MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Chiku Gallawa amepiga marufuku vyandarua
kufugia kuku, shughuli za bustani akisema watakaobainika kufanya hivyo
hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Alisema hayo jana mjini hapa wakati wa mkutano wake na waandishi wa
habari kuzungumzia masuala ya maendeleo na changamoto zilizopo, ikiwa ni
pamoja na masuala ya usalama wa chakula, changamoto za sekta ya elimu
na umasikini wa kipato.
Aidha watakaobainika wakiuza vyandarua vilivyotolewa na serikali kwa ajili ya kujikinga na malaria, watachukuliwa hatua.
Gallawa alisema katika maeneo mengi watu wamekuwa wakitumia vyandarua
hivyo katika bustani na kufugia kuku, jambo ambalo halikubaliki.
Ugawaji wa vyandarua ulianza Februari 7, mwaka huu, lengo likiwa ni
kuhakikisha kaya zote 453,844 mkoani Dodoma zinafikiwa na kupewa
vyandarua vyenye viuatilifu vya muda mrefu kwa asilimia 100.
Alisema jumla ya vyandarua 1,595,041 vilipangwa kugawiwa mkoani
Dodoma na mpaka sasa ugawaji umefikia asilimia 96 ya lengo, maeneo
machache yaliyosalia yalitakiwa kukamilisha ugawaji jana. Pia aliwataka
wananchi kupuuza uvumi kuwa vyandarua hivyo vina dawa ya sumu inayoweza
kuwaathiri.
Chanzo: Habari leo
Chanzo: Habari leo
0 comments:
Post a Comment