Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, Ummy Mwalimu, imelitaka Baraza la Wauguzi na Wakunga kuchukua
hatua dhini ya watoa huduma za afya ambao wanatoa lugha chafu kwa
wagonjwa ili kurudisha nidhamu ya sekta ya afya nchini.
Mwalimu alitoa agizo hilo wakati akijibu swali la nyongeza la
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Faida Mohamed Bakari, aliyetaka kujua
serikali inachukua hatua gani kwa wahudumu wa afya ambao wanatoa lugha
chafu za matusi kwa wagonjwa wanaopofika kutibiwa katika vituo vya afya
na hospitali.
Mwalimu alisema watoa huduma za afya ambao wamekuwa wakitoa lugha
chafu kwa wagonjwa watawajibishwa, huku akiwataka wananchi kutoa taarifa
wanapokutana na hali hiyo.
Waziri huyo alisema nidhamu imeshuka katika sekta ya afya nchini,
kutokana na baadhi ya watoaji wa huduma kuwa na lugha chafu na kuahidi
kurejesha sifa nzuri ya sekta hiyo kwa kuwawajibisha wasio na nidhamu.
Mwalimu alisema tangu alipoingia katika wizara hiyo aliweka
utaratibu wa watumishi wote wa sekta ya afya kuvaa vitambulisho vyenye
majina, ili kumuwezesha mgonjwa kujua mhudumu anayemhudumia.
Aliwataka wagonjwa kuhakikisha wanasoma majina ya waaguzi
wanaowahudumia ili watakapotoa lugha chafu ambazo haziendani na maadili
ya kazi yao waweze kutoa taarifa mara moja sehemu husika.
Alisema ameandaa utaratibu wa kupokea malalamiko mbalimbali na
kuyafanyia kazi kisha kuchukua hatua stahiki kwa wahusika ikiwa ni
pamoja kuwafikisha kwenye Baraza la Waaguzi na Wakunga kwa hatua za
kinidhamu dhidi ya wanaokiuka maadili ya utoaji wa huduma za afya.
CHANZO:
NIPASHE.
0 comments:
Post a Comment