo wabunge waliokiri kwamba kiasi hicho ni kidogo, lakini
wanaridhika nacho ili kuipa unafuu Serikali ya Rais Dk. John Magufuli
katika kutimiza dhamira yake ya kutatua kero mbalimbali za wananchi,
hasa zinazohusiana na huduma za kijamii kama maji na utoaji wa elimu
bure.
Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa, alisema
wanacholalamikia kuhusiana na mkopo huo ni kupewa fedha kwa kuzingatia
bei ya zamani ya gari madhubuti aina ya Toyota Land Cruiser, ambalo
wakati wa kuanza kwa Bunge la 10 mwaka 2010 lilikuwa likiuzwa kwa Sh.
milioni 90 lakini hivi sasa bei yake imepanda hadi kufikia Sh. milioni
150.
Aliongeza kuwa mazingira ya majimbo yao nchini yanatofautiana,
hivyo hata mahitaji ya magari kwa wabunge hutofautiana, akitolea mfano
wa jimbo lake kuwa ni dogo na lina miundombinu mizuri, tofauti na
wenzake wengi wa majimbo ya vijijini.
Alisema kuna majimbo yanahitaji magari imara kama ya aina ya Land
Cruiser Hardtop maarufu kama ‘mkonge’, ambalo jipya huuzwa kuanzia Sh.
milioni 150 hivyo wanapaswa kupewa fedha zitakazotosha kununua magari ya
aina hiyo ili kuwaondolea bughudha ya usafiri wabunge waishio kwenye
majimbo yenye miundombinu duni ya barabara.
“Kwa sababu hiyo, fedha hizi zinaweza kuwa kidogo au nyingi kwa
mbunge kulingana na ukubwa wa jimbo lake na miundombinu ya jimbo
husika,” alisema Msigwa.
Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally Keissy Mohamed, alisema fedha
hizo (Sh. milioni 90) hazitoshi kununulia gari litakalokidhi mahitaji
yake katika kuwatembelea wananchi wa jimbo lake.
Alisema jimbo lake lina ukubwa wa mita za mraba 8,000 na
miundombinu yake ni mibovu, hivyo anahitaji gari imara litakaloendana na
mazingira ya jimbo lake.
“Kuna majimbo unaweza kutumia bajaji kutembelea au hata kusafiri
kwa miguu lakini si jimbo la kwangu. Mbuga ya wanyama peke yake ina mita
za mraba 2,000. Fedha hizi hazitoshi,” alisema Keissy.
Hata hivyo, alisema hajapata fedha hizo, lakini atakapozitia mkononi ataongezea fedha zingine ili kununua gari imara.
Mbunge wa Korogwe Vijijini (CCM), Steven Ngonyani, alisema kutokana
na hali ya kiuchumi, wabunge wanapaswa kukubalina na mkopo huo wa Sh.
milioni 90 hata kama haukidhi mahitaji yao.
Alisema kwa kufanya hivyo, wabunge wataonyesha kuwajali wananchi
wao ambao hivi sasa wengi hupata shida mbalimbali ikiwamo ya uhaba wa
dawa hospitalini, hivyo mkopo huo wa gari kama ni mkubwa au mdogo,
wanapaswa kuupokea.
“Yaani Mbunge aongezewe fedha za gari wakati wanafunzi wanakaa
chini, au hakuna dawa hospitalini…hiyo haitakuwa sawa,” alisema
Ngonyani.
Kadhalika, alisema kwa Sh. milioni 90 mbunge anaweza kununua gari
zuri la kutembelea jimboni kwake, mfano kuna gari za muundo wa ‘pick up
hard board’ ambazo ni imara, nzuri na bei yake huanzia dola za Marekani
elfu 50 (Sh. milioni 107) hivyo kazi ya mbunge itakuwa kuongeza kiasi
kilichozidi.
Alisema ni kweli wabunge wanahitaji magari kwa ajili ya kufika
majimboni kwao ambao wengine miundombinu ni mibovu, lakini kwa sasa
wabunge wanapaswa kukubalina na hali iliyopo kwa kupokea kiasi cha fedha
walichopewa.
Mbunge wa Urambo (CCM), Margaret Sitta, alisema wabunge kwa sasa
wanapaswa kusubiri na kuwa watulivu kama walivyopewa taarifa na Spika wa
Bunge.
KATIBU WA BUNGE
Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, aliiambia Nipashe kuwa Bunge limetoa fedha kulingana na mahitaji ya miaka yote.
Alisema endapo fedha hizo hazitoshi au zinatosha kununulia gari
Bunge halihusiki, na kusema wabunge ndio wanaopaswa kuulizwa kama fedha
hizo zinafaa kununulia gari aina gani.
“Waulizeni wabunge wenyewe wanafahamu kiasi hicho kinafaa kununulia
gari aina gani. Bunge limetoa fedha kulingana na mahitaji ya miaka
yote,” alisema Dk. Kashililah.
UKWELI MIKOPO YA MAGARI KWA WABUNGE
Uchunguzi uliofanywa na Nipashe umebaini kuwa fedha hizo (Sh.
milioni 90), ijapokuwa baadhi ya wabunge wanalalamika kuwa ni kidogo na
hawajui ni magari ya aina gani wanunue kulingana na maeneo wanakotoka,
wengi wamekuwa hawaelekei kutegemea fedha hizo kwa ajili ya kununulia
magari pekee.
Mmoja wa wafuatiliaji wa karibu wa masuala yahusuyo Bunge (jina
limehifadhiwa) aliiambia Nipashe kuwa si wabunge wote hutumia fedha hizo
kununulia magari kwa kuwa wengine huendelea kutumia magari yao na
baadhi hulazimika kuzielekeza fedha hizo katika matumizi mengine, hasa
kuhusiana na utatuzi wa kero za wananchi wao.
Kadhalika, imeelezwa kuwa baadhi ya wabunge huwa hawana kawaida ya
kutumia magari yanayoonekana kuwa ya kifahari, hivyo ni wazi fedha hizo
si lazima kuzitumia zote kwa ajili ya kununulia magari.
Kwa mfano, mfuatiliaji huyo aliwataja baadhi ya wabunge aliodai
kuwahi kuwashuhudia mara kadhaa wakitumia magari yasiyolingana na fedha
za kiwango hicho kuwa ni Mbunge wa Kibamba (Chadema), John Mnyika, Grace
Kiwelu, Zainab Vullu na pia marehemu Dk. William Mgimwa aliyekuwa wa
Jimbo la Kalenga.
“Mnyika ameshawahi kuonekana mara kadhaa akiwa na gari aina ya
Toyota Vitz, Kiwelu ameshawahi kuonekana na Rav 4, Dk. Mgimwa alikuwa
akitumia Jeep lake na wakati mwingine Nissan Patrol. nakumbuka Profesa
(Peter) Msolla alikuwa akitumia pia Land Cruiser alilowahi kuwa nalo kwa
muda mrefu. Huu ni ushahidi kwamba si wabunge wote hutegemea fedha hizo
kwa kununulia magari tu,” alisema.
Kadhalika, mmoja wa wabunge wa muda mrefu aliiambia Nipashe kuwa
baadhi yao hutumia fedha hizo kwa mambo mengine mengi yanayowakabili
majimboni na siyo magari tu kama mkopo huo unavyoelezewa.
“Pale mbunge anapokwenda jimboni, wananchi huwafuata kwa makundi
wakiomba msaada wa shida na mambo mbalimbali. Wapo wanaosumbuliwa na
magonjwa, misiba, michango ya harusi, vipaimara, Maulid, ujenzi wa
nyumba za ibada na pia kuchangia mitaji ya vikundi vya wajasiriamali
wadogo,” alisema mbunge huyo.
Alieleza zaidi kuwa hata pale wabunge wanapokuwa Dodoma wakati wa
vikao vya Bunge, baadhi ya wapigakura wao hufika huko kuwalalamikia
matatizo mbalimbali huku wakiwa hawana fedha, hivyo gharama zote za
kuishi (Dodoma) na nauli ya kurejea jimboni walikotoka huwa ni juu ya
wabunge.
"Katika mazingira kama hayo, utaona kwamba wengi hawazitumii fedha
hizi kununulia magari tu… zina matumizi mengi,” mbunge huyo aliongeza.
WASTANI WA BEI ZA MAGARI 'USED'
Katika uchunguzi wake, Nipashe imebaini kuwa fedha hizo (Sh.
milioni 90), zinaweza kutumika katika kununulia magari kadhaa yenye hali
nzuri, lakini yaliyotumika.
Uchunguzi huo uliohusisha ziara katika 'show room' mbalimbali
jijini Dar es Salaam zinazojihusisha na uuzaji wa magari yaliyotumika
maarufu kama ‘used’, ulidhihirisha kuwa kwa mkopo wa Sh. milioni 90,
wabunge wanaweza kununua magari zaidi ya moja kulingana na mahitaji yao.
Magari hayo pia yanakuwa tayari yameshalipiwa tozo mbalimbali
zikiwamo za ushuru na leseni (road licence). Kazi kubwa kwa mteja wa
magari ya aina hiyo ni kugharimia bima na kuhamisha jina la umiliki.
Kupitia uchunguzi huo, Nipashe pia imebainika kuwa wastani wa bei
za magari aina ya Toyota Vitz toleo la zamani ni Sh. milioni nane na
toleo jipya Sh. milioni 10; Rav4 ya milango mitano (toleo la zamani)
huuzwa Sh. milioni 18 na toleo jipya Sh. milioni 22 wakati Mark X Sh.
milioni 18; Brevis Sh. milioni 15; Hilux Double Cabin Sh. milioni 35;
Passo Sh. milioni 8; Harrier (toleo la zamani) Sh. milioni 18 na toleo
jipya Sh. milioni 42.
Noah toleo la zamani ni Sh. milioni 14 na toleo jipya hupatikana
kwa Sh. milioni 12; IST toleo la zamani Sh. milioni 12 na toleo jipya
Sh. milioni 20; Crown Sh. milioni 22; Alphard Sh. milioni 22; Lapitz Sh.
milioni 12; Nissan Caravan (Elgrand) Sh. milioni 23; Carina TI Sh.
milioni 11 na Toyota Land Cruiser Hardtop (Mkonga) Sh. milioni 75.
Kwa bei hizo, kila mbunge anaweza kutumia Sh. milioni 90 kununua
Land Cruiser 'Mkonga' moja na kubakiwa na chenji ya Sh. milioni 15;
magari tisa ya toleo jipya la Vitz; Rav4 nne toleo jipya; magari manne
ya toleo jipya la IST; Harrier toleo jipya mbili; Brevis sita; Noah sita
(toleo la zamani); Crown nne; Carina TI nane; Alphard nne; Hilux Double
Cabin mbili na kubaki Sh. milioni 20; Lapitz saba na magari manne aina
ya Nissan Elgrand.
CHANZO:
GAZETI LA NIPASHE
0 comments:
Post a Comment