WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali itaanza kusambaza kiasi
cha tani milioni 1.5 za chakula zilizobaki msimu uliopita katika maeneo
yenye uhitaji mkubwa ili kupunguza kasi ya ongezeko la bei ya vyakula
nchini.
Waziri Mkuu aliwaambia waandishi wa habari jana mjini Dodoma kwamba
katika msimu uliopita, kulikuwa na zaidi ya tani milioni tatu na hivyo
baada ya wabunge kushinikiza serikali kuruhusu kuuza vyakula nje, kiasi
cha tani milioni 1.5 kiliuzwa na hivyo kubakiwa na tani milioni 1.5.
Aidha, imefahamika kuwa hadi kufikia Januari 12, mwaka huu, Wakala wa
Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) walikuwa na akiba ya tani 88,152 za
mahindi.
Waziri Mkuu Majaliwa alisema serikali ndio yenye jukumu la kutangaza hali ya chakula kama ni mbaya au nzuri.
“Tanzania bado haina tatizo la chakula, kelele zinazopigwa na baadhi
ya vyombo vya habari na taarifa zinazotolewa si sahihi, serikali ndiyo
yenye mamlaka ya kutangaza hali ya chakula na kwa maana hiyo basi bado
tuna chakula cha kutosha,” alieleza Majaliwa na kuongeza kuwa pale
serikali itakapokuwa na upungufu Watanzania watapata taarifa.
Waziri Mkuu alisema ni kweli kumekuwa na shida ya mvua, lakini sasa
karibia maeneo yote mvua zimeanza kunyesha na mikoa mingine mvua
zinanyesha na kutaka kutumia mvua zinazonyesha kwa kupanda mazao ya muda
mfupi ili msimu ujao chakula cha kutosha kipatikane.
Pia alisema kwenye baadhi ya mazao yamepanda bei kutokana na nchi jirani za Afrika Mashariki kuwa na uhaba wa chakula.
“Kazi yetu ni kuhakikisha chakula kinakuwa kingi ili kiweze kuwa na
bei nafuu,” alieleza na kuongeza kuwa tatizo hili limekuwa kama kampeni
ya wafanyabiashara kuonesha nchi ina upungufu mkubwa wa chakula, jambo
ambalo si sawa sawa.
Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles
Tizeba, alisisitiza kuwa hali ya chakula nchini inaridhisha isipokuwa
zao la mahindi ambalo kwa sasa bei yake imepanda ikilinganishwa na msimu
kama huu, wa mwaka jana.
Aidha, amekiri kuwa kwa sasa kumekuwa na uingiaji wa taratibu wa
mazao mapya kutokana na baadhi ya maeneo kukumbwa na tatizo la uhaba wa
mvua za vuli.
Aidha, ametoa onyo kwa wafanyabiashara aliowaita wenye hila
wanaonunua mahindi kwa kasi na kuyafungia ndani na kusubiri bei ya zao
hilo ipande zaidi ndipo wayalangue, na kuwataka wayauze mazao hayo mara
moja kabla serikali haijachukua hatua za ziada dhidi yao.
Dk Tizeba alibainisha hayo jana jijini Dar es Salaam wakati
akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya chakula nchini, ikiwa
ni pamoja na kutoa ufafanuzi dhidi ya madai kwamba nchi imekumbwa na baa
la njaa.
“Nawahakikishia Watanzania kuwa hali ya chakula si mbaya, serikali
inao utaratibu wake wa kutathmini hali ya chakula eneo kwa eneo, mkoa
kwa mkoa na wilaya kwa wilaya,” alifafanua Dk Tizeba na kuongeza:
“Nafahamu kuwa kuna watu wanavumisha huko kwenye mitandao ya kijamii
na baadhi ya vyombo vya habari kuwa kuna baa la njaa. Si kweli, serikali
iko hadi kwenye ngazi ya mamlaka ya vitongoji inafahamu vyema hali
halisi ya chakula ilivyo nchini,” alisisitiza.
Alisema kuanzia Oktoba mwaka jana, Tanzania ilikuwa na ziada ya
chakula kilichozalishwa ya zaidi ya tani milioni tatu na hivyo kuwa na
kiwango cha akiba ya chakula kwa asilimia 100.
Alisema kutokana na wingi huo wa mazao yaliyovunwa, wabunge na
wananchi waliwasilisha kilio na wasiwasi wao juu ya uwezekano wa kushuka
kwa bei ya mazao na kuomba waruhusiwe kuuza mazao hayo nje, ombi
lililokubaliwa.
“Sasa ni takribani miezi miwili tangu turuhusu mazao hayo kuuzwa nje
ambayo ni takribani tani milioni 1.5, tena tulitahadharisha wakulima
kuwa makini kwa kutonogewa na bei na kujikuta wanauza kila kitu bila
kuweka akiba, tulifanya hivi ili kuhakikisha usalama wa chakula nchini
mwetu,” alifafanua.
Alisema nchi nyingi za jirani kama vile Msumbiji, Zambia, Malawi,
Kenya na Uganda nazo hazikuzalisha kwa kiwango cha kuridhisha mazao
msimu uliopita na hivyo kutegemea zaidi Tanzania.
“Kama kweli tungekuwa na uhaba wa chakula, nchi hizi nazo zingetangaza kukumbwa na balaa la njaa.”
Alisema katika taarifa inazokusanya kutoka sehemu mbalimbali nchini
hali ya upatikanaji wa chakula katika masoko yaliyopo kwenye halmashauri
zote inaridhisha isipokuwa bei ya mahindi iliyopanda ikilinganishwa na
mwaka jana katika msimu kama huu.
Dk Tizeba alisema katika msimu wa chakula na soko kwa mwaka 2016/17
bei ya mazao imekuwa na mwelekeo wa kupanda kuanzia mwanzoni mwa Julai
mwaka jana.
Alisema hadi kufikia Desemba mwaka huo, bei ya mahindi kwagunia la
kilo 100 ilipanda na kufikia wastani wa Sh 84,000 ikilinganishwa na
Desemba mwaka 2015 ambapo gunia la kilo hizo 100 liliuzwa kwa wastani wa
Sh 65,104.
Kwa upande wa mchele na maharage, bei ina mwelekeo wa kushuka ambapo
bei ya wastani kwa mwezi Desemba mwaka jana kwa gunia la kilo 100 ni Sh
151,957 wakati kwa mwaka 2015 bei ya gunia hilo liliuzwa kwa Sh 176,237
na maharage mwaka 2015 yaliuzwa kwa Sh 172,852 na hadi kufikia Desemba
mwaka jana zao hilo liiuzwa kwa Sh 171.251.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa pamoja na hali hiyo hakuna hata soko
moja hapa nchini ambalo limekosa bidhaa za mahindi, mchele na maharage.
Alisema serikali inatambua uwepo wa tatizo la uhaba wa mvua za vuli
ambazo katika baadhi ya maeneo hazikunyesha kwa kiwango kinachoridhisha
hali iliyosababisha kuwepo na tatizo la uingizwaji wa mazao mapya.
“Lakini nataka ieleweke kuwa Tanzania inategemea zaidi mazao kupitia
msimu wa mvua za masika na si vuli. Kutokana na hali iliyopo kupitia
Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini tayari tumeanza kuona kuwa huenda pia
mvua za masika zisijitosheleze katika baadhi ya maeneo,” alisema.
Alisema serikali imejipanga kupitia wakuu wa mikoa kueneza uelewa kwa
wakulima kuhakikisha wanatumia mbegu zinazokomaa mapema na kupanda
mazao yanayostahimili ukame.
Dk Tizeba alisema katika kuhakikisha nchi inakuwa salama Wakala wa
Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kwa mwaka wa fedha 2016/17 ilipanga
kununua jumla ya tani 100,000 za chakula, lakini hadi kufikia Januari 8,
mwaka huu ilinunua tani 62,087 za mahindi sawa na asilimia 62 ya lengo
iliyojiwekea.
Alisema kati ya tani hizo, tani 38,162 zilinunuliwa kupitia vituo vya
ununuzi na tani 23,925 zilinunuliwa kupitia vikundi vya wakulima na
hadi kufikia Januari 12, mwaka huu NFRA ina akiba ya tani 88,152 za
mahindi. Waziri huyo, aliwataka viongozi wote nchini kutotumia hali ya
ukame katika baadhi ya maeneo kueneza uvumi wa kuwepo kwa baa la njaa na
kuwapatia taharuki wananchi.
Aidha, aliwataka wafanyabiashara wanaotumia fursa hiyo kwa lengo la
kujifaisha wenyewe hapo baadaye kwa kununua mazao na kuyaficha kuacha
mara moja kwani tayari serikali kupitia vyombo vyake inazo taarifa za
wafanyabiashara hao na wakiendelea kukaidi watachukuliwa hatua.
Hivi karibuni, Rais John Magufuli alitoa mwito kwa wakazi wa maeneo
mbalimbali nchini kutumia mvua zinazoendelea kunyesha kwa ajili ya
kulima mazao yanayostahimili ukame badala ya kutegemea chakula kutoka
serikalini.
Rais Magufuli alisema sasa wakati wa kulima mahindi umebadilika, na
wakulima wasijilazimishe kulima mahindi ambayo yanahitaji mvua nyingi.
“Mvua zinaponyesha tulime kwani hakuna shamba la serikali,” alieleza
Dk Magufuli. Imeandikwa na Sifa Lubasi, Dodoma na Halima Mlacha, Dar.
CHANZO GAZETI LA HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment