1.
Mheshimiwa Spika, awali ya yote, naomba kutumia fursa hii kumshukuru
Mwenyezi Mungu kwa kutulinda na kutufikisha salama siku ya leo
tunapohitimisha Mkutano wa Tano wa Bunge lako Tukufu tuliouanza tarehe 1
Novemba, 2016.
2.
Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia kukupa pole, kwa msiba mzito
uliotokea tarehe 7 Novemba, 2016 ambao Bunge lako tukufu, Serikali na
Taifa tumepata kwa kumpoteza Mheshimiwa Samwel Sitta, mmoja wa Viongozi
mahiri wa Bunge hili katika historia ya nchi yetu.
Msiba
uliotupata wa aliyekuwa Spika Mstaafu wa Bunge la Tisa (2005-2010) na
Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Urambo Mkoani Tabora ni pigo kwa Taifa letu.
Nasi Wabunge kwa kuwawakilisha Watanzania leo hii muda mfupi ujao
tutaaga mwili wa kipenzi chetu Mheshimiwa Samuel Sitta. Tunamwomba
Mwenyezi Mungu ailaze Roho ya Marehemu mahali pema Peponi. Amina.
3.
Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kutoa pole kwa mjane wa
marehemu, Mheshimiwa Margareth Simwanza Sitta, Mbunge mwenzetu, watoto
wake na wanafamilia wote na marafiki wote kwa ujumla kutokana na msiba
mzito uliowapata. Tunamuomba Mwenyezi Mungu awape subira katika kipindi
hiki kigumu cha majonzi na siku zote wamtangulize Mwenyezi Mungu katika
kuwaongoza wanafamilia waliobakia.
Sina
budi kukiri kuwa Taifa limempoteza mtu muhimu aliyetoa mchango mkubwa
katika uongozi na maendeleo. Enzi za uhai wake, Marehemu Mheshimiwa
Sitta, alibahatika kufanya kazi na Marais wa awamu zote nne zilizopita
tangu ya kwanza ya Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, akiwa
Mbunge kwa miaka 30. Alikuwa ni Spika wa Bunge la Tisa la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Nyadhifa nyingine alizowahi kushika ni pamoja na
Mkuu wa Mikoa ya Iringa na Kilimanjaro, Waziri wa Ujenzi, Waziri
aliyesimamia Ustawishaji Makao Makuu, Waziri wa Katiba na Sheria, Waziri
wa Afrika Mashariki, Waziri wa Uchukuzi na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu
la Katiba.
4.
Mheshimiwa Spika, tarehe 8 Novemba, 2016 tumeondokewa tena na Kiongozi
wa muda mrefu Serikalini Ndugu Joseph Mungai. Kiongozi huyu ameshika
nafasi mbalimbali katika utumishi wa umma ikiwemo Ubunge na Uwaziri.
5.
Mheshimiwa Spika, tangu tulipokutana mara ya mwisho, pametokea majanga
mbalimbali yakiwemo maradhi, ajali, na matukio mengine ambayo
yamesababisha vifo na majeruhi kwa Watanzania wenzetu. Sote tunakumbuka
tukio la kusikitisha la watumishi wa Serikali waliopoteza maisha wakiwa
kazini walipovamiwa na wanakijiji wa Makang’wa wilayani Chamwino mkoani
Dodoma. Nalaani mauaji hayo na kuvitaka vyombo vya usalama kuwachukulia
hatua wote waliohusika. Vilevile, katika miezi ya Oktoba na Novemba,
kumetokea ajali za barabarani katika Mikoa ya Mbeya, Pwani, Singida,
Lindi, Iringa, na ile iliyopoteza ndugu zetu 19 mkoani Shinyanga na
kwingineko ambako ndugu zetu walipoteza maisha. Ninatoa pole kwa wafiwa
wote na wale wote waliopatwa na majanga kutokana na matukio hayo.
Tunawaombea
afya njema wale waliopata majeraha na waliopo hospitali. Pia niendelee
kuwataka Askari wa usalama barabarani kuhakikisha wanasimamia madereva
na watumiaji wa Barabara kuzingatia Sheria za usalama wa barabarani.
6.
Mheshimiwa Spika, leo tunahitimisha Mkutano huu wa Tano tukiwa
tumekamilisha shughuli zote zilizopangwa. Naomba nitumie fursa hii
kukupongeza wewe Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa
Wenyeviti wa Bunge na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kukamilisha kazi zote
kwa ufanisi mkubwa. Nawapongeza sana!
SHUGHULI ZA BUNGE
7.
Mheshimiwa Spika, katika mkutano huu tumepata fursa ya kujadili,
kupokea na kushauri kuhusu mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa
unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na muongozo wa kuandaa
Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2017/2018. Aidha, katika
kipindi hiki, tumejadili Hoja mbalimbali za Serikali ikiwemo Miswada,
Taarifa za Kamati, Mkataba wa EPA, Maazimio na Kauli mbalimbali za
Mawaziri. Vilevile, Wabunge walipata majibu ya maswali mbalimbali ya
msingi na ya nyongeza yaliyoulizwa na Waheshimiwa Wabunge na maswali ya
Papo kwa Papo kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
8.
Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kumshukuru Mwanasheria Mkuu
wa Serikali, pamoja na Wataalam wake, kwa kazi kubwa ya kuandaa miswada
mbalimbali iliyowasilishwa katika Bunge lako Tukufu. Aidha, napenda
kutumia fursa hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao
mizuri. Serikali itazingatia ushauri na maoni yenu wakati wa
utekelezaji.
MAAZIMIO
9.
Mheshimiwa Spika, katika mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge wamepata
fursa ya kupokea na kujadili Mkataba wa Ubia wa Uchumi baina ya Jumuiya
ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya yaani East Africa Community –
European Union Economic Partnership Agreement. Napenda kuwashukuru
Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yenu mizuri tuliyoipata wakati wa
mjadala wa Mkataba huo. Serikali itafanyia kazi maoni, ushauri na uamuzi
wenu kuhusu Mkataba huo.
JUHUDI ZA SERIKALI ZA KUWAHUDUMIA WAATHIRIKA WA TETEMEKO LA ARDHI MKOANI KAGERA
10.
Mheshimiwa Spika, mtakumbuka kuwa mnamo tarehe 10 Septemba, 2016
lilitokea tetemeko la ardhi katika eneo la Kanda ya Ziwa na hususan Mkoa
wa Kagera. Tetemeko hilo lilisababisha athari mbalimbali zikiwemo vifo,
majeruhi, uharibifu wa makazi na miundombinu ya umma na watu binafsi.
Jumla ya Watu 117,721 wameathirika kwa kupoteza makazi yao, mali na
athari za kisaikolojia katika Wilaya za Bukoba, Missenyi, Muleba,
Karagwe na Kyerwa. Aidha, jumla ya watu 17 walipoteza maisha na 560
walijeruhiwa. Vilevile, nyumba 2,072 za makazi zilianguka kabisa na
nyumba 14,595 za makazi zilibomoka, baadhi zina kuta au kupata nyufa
kubwa na hivyo kuzifanya kuwa hatarishi kwa makazi ya binadamu.
Vilevile,
maafa haya yalisababisha uharibifu wa miundombinu ya barabara na
majengo ya Serikali 1,718 yaliyoharibika kwa viwango tofauti.
11.
Mheshimiwa Spika, kufuatia hali hiyo, Serikali ilianzisha Kituo cha
Operesheni na Kuratibu Maafa kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera kwa
lengo la kuharakisha huduma. Aidha, Serikali ilitoa matibabu bure kwa
majeruhi wote, kuandaa na kugharamia mazishi ya watu 17 waliofariki
ambapo mimi binafsi nilihudhuria na pia kutoa mkono wa pole wa Shilingi
Milioni 17 kwa wafiwa. Vilevile, Serikali kwa kushirikiana na Wadau
mbalimbali iliwahudumia wananchi walioathirika na tetemeko kwa kuwapatia
misaada ya kibinadamu ikiwemo chakula, madawa, nguo, makazi ya muda,
vifaa vya ujenzi, vifaa tiba, vifaa vya shule na huduma ya ushauri wa
kisaikolojia. Aidha, Serikali kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwakilishi
Mkazi wa Umoja wa Mataifa na wadau mbalimbali walifanya Tathmini ya
pamoja ya mahitaji ya haraka katika kukabiliana na Athari za Tetemeko
hilo. Ambapo utekelezaji wa masuala muhimu yaliyoainishwa katika
tathmini hiyo unaendelea.
12.
Mheshimiwa Spika, ili kuwezesha wadau, taasisi na wananchi mbalimbali
kuchangia maafa hayo, Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Kamati ya
Maafa ya Mkoa wa Kagera ilifungua Akaunti pekee Namba 0152225617300
katika Benki ya CRDB Bukoba yenye jina la “KAMATI MAAFA KAGERA”. Hadi
kufikia tarehe 10 Novemba, 2016 kiasi cha Shilingi 5,427,671,677.32
kilikuwa kimeingizwa kwenye Akaunti hiyo. Hadi kufikia tarehe 10 Novemba
2016 Salio katika Benki ni Shilingi 4,296,038,711.79 na matumizi hadi
tarehe tajwa yalikuwa ni Shilingi 1,130,428,347.53. Aidha, Kamati pia
ilisajili namba za simu za mkononi za kupokea michango katika Kampuni za
Vodacom (M-Pesa) 0768 196 669, Tigo (Tigopesa) 0718 069 616 na Airtel
(Airtel Money) 0682 950 009 kwa jina la “KAMATI MAAFA KAGERA”. Hadi
kufikia tarehe 10 Novemba, 2016, kiasi cha Shilingi 16,638,747
kilichangwa kupitia mitandao hiyo ya simu. Hivyo kufanya jumla ya fedha
zilizopokelewa kupitia Benki na Mitandao ya Simu kuwa Shilingi
5,444,310,424.32. Aidha, Serikali imechangia Shilingi Billioni Moja
katika kukabili janga hilo.
13.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kupokea misaada kutoka kwa
Washirika wetu wa Maendeleo, Balozi na hata Nchi marafiki. Mathalan,
tumepokea kutoka Serikali ya Uganda Dola za Kimarekani 200,000 sawa na
Shilingi Milioni 419.2, Serikali ya India Shilingi Milioni 547, Serikali
ya Kuwait Shilingi Milioni 51 na Serikali ya Uingereza iliahidi kutoa
Shilingi Bilioni Sita zitakazoelekezwa kwenye ujenzi wa shule.
14.
Mheshimiwa Spika, tumepokea vifaa mbalimbali vyenye thamani ya zaidi ya
shilingi milioni 357 yakiwemo maturubai, magodoro, ndoo, mashuka, vifaa
tiba, dawa na chakula kutoka Serikali za Japan, China, Kenya, Pakistan,
Burundi na Rwanda.
15.
Mheshimiwa Spika, taarifa ya Kikosi Kazi cha Wataalam imeainisha kuwa
takribani Shilingi Bilioni 63.2 zitahitajika kurejesha hali ya kawaida
katika Mkoa wa Kagera kufuatia maafa hayo. Gharama hii inajumuisha
ukarabati wa shule za msingi, sekondari, vituo vya afya na taasisi
nyingine katika wilaya zote sita za Mkoa huo, ujenzi mpya wa shule za
Ihungo na Nyakato (tayari wafadhili wamejitolea kujenga shule hizi).
Aidha, hadi kufikia tarehe 10 Novemba, 2016 kiasi cha Shilingi
966,898,826 zilitumika katika kufanya ukarabati mkubwa na mdogo wa Shule
za Msingi na Sekondari pamoja na Zahanati katika Halmashauri za Mkoa wa
Kagera. Serikali inaendelea na ujenzi wa Zahanati mpya (Ishozi)
inayojumuisha chumba cha Upasuaji na wodi ya kinamama na watoto na
usimamizi wa ujenzi wa shule za Ihungo na Nyakato. Aidha, katika
kuongeza nguvu ya urejeshaji hali jumla ya Askari 96 wa Jeshi la
Wananchi wa Tanzania wakiwemo Wahandisi, Mafundi, Wapishi, na Madereva
waliwasili Mkoani Kagera tarehe 19 Oktoba, 2016 kushiriki katika zoezi
la kurejesha hali ya majengo na miundombinu.
16.
Mheshimiwa Spika, Serikali inapenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu na
wananchi kwa jumla kuwa Serikali ipo pamoja na waathirika hawa katika
suala hili na ina mikakati madhubuti ya kuhakikisha tunarejesha hali
bora kwa kuendelea kurudisha miundombinu, kutoa huduma za kibinadamu na
matibabu kwa waathirika. Aidha, napenda kuwashukuru wale wote
waliochangia katika kusaidia wenzetu wa Kagera, kwani katika kipindi
hiki, tumeonesha umoja wetu, upendo wa dhati, hali ya kuthaminiana na
kujaliana. Mungu awabariki sana na kuwaongezea pale walipotoa. Kipekee,
niwashukuru Nchi marafiki, Balozi, Wadau wa Maendeleo wa ndani na nje ya
Nchi, Taasisi za Kiserikali na zisizo za Kiserikali, Taasisi za Fedha,
Kampuni, Vikundi mbalimbali, pamoja na Wananchi wote wakiwemo wale
waishio nje ya Nchi.
MAPENDEKEZO YA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA WA MWAKA 2017/2018
17.
Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu wa tano wa Bunge, Serikali
imewasilisha mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka
2017/2018. Napenda kutumia fursa hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa
michango yao mizuri iliyotolewa wakati wa kujadili Hoja hiyo. Maoni na
ushauri uliotolewa utazingatiwa wakati wa maandalizi ya Mpango na Bajeti
ya mwaka wa fedha wa 2017/2018.
TAARIFA ZA KAMATI ZA KUDUMU ZA BUNGE ZA PAC NA LAAC KUHUSU HESABU ZILIZOKAGULIWA KWA MWAKA 2013/2014 NA 2014/2015
18.
Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge wamepata
fursa ya kujadili Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali na Taarifa za Kamati za Kudumu za Bunge za PAC na LAAC kuhusu
Hesabu za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Serikali za Mitaa
zilizokaguliwa kwa mwaka ulioishia tarehe 30 Juni, 2014 na tarehe 30
Juni, 2015. Serikali imepokea michango na Hoja za Waheshimiwa Wabunge na
itazifanyia kazi.
19.
Mheshimiwa Spika, napenda kuwakumbusha Waheshimiwa Wabunge kwamba kwa
mujibu wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 hadi 2016, Serikali
imetakiwa kuchukua hatua kali na za haraka kwa wale wote watakaobainika
kujihusisha na ubadhirifu na
wizi wa mali ya umma, ukiukaji wa maadili ya Utumishi wa Umma na wale
wanaoendeleza vitendo vya rushwa na matumizi mabaya ya fedha za Umma.
Kutokana na maelekezo hayo, Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea
kuimarisha udhibiti wa matumizi ya Serikali na kuchukua hatua kwa
Watumishi wa Umma wasiozingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za matumizi
ya Fedha za Umma. Maafisa Masuuli wote wanakumbushwa kuzingatia
kikamilifu Sheria ya Ununuzi wa Umma na Kanuni zake. Aidha, Maafisa
Masuuli wote wanatakiwa kuchukua hatua stahiki za kinidhamu na kisheria
kwa Wakuu wa Idara, Vitengo na Taasisi za Serikali wanaofanya malipo
yenye mashaka wakati wa kufanya manunuzi ya Umma au kuingia Mikataba na
Zabuni tata za utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Hatua hizo
zitapunguza na kuondoa Hoja za ukaguzi na kuimarisha usimamizi wa fedha
za walipa kodi.
SEKTA YA KILIMO
Mwenendo wa Uzalishaji wa Mazao Katika Msimu wa Mvua za Vuli
20.
Mheshimiwa Spika, naomba nitoe taarifa kutoka Mamlaka ya Utabiri wa
Hali ya Hewa kuwa, kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2016 imeonesha
kuwa katika maeneo mengi ya nchi, mvua zinatarajiwa kuwa chache,
kuchelewa kuanza na mahali pengine kunyesha kwa mtawanyiko usioridhisha.
Aidha, kwa maeneo yanayopata mvua za vuli zikiwemo Wilaya za Kyerwa,
Missenyi na Karagwe, mvua zilipoanza kunyesha zilikuwa chini ya wastani
na kusababisha baadhi ya mazao yaliyopandwa kuathirika. Vile vile,
taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa TMA zinaeleza kuwa katika maeneo
yanayopata msimu mmoja wa mvua zinazoanza mwezi Novemba hadi Aprili,
mvua zitachelewa na kunyesha chini ya wastani hadi wastani katika maeneo
mengi isipokuwa katika baadhi ya maeneo ya Mtwara Lindi na Ruvuma.
Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kuwataka wataalam wa kilimo
kuhakikisha wananchi katika maeneo yatakayopata mvua kidogo wanawezeshwa
kupata mbegu za mazao yanayostahimili ukame na zinazokomaa haraka.
Aidha,
niwashauri wakulima kuandaa mashamba yao mapema na kutumia mbegu hizo
zinazokomaa mapema na kustahimili ukame. Niwasihi wananchi na wakulima
kuendelea kutumia kwa uangalifu na kuhifadhi akiba ya chakula
walichovuna au kununua kwa matumizi katika kaya zao. Nitoe wito kwa
Sekta binafsi kuendelea kushiriki katika kutoa masoko ya kununua na
kuuza mazao katika maeneo yenye ziada na kuyauza katika maeneo yenye
uhaba.
Usambazaji wa Pembejeo za Zao laTumbaku
21.
Mheshimiwa Spika, ili kuondoa kero ya upatikanaji wa pembejeo kwa zao
la tumbaku kwa msimu wa 2016/2017, Serikali imebadili utaratibu kutoka
ule uliohusisha zabuni kwa wauzaji wa kati (middlemen) na kuweka
utaratibu mpya unaohusisha wazalishaji wa pembejeo kuzisafirisha
pembejeo hizo hadi katika Vyama vya Msingi vya Ushirika moja kwa moja
kwa bei ya Dola za Kimarekani 40.45 kwa mfuko wa NPK (ikilinganishwa na
Dola za Kimarekani 52.7 za msimu uliopita), na Dola za Kimarekani 21
pungufu kwa mbolea aina ya Urea na CAN kwa tani moja ukilinganisha
uliopita. Hadi sasa wazalishaji wawili wa mbolea za tumbaku (Kampuni ya
Yara Tanzania na Rosier) wamechukua jukumu hilo. Napenda kuchukua fursa
hii kuvitaka Vyama vya Ushirika kusimamia kikamilifu mpango huu ili
wakulima wazalishe kitaalamu na kuongeza tija katika uzalishaji.
SEKTA YA VIWANDA NA UWEKEZAJI
22.
Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 17 Oktoba, 2016, Mheshimiwa Waziri wa
Viwanda, Biashara na Uwekezaji alizindua rasmi matokeo ya Sensa ya
Uzalishaji Viwandani ya mwaka 2013 iliyofanyika kwa ushirikiano wa
Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji na Ofisi ya Taifa ya Takwimu
(NBS). Zoezi la sensa hii lilitumia taarifa za uzalishaji za viwanda za
mwaka, 2013, yaani viwanda vilivyokuwepo mwaka 2013 na vilivyokuwa
vinazalisha. Zoezi la ukusanyaji wa taarifa za uzalishaji, za viwanda
lilifanyika mwaka 2014 na mwaka 2015 ilikuwa ni kufanya uchambuzi wa
kitalaamu na kuandika ripoti.
23.
Mheshimiwa Spika, matokeo ya Sensa hiyo yanaonesha kuwa, kufikia mwaka
2013 Tanzania ilikuwa na jumla ya viwanda 49,243 ambapo viwanda vidogo
vinavyoajiri mtu 1 – 4 vilikuwa ni Asilimia 85.13, viwanda vidogo vyenye
watu 5 – 49 ni Asilimia 14.02, viwanda vya kati vyenye watu 50 – 99 ni
Asilimia 0.35 na viwanda vikubwa vyenye watu kuanzia 100 na kuendelea ni
Asilimia 0.5. Hivyo, Asilimia 99.15 ya viwanda vyote nchini ni viwanda
vidogo.
24.
Mheshimiwa Spika, katika utafiti wa mwaka jana ilionekana kuwa mpaka
mwezi Oktoba, 2015 kulikuwa na viwanda 52,579. Aidha, kwa kipindi cha
mwaka mmoja tu, yaani kuanzia Novemba, 2015 mpaka Oktoba, 2016 jumla ya
viwanda vipya 1,843 vimeanzishwa na kufanya jumla ya viwanda vyote
nchini kufikia 54,422. Ni matumaini ya Serikali kuwa kutokana na juhudi
za uhamasishaji zinazofanyika, kasi ya uanzishwaji viwanda na hasa
viwanda vidogo na vya kati na vikubwa itaongezeka sana.
25.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara mbalimbali za Kisekta tayari
imebainisha maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya kuchochea uwekezaji
kama vile kuendeleza eneo la Mji wa Kigamboni na kutenga maeneo maalum
ya Uwekezaji katika Mikoa mbalimbali Nchini. Hatua nyingine ni kuboresha
miundombinu kama vile barabara na reli. Mfano mzuri ni ujenzi wa reli
yenye urefu wa kilomita 4 katika kiwanda kipya cha KILUA GROUP cha
kutengeneza nondo kilichopo Mlandizi, Pwani. Pia, Serikali inaendelea
kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika. Kwa viwanda ambavyo vipo
karibu na bomba la gesi watasaidiwa kuunganishwa na gesi. Vilevile,
Serikali, imechukua hatua madhubuti za kuharakisha upatikanaji wa ardhi
ambacho ni kivutio muhimu katika kuhamasisha uwekezaji.
Uongezaji Kasi ya Uwekezaji kwenye Sekta ya Viwanda Nchini
26.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha
kasi ya uwekezaji kwenye sekta ya viwanda inaongezeka ili ichangie
Asilimia 15 ya Pato la Taifa ifikapo mwaka 2020 Ili kutekeleza adhima
hiyo hatua zifuatazo zinaendelea kuchukuliwa:-
Kwanza:
Kutambua sekta za kipaumbele kwa kuzingatia viwanda vinavyotumia
malighafi za ndani, na hususan kwenye sekta za kilimo na maliasili ili
kuchochea uzalishaji vijiini na kuongeza ajira; viwanda vinavyotumia
malighafi za ndani ambazo si za kilimo kama vile madini na kemikali; na
kuweka msukumo kwenye kuanzisha viwanda visivyotumia malighafi za ndani
kama vile uunganishaji wa magari na uzalishaji wa vifungashio.
Pili:
Kuandaa Mpango mahsusi wa uwekezaji kwenye viwanda kupitia Mifuko ya
Hifadhi ya Jamii. Mpaka sasa, Mifuko ya LAPF, PPF, PSPF, NSSF na GEPF
tayari wameainisha miradi ya uzalishaji watakayoanza nayo.
Tatu:
Kuhamasisha Sekta Binafsi, ya ndani na nje ya Nchi, kuwekeza kwenye
viwanda. Kupitia makongamano ya biashara na uwekezaji nchi mbali mbali
zimehamasishwa kuwekeza nchini. Baadhi ya nchi hizo ni China, Oman,
Vietnman, Urusi, Morocco n.k.
Nne: Kuingia makubaliano ya ushirikiano na Nchi zingine ili kuongeza uwekezaji.
Mpaka
sasa Nchi ya China imechagua jimbo la Jiangsu kuleta viwanda nchini na
pia kupitia Jukwaa la Ushirkiano la China na Afrika itawezesha ujenzi wa
miundombinu ikiwemo Bandari ya Bagamoyo. Aidha, kwa utaratibu huu
Serikali tayari imeanza utekelezaji wa mradi wa kuunganisha matrekta
2400 pale TAMCO Kibaha kufuatia ushirikiano na Serikali ya Poland,
uunganishaji wa magari wa Kampuni ya Kitanzania ya SIMBA MOTOR kwa
ushirikiano na Jeshi (NYUMBU) na Kampuni ya China. Vile vile, India
kupitia mradi wake wa kuimarisha uwekezaji Afrika (SITA) inasaidia
utekelezaji wa mikakati minne ya kukuza na kuendeleza alizeti, pamba,
ngozi na mazao ya jamii ya kunde.
Tano:
Kutoa elimu na mwongozo kwa Serikali ngazi ya Mikoa na Wilaya kuendelea
kuhamasisha uwekezaji katika maeneo yao. Serikali imegawa Mikoa katika
makundi manane ambayo Watendaji Waandamizi wa Wizara ya Viwanda,
Biashara na Uwekezaji watakwenda kuzungumza na wadau ili kuhakikisha
viwanda vinasambaa Nchi nzima.
27.
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza jukumu hili mambo muhimu ambayo
Mikoa inatakiwa kuzingatia ni pamoja na Mikoa kuweza kubaini fursa
walizonazo na kuandaa taswira ya mkoa kutegemeana na fursa walizonazo.
Aidha, Mikoa inahimizwa kuhamasisha wananchi juu ya uwekezaji. Vilevile,
Viongozi wa Mkoa wanashauriwa kuongeza kasi ya kuhamasisha Mamlaka za
Serikali za Mitaa kutenga maeneo na kuhakikisha kuwa wanazingatia katika
mipango ya Halmashauri za wilaya ujenzi wa miundombinu wezeshi kwenye
maeneo watakayotenga kwa ajili ya uwekezaji.
SEKTA YA ELIMU
Matokeo ya Mitihani ya Darasa la Saba 2016
28.
Mheshimiwa Spika, mwezi Oktoba, 2016 Baraza la Mitihani la Taifa
lilitangaza matokeo ya Mitihani wa Darasa la Saba kwa mwaka 2016.
Taarifa hiyo ilibainisha kuwa katika mtihani huo, kati ya wanafunzi
789,479 waliofanya mtihani, jumla ya wanafunzi 555,291 walifaulu sawa na
Asilimia 70.36. Kati yao wasichana ni 283,751 na wavulana ni 271,540.
Nitumie fursa hii kuwapongeza wanafunzi wote waliofaulu na Shule zote
zilizofanya vizuri na hasa wale kumi bora. Napenda kuwaagiza Viongozi wa
Mikoa na Halmashauri kuendelea kukamilisha miundombinu ya vyumba vya
madarasa na miundo-mbinu mingine ili kuandaa mazingira ya kuwapokea
wanafunzi wanaotakiwa kujiunga na kidato cha kwanza mwezi Januari, 2017.
Kila Mkoa uweke lengo la kuhakikisha Wanafunzi wote watakaochaguliwa
wanajiunga na Sekondari. Serikali kwa upande wake itahakikisha inatoa
ruzuku kwa ajili ya mahitaji ya Wanafunzi watakaojiunga na Sekondari.
Mwenendo wa utoaji wa mikopo
29.
Mheshimiwa Spika, tangu mwaka 1994 Serikali ilipoanza kutoa mikopo kwa
wanafunzi wa Elimu ya Juu, jumla ya kiasi cha Shilingi Trilioni 2.44
kimekwishatolewa. Jumla ya wanafunzi 324,994 wamenufaika na fedha hizo.
30.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017 jumla ya wanafunzi 64,441
wamedahiliwa na Tume ya Vyuo Vikuu na orodha yao kuwasilishwa Bodi ya
Mikopo ya Elimu Juu. Kama alivyoeleza Mheshimiwa Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia tarehe 3 Novemba, 2016, wakati akitoa kauli ya
Serikali Bungeni kuhusu upangaji na utoaji wa Mikopo ya Elimu ya Juu, ni
kwamba hadi kufikia tarehe 2 Novemba, 2016 jumla ya wanafunzi 25,228 wa
mwaka wa kwanza walikuwa wamekwishapewa fedha za mikopo. Kati ya
wanafunzi hao, 4,787 ni Yatima, 127 wenye Ulemavu na 94 ni waliosoma
Sekondari kwa Ufadhili wa Taasisi mbalimbali.
31.
Mheshimiwa Spika, napenda kusisitiza kuwa wanafunzi wote wanaoendelea
na masomo, ambao ni wanufaika wa mikopo na vyuo vyao vimewasilisha Bodi
ya Mikopo taarifa za matokeo wameendelea kupatiwa mikopo kama ilivyokuwa
katika mwaka uliopita wa masomo.
Changamoto Zilizopo za Mkopo na Utatuzi Wake
32.
Mheshimiwa Spika, ili kutatua changamoto zinazojitokeza katika uratibu
wa mikopo ya wanafunzi, Serikali inafanya mapitio ya mfumo wa udahili wa
wanafunzi vyuoni, utaratibu mzima wa utoaji na urejeshwaji mikopo kwa
lengo la kuwa na mfumo bora zaidi na kuondoa adha inayowapata wanafunzi
wanapofungua vyuo kutokana na mfumo uliopo sasa. Nimeagiza kazi hii
ikamilike mapema ili mapendekezo ya mfumo utakaokuwa na tija zaidi
yaweze kuzingatiwa wakati wa maandalizi ya Bajeti ya 2017/2018.
SEKTA YA ARDHI
Hali ya Migogoro baina ya Watumiaji wa Ardhi Nchini:
33.
Mheshimiwa Spika, nchi yetu imeendelea kukumbwa na migogoro mbalimbali
ya ardhi baina ya watumiaji wa ardhi ikiwemo migogoro mikubwa baina ya
wakulima na wafugaji; migororo baina ya wananchi na wawekezaji; wafugaji
na hifadhi za Taifa na baina ya wakulima na baadhi ya maeneo ya hifadhi
za Wilaya mbalimbali.
Juhudi na Mikakati ya Serikali ya Kuondoa Migogoro Mikubwa ya Wakulima na Wafugaji
34.
Mheshimiwa Spika, migogoro ya matumizi ya ardhi baina ya Wakulima na
Wafugaji imeendelea kuongezeka kutokana na ongezeko la watu na mifugo,
na vijiji kutokuwa na Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi inayoainisha
maeneo mahsusi kwa ajili ya Kilimo na Ufugaji. Aidha, uwepo wa
mabadiliko ya tabia nchi yanayosababisha ukame na ukosefu wa malisho na
maji katika maeneo ya wafugaji kumesababisha uhusiano hafifu baina ya
jamii za wafugaji na wakulima kutokana na mifugo kuingizwa katika
mashamba ya wakulima kwa mabavu.
35.
Mheshimiwa Spika, migogoro hii imesababisha kuwepo kwa vitendo vingi
vya uvunjifu wa amani, upotevu wa maisha ya wananchi, baadhi ya wananchi
kupata vilema vya maisha, uharibifu wa mali, uharibifu wa mazingira,
athari za kijamii kama watoto kushindwa kwenda shule na wananchi
kushindwa kushiriki katika shughuli za maendeleo kutokana na hofu jambo
linaloweza kusababisha njaa na umaskini miongoni mwa jamii na Taifa.
Hatua za kutatua migogoro mikubwa ya wakulima na wafugaji
36.
Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na migogoro na kuwawezesha wakulima
na wafugaji kuendelea na shughuli zao bila migogoro, Serikali inaendelea
kutekeleza mikakati ya kuainisha, kupima, kutenga na kumilikisha ardhi
kwa ajili ya wafugaji na wakulima; na kanda za malisho kwa wafugaji
wakubwa na wadogo itakayohusisha vijiji, Wilaya na Mikoa. Maeneo haya
yatakayotengwa yatalindwa kwa kuyatangaza kwenye Gazeti la Serikali, na
matumizi yake yatasimamiwa ili kuhakikisha wanafuga kwa kuzingatia
uwiano wa malisho na mifugo.
37.
Mheshimiwa Spika, mikakati hiyo ni pamoja na kuzigawanya Ranchi
zilizopo katika vitalu ili wafugaji wenye ng’ombe zaidi ya 200 wahamie
huko, kila kitalu kimoja kulingana na uwezo wa kitaalamu wa kulisha
idadi maalum ya ng’ombe. Wafugaji wenye mifugo chini ya 200 watagawiwa
maeneo katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili yao katika vijiji na
watakuwa wanauza mifugo yao katika minada ambapo wafugaji kutoka Ili
katika ranchi watafika kununua mifugo hapo. Kwa mikoa ambayo haina
Ranchi za Taifa, watatenga maeneo yaliyo wazi kwa ajili ya wafugaji
wakubwa.
38.
Mheshimiwa Spika, ili kuzuia wafugaji kuhamahama kutafuta maji na
huduma nyingine, Serikali kwa kushirikiana na wafugaji itaweka
miundombinu ya majosho, mabwawa ya kunyweshea maji, huduma za ugani
zikiwemo matibabu, elimu ya kulima malisho, unenepeshaji, uwekaji sahihi
wa chapa za ng’ombe n.k.
39.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hatua hizo, jawabu la kudumu la migogoro
hii ni kuhakikisha kuwa tunawawezesha wafugaji kuvuna na kupunguza
mifugo bila kupata hasara, kupitia uwekezaji wa Viwanda vya Kuchakata
Nyama na Usindikaji Maziwa ili kuongeza thamani. Wizara husika zikae
pamoja na kubuni Mikakati na Mipango ya kuvutia wawekezaji katika eneo
hili katika miaka mitatu ijayo kuwe na tofauti.
40.
Mheshimiwa Spika, aidha napenda kuzikumbusha Halmashauri za Wilaya kote
nchini kuendelea kuweka na kutekeleza mipango madhubuti ya matumizi
bora ya ardhi, na wale wenye Benki ya Ardhi wagawe kwa busara kwa
wafugaji, wazuie wafugaji wengine wasiendelee kuingiza mifugo katika
maeneo ya kilimo na watumie sheria ndogo zilizopo na kama hazipo
ziandaliwe na kutumiwa; na ikibidi wahalifu wapelekwe mahakamani. Aidha,
niwakumbushe wafugaji wote kufuata sheria na kwamba Serikali haitasita
kuwachukulia hatua wafugaji watakaoingiza mifugo yao katika mashamba ya
wakulima kwa makusudi.
SEKTA YA NISHATI
Mradi Kabambe wa Kupeleka Umeme Vijijini Awamu ya Pili
41.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia umuhimu wa nishati ya umeme, Serikali
imeendelea kutoa mkazo katika kutekeleza na miradi mikubwa ya uzalishaji
na usafirishaji umeme pamoja na miradi ya kusambaza umeme vijijini. Ili
kuhakikisha huduma ya umeme inawafikia wananchi wengi, hususan waishio
vijijini, Serikali kupitia REA imeendelea kutekeleza Mradi Kabambe wa
Kupeleka Umeme Vijijini Awamu ya Pili tangu mwaka 2014. Mradi huu
unatekelezwa katika wilaya zote za Tanzania Bara. Hadi kufikia Oktoba,
2016 ujenzi wa kilometa za njia ya msongo wa Kilovolti (kV) 33 umefikia
Asilimia 95.6; ujenzi wa kilometa za njia ya Msongo wa Volti 400
umefikia Asilimia 89.3; na ufungaji wa transfoma umefikia Asilimia 87.2.
Aidha, jumla ya wateja 146,311 wa awali sawa na Asilimia 59 ya lengo la
wateja 255,000 wameunganishiwa umeme kupitia mradi huo.
Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu
42.
Mheshimiwa Spika, Mradi huu utatekelezwa kwa kipindi cha miaka 5 katika
vijiji 7,873 vya wilaya zote za Tanzania Bara. Takriban vijiji 7,697
vitapelekewa umeme wa gridi ya Taifa na vijiji 176 umeme wa nje ya gridi
(Off-grid). Mpango huu utaongeza wigo wa usambazaji umeme katika maeneo
ambayo hayakufikiwa na miradi ya REA Turnkey Phase I na II. Ili
kutekeleza miradi hiyo kwa kasi zaidi, Serikali ya Awamu ya Tano katika
bajeti yake ya mwaka 2016/17 iliongeza fedha za kupeleka umeme Vijijini
kutoka Shilingi Bilioni 357.117 zilizotengwa mwaka 2015/16 hadi Shilingi
Bilioni 587.61 mwaka 2016/17. Hadi kufikia mwezi Oktoba, Serikali
imetoa jumla ya Shilingi Bilioni 109.8 kwa ajili ya Mfuko wa Nishati
Vijijini kutoka kwenye vyanzo vya fedha za ndani. Kati ya fedha hizo
Shilingi Bilioni 100.4 ni tozo ya mafuta na Shilingi Bilioni 9.4 ni tozo
ya umeme.
43.
Mheshimiwa Spika, zabuni za kupata wakandarasi wa kutekeleza mradi huu
zilitangazwa tarehe 1 Agosti, 2016. Kwa sasa REA inaendelea na uchambuzi
wa zabuni hizo. Taratibu zote za mradi huo zimepangwa kukamilika mwezi
Januari, 2017. Natoa rai kwa viongozi mbalimbali wa Serikali wakimemo
Waheshimiwa Wabunge kuwahamisha wananchi katika maeneo yao kutumia fursa
ya kuunganishiwa umeme wakati wakandarasi wakiwa kwenye maeneo ya
miradi. Katika kipindi hicho bei ya kuunganisha umeme ni Shilingi 27,000
tu kama ilivyotaarifiwa awali katika Bunge hili.
44.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia imeanzisha Mradi wa Kupanua Wigo wa
Upatikanaji wa Umeme Vijijini (Tanzania Rural Electricity Expansion
Project). Mradi huo utagharamiwa kwa mkopo kutoka Benki ya Dunia wa Dola
za Kimarekani milioni 209. Mradi ulizinduliwa tarehe 26 Agosti 2016,
katika kijiji cha Kwedikwazu wilayani Handeni Mkoani Tanga na utawezesha
kaya takriban 500,000 kupata huduma ya umeme nchini.
SEKTA YA MADINI
Migodi Mikubwa Kuendelea Kulipa Mrabaha
45.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha kati ya Oktoba, 2015 na Oktoba,
2016 Serikali ilifanya ukaguzi na kuwezesha migodi mikubwa kulipa
mrabaha ambapo: Migodi Mikubwa ya Dhahabu ya Biharamulo, Bulyanhulu,
Buzwagi, Geita, New Luika na North Mara imelipa kiasi cha Dola za
Kimarekani Milioni 69.4 ikiwa ni Mrabaha, sawa na Shilingi Bilioni
151.4. Vilevile, Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Ngaka umelipa kiasi cha Dola
za Kimarekani 309,836 na Shilingi Milioni 676 ikiwa ni mrabaha. Aidha,
Mgodi wa TanzaniteOne umelipa mrabaha wa Dola za Kimarekani 189,731 sawa
na Shilingi Milioni 414.
Kuhamasisha Masoko ya Madini ya Vito Nchini
46.
Mheshimiwa Spika, Serikali iliandaa mnada wa madini ya vito, hususan
tanzanite uliofanyika kuanzia tarehe 9 hadi 12 Agosti, 2016 Jijini
Arusha. Katika mnada huo madini yenye thamani ya Dola za Kimarekani
3,448,050, sawa na Shilingi Bilioni 7.56, yaliuzwa na kuwezesha Serikali
kukusanya Dola za Kimarekani 150,491.06, sawa na Shilingi Milioni 331
ikiwa ni mrabaha kutokana na madini yaliyouzwa.
47.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kusimamia Sekta za Nishati na
Madini ili ziweze kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii kwa ajili ya
maendeleo ya Taifa letu.
TAARIFA YA MAKUSANYO YA FEDHA KWENYE HALMASHAURI KWA MWAKA 2016/2017
48.
Mheshimiwa Spika, katika Bajeti ya mwaka 2016/2017 Halmashauri
ziliidhinishiwa kukusanya mapato ya Shilingi Bilioni 665.4. Hadi kufikia
Septemba, 2016 Halmashauri zimekusanya Shilingi Bilioni 114.46, sawa na
Asilimia 17.2 ya makisio. Kiwango hiki cha ukusanyaji wa mapato katika
Halmashauri bado hakiridhishi. Hivyo, naomba nitumie fursa hii kuhimiza
Halmashauri zote nchini kuongeza jitihada katika kukusanya mapato ya
vyanzo vya ndani. Nazihimiza Halmashauri kutumia mifumo ya kielektroniki
katika ukusanyaji mapato na pia katika maeneo ya kutolea huduma za afya
ili kudhibiti upotevu wa mapato. Aidha, naelekeza Mamlaka za Serikali
za Mitaa waimarishe mifumo ya udhibiti wa ndani na kuhakikisha thamani
ya fedha inapatikana katika kila huduma au bidhaa inayonunuliwa na
Halmashauri. Halmashauri hazina budi kuepuka matumizi ya fedha yasiyo na
tija katika shughuli za uendeshaji wa Mamlaka hizo.
49.
Mheshimiwa Spika, Halmashauri zote zinaagizwa zifuatilie kwa karibu
mapato na matumizi ya fedha zinazopelekwa kwenye shule na kwenye vituo
vinavyotoa huduma za afya ikiwemo Hospitali, vituo vya afya na zahanati.
Ili kufikia azma hiyo, uwekwe utaratibu madhubuti wa ukaguzi wa mapato
na matumizi ya fedha hizo kwa kushirikisha Wakaguzi wa ndani wa
Halmashauri.
MAONI NA MAPENDEKEZO KUHUSU TAARIFA YA KAMATI YA BUNGE YA LAAC
50.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia ushauri mzuri na mapendekezo
yaliyotolewa na Kamati ya LAAC kuhusu ukaguzi uliofanywa na Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka 2013/2014 na 2014/2015,
Serikali imeshatoa maelekezo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa
kuhakikisha kuwa zinatekeleza kwa ukamilifu maelekezo yote ya Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa na Kamati nyingine ili
kuondoa hoja zilizojitokeza katika taarifa ya CAG. Aidha, Halmashauri
zinaelekezwa kuimarisha mifumo ya uthibiti wa ndani na kutumia vizuri
ushauri unaotolewa na Kamati za Ukaguzi ili kuimarisha uwazi na
uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma.
51.
Mheshimiwa Spika, napenda kusisitiza kwamba Halmashauri zote ni lazima
zitekeleze vipaumbele vilivyoidhinishwa katika mpango na bajeti kwa
mwaka 2016/17 kwa kupanga vema utekelezaji kwa kuzingatia upatikanaji wa
fedha. Halmashauri ziendelee kuimarisha usimamizi wa mikataba ili
thamani ya fedha za Serikali iweze kupatikana katika miradi na Kandarasi
nyingine zilizoingia Mikataba na Halmashauri.
HITIMISHO
52.
Mheshimiwa Spika, wakati tunahitimisha mkutano huu leo, napenda nitumie
nafasi hii kukushukuru wewe binafsi, Mheshimiwa Naibu Spika na
Wenyeviti wote wa Bunge kwa kusimamia vizuri na kwa weledi mkubwa vikao
vyote vya mkutano huu. Niwashukuru tena Waheshimiwa Wabunge wote kwa
michango yenu. Ninashukuru pia Watendaji wa Serikali kwa kuwasaidia
Mawaziri na Naibu Mawaziri katika kujibu maswali na hoja mbalimbali za
Wabunge. Niwashukuru wanausalama wote kwa kazi yao nzuri. Niwashukuru
madereva wote kwa kuwaendesha Mawaziri, Wabunge na Watendaji wote kwa
usalama kabisa. Niwashukuru pia wanahabari wote kwa kuihabarisha jamii
juu ya mkutano wetu. Kipekee, nimshukuru Katibu wa Bunge Dkt. Thomas
Kashililah na timu yake kwa kutuwezesha kukamilisha shughuli zote za
mkutano huu kwa mafanikio makubwa.
53.
Mheshimiwa Spika, mwisho, lakini si kwa umuhimu, nitumie muda huu
kumwomba Mwenyezi Mungu awalinde na awaongoze Waheshimiwa Wabunge wote
katika safari ya kurejea majumbani kwenu. Aidha, nawatakia kila la kheri
na fanaka katika sikukuu zijazo za mwisho wa mwaka na kuwatakia mwaka
mpya wa 2017.
54.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, napenda kutoa hoja kuwa Bunge
lako tukufu sasa liahirishwe hadi tarehe 31 Januari, 2017, siku ya
Jumanne, saa 3:00 asubuhi litakapokutana katika ukumbi huu hapa Dodoma.
55. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
0 comments:
Post a Comment