Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe.
Dkt Hamis Kigwangalla akijibu hoja mbalimbali kutoka kwa wabunge katika
kikao cha saba cha mkutano wa tano wa Bunge la 11 linaloendelea Mjini
Dodoma Novemba 9, 2016.
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO, Dodoma.
Wizara
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeanzisha mafunzo
ya Tiba Shufaa (Palliative Care Services) kwa watumishi wa Sekta ya
Afya ili kuhakikisha huduma hiyo inapatikana kwa wakati kwa wagonjwa
wanaohitaji.
Naibu
Waziri wa Wizara hiyo, Dkt. Hamis Kigwangalla ameyathibitisha haya leo
mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mhe. Susan Lyimo aliyehitaji
kufahamu juu ya mikakati ya Serikali katika kuhakikisha huduma ya Tiba
Shufaa inaboreshwa hapa nchini.
Dkt.
Kigwangalla amesema kuwa katika kuhakikisha huduma za tiba shufaa
zinapatikana hapa nchini, hospitali takribani 35 zikiwemo za Rufaa za
kanda za Bugando, KCMC na Mbeya , Hospitali za mikoa pamoja na Hospitali
za dini zinatoa huduma hizo.
Ameongeza
kuwa huduma hizo pia zimekuwa zikitolewa majumbani kwa wagonjwa
wanaokaa karibu na maeneo yenye hospitali zinazotoa huduma hizo ambapo
watoa huduma za majumbani husaidia kumfikia mgonjwa moja kwa moja katika
maeneo wanayoishi.
“Sera
ya kitaifa ya Tiba Shufaa iliyotolewa Mwezi Juni mwaka huu imeagiza
mafunzo yafanyike ili kuwajengea uwezo watumishi waliopo katika vituo
vya afya na hospitali nchini ili waweze kutoa huduma hiyo” alisisitiza
Mhe. Dkt Kigwangalla.
Aidha
Wizara hiyo imeanza kutoa mafunzo hayo kwa kushirikiana na Taasisi ya
Saratani ya Ocean Road, Chama cha Tiba Shufaa pamoja na wadau wengine
kwa lengo la kuhakikisha kunakuwa na watumishi watano katika kila kituo
cha afya ambao wana uwezo wa kutoa tiba hiyo wakijumuisha madaktari,
wauguzi, wafamasia pamoja na maafisa ustawi wa jamii.
Tiba
Shufaa ni huduma inayotolewa kwa wagonjwa walio katika hatua za mwisho
za maisha yao hasa walio na magonjwa yasiyo na uwezekano wa kupona kwa
ajili ya kuwapunguzia maumivu makali wanayoyapata kutokana na magonjwa
hayo.
MWISHO.
0 comments:
Post a Comment