JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
TAARIFA KWA UMMA
Wizara
ya Maliasili na Utalii imesitisha utoaji wa vibali vya kusafirisha mkaa
kutoka Wilaya moja hadi nyingine kuanzia terehe 01 Julai mwaka huu.
Agizo
hilo limetolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne
Maghembe na kuungwa mkono na Baraza la wafanyakazi la Wizara wa
Maliasili na Utalii kwa lengo kupunguza uharibifu mkubwa wa mazingira
hususan ukataji wa miti hovyo.
Baraza
hilo lililofanyika mjini Dodoma tarehe 10 Aprili, 2017 pia lilijadili
umuhimu wa kutumia mkaa mbadala kwa miji mikubwa kama Dar es Salaam,
Mwanza na Mbeya ambapo mpango mahususi wa kutumia mkaa mbadala
utakaozalishwa na kiwanda cha Mufindi – Iringa utawasilishwa ifikapo
mwezi Julai mwaka huu.
Baraza
la Wafanyakazi wa Maliasili na Utalii pia limepitisha kwa kauli moja
kuongeza jitihada katika kukabiliana na ujangili hasa katika Pori la
Akiba la Selous, Pori Tengefu la Loliondo, Rungwa na Yaeda Chini. Nguvu
zaidi ya kukabiliana na changamoto ya uingizaji wa mifugo katika maeneo
ya hifadhi ambao unachangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la ujangili pia
ilijadiliwa.
Aidha,
Baraza liliazimia mali za majangili pamoja na mifugo itakayokamatwa
katika maeneo ya hifadhi yataifishwe kwa mujibu wa sheria.
Katika
kukabiliana na changamoto ya usafirishaji wa magogo nje ya nchi, Baraza
liliazimia kuwa usafirishaji wa magogo ufanyike kwa kutumia nyaraka
halisi (Original Documents) badala ya vivuli vya nyaraka (Photocopy).
Baraza
hilo la Wafanyakazi pia liliazimia kuwa watumishi wote wa wizara
wazingatie sheria na kanuni za utumishi wa umma katika maeneo yao ya
kazi pamoja na utoaji wa huduma kwa Umma.
Mkutano
huo wa Baraza la Wafanyakazi hufanyika mara mbili kwa mwaka kwa lengo
la kupitia utekelezaji wa bajeti ya mwaka uliopita na kutoa maoni yao
kwa bajeti ya Wizara inayotarajiwa kuwasilishwa bungeni pamoja na
kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili na kuweka mkakati wa
kukabiliana nazo. Wajumbe wa Baraza hilo ni wawakilishi wa watumishi
kutoka katika Idara, Vitengo, Taasisi na Vituo vya Wizara.
Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Maliasili na Utalii,
11 Aprili, 2017
Dodoma.
0 comments:
Post a Comment