MPANGO wa Kunusuru Kaya Masikini (Tasaf), mkoani Dodoma utafanya
uhakiki nyumba kwa nyumba kubaini wanufaika hewa wa fedha zake,
wanaoendelea kulipwa mamilioni ya fedha wakati hawastahili.
Mratibu wa Tasaf mkoani hapa, Bogit Samhenda, alisema hayo juzi
wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi wa wilaya na halmashauri,
kuhusu utekelezaji wa mpango huo wa Tasaf, pamoja na shughuli za
serikali.
Samhenda alisema sasa utafanyika uhakiki nyumba kwa nyumba katika
wilaya zote saba za Dodoma zinazotekeleza mpango huo, kwani inaonekana
baadhi ya wanufaika ni hewa.
“Kuna watu wamehama, wamefariki lakini bado wanaendelea kulipwa,
lazima uhakiki ufanyike ili watu hao waondolewe, uhakiki utakuwa
endelevu,” alisema.
Alisema katika Awamu ya Tatu ya Tasaf jumla ya kaya 68,730 zilifikiwa na mpango huo na Sh bilioni 33 zilitolewa.
“Wilaya zote saba za mkoa wa Dodoma zinatekeleza mpango huo, Chamwino
ilikuwa ya kwanza kuanza kutekeleza mpango huo Januari 2014 na wilaya
nyingine zote zilizobaki zilianza Septemba 2014,” alisema na kuongeza
kuwa, sasa Chamwino iko katika awamu ya 17, wakati wilaya nyingine sita
zimehaulisha awamu 13.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana, amepiga
marufuku masuala ya siasa kuingizwa kwenye mpango huo wa kunusuru kaya
masikini na kutaka kuondolewa wote wasiostahili ili walengwa wanufaike.
Pia, amewataka viongozi wa wilaya ya halmashauri za mkoa wa Dodoma
kukaa na kuzungumza lugha moja juu ya utekelezaji wa mpango huo ambapo
sasa uhakiki utafanyika nyumba kwa nyumba ili kuwabaini wasiostahili na
kuondolewa.
Katibu Tawala wa Mkoa, Rehema Madenge, alisema suala la uhakiki wa
walengwa ni lazima lipewe kipaumbele. Alitaka kila mkuu wa wilaya
asimamie shughuli hiyo.
Chanzo Gazeti la Habari Leo
0 comments:
Post a Comment