MKUU wa Mkoa wa Dodoma Chiku Galawa amependekeza kuvunjwa kwa
halmashauri za Dodoma na Chamwino kutokana na maeneo hayo kuonekana kama
hayana viongozi.
“Natamani kuona halmashauri za Dodoma na Chamwino zinavunjwa ili
ziweze kuundwa upya kutokana na utendaji wa viongozi wake kwani
inaonekana kama hakuna viongozi,” alisema.
Alisema hayo juzi mjini hapa wakati wa kikao cha kwanza cha Bodi ya
barabara kwa mwaka 2015/2016 na kusema alichofanya ni kutoa mapendekezo
na mamlaka husika itaangalia juu ya suala hilo.
Alisema mambo mengi katika maeneo hayo yamekuwa yakienda ndivyo sivyo
licha ya kutoa maelekezo mbalimbali. Alisema kusuasua huko kwa utendaji
kunaweza kuchukua muda mrefu kuwatoa wananchi hapo walipo katika kupiga
hatua za kimaendeleo.
Alibainisha kuwa wameunda kikao kinachofanyika kila mwezi ili kutatua
matatizo na kero mbalimbali za wananchi. Aidha alisema kuanzia sasa ni
marufuku kuona mifugo inatembea katika maeneo ya mijini na hata vijijini
kuwe na sehemu moja ya kukatisha mifugo.
“Mifugo inazurura ovyo tu mijini hakuna wa kuzuia kumekuwa kama hakuna viongozi,” alisema.
Alisema katika baadhi ya maeneo wananchi wamelima mpaka karibu na
mifereji ya barabara hali ambayo kwa kiasi kikubwa inasababisha ng’ombe
kupita kwenye barabara za lami kwa umbali mrefu na kutaka hifadhi za
barabara zisitumiwe kwa ajili ya kilimo au uzoaji wa mchanga.
Aidha alisema nyumba zisizo na vyoo katika manispaa ya Dodoma ni
asilimia 40 tu ambapo pia katika baadhi ya maeneo visima vimechimbwa
karibu na vyoo hali ambayo inahatarisha afya za watumiaji wa maji
kukumbwa na magonjwa ya mlipuko na hata kuhara.
“Uchafu umezagaa kila mahali kama hakuna halmashauri kila mtu anavunja sheria,” alisema.
Akizungumza wiki iliyopita katika ziara yake wilayani Chamwino, Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Seleman
Jaffo alitaka watendaji katika wilaya ya Chamwino kujitafakari upya
kutokana na wilaya hiyo kuwa ya mwisho nchini kwa ukusanyaji wa mapato.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Sada Mwaruko wastani wa
makusanyo ya mapato kwa mwezi ni katika halmashauri hiyo ni Sh milioni
17.
Chanzo Habari leo
0 comments:
Post a Comment