Imeandikwa na Sifa Lubasi, Dodoma.
MWANASHERIA Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu jana alikataa kuondoka chumba
cha Mahakama ya Wilaya ya Dodoma, akidai kuwa ana taarifa ya kutakiwa
kukamatwa na Polisi ili kupelekwa jijini Dar es Salaam.
Tukio hilo lililotokea mahakamani hapo jana, lilileta taharuki na
kufanya watu wajae mahakamani. Hali hiyo ilitokea mara baada ya
kuahirishwa kwa kesi ya Chama cha Walimu Manispaa ya Dodoma (CWT)
iliyokuwa inahusu mgogoro wa viongozi wa chama hicho wanaodaiwa kufanya
matumizi mabaya ya mali za chama hicho.
Katika kesi hiyo, Lissu alikuwa ni Wakili wa Utetezi upande wa
Viongozi wapya. Akizungumza baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo hadi
Septemba 27, mwaka huu, Lissu alisema amepata taarifa za kutaka
kukamatwa kupitia ujumbe mfupi aliotumiwa na Mkewe toka Dar es salaam
ambapo asubuhi askari walifika nyumbani kwake na kujulishwa kuwa yupo
Dodoma.
“Sitatoka Mahakamani hapa kama wao wana uwezo na wanafanya kazi kwa
maelekezo waje wanikamatie hapa mahakamani, sitoki nitaendelea kunywa
maji yangu haya yatanipa nguvu ya kukaa hadi jioni,” alisema Lissu.
Lissu alisema aliamua kubaki mahakamani baada ya kudokezwa kuwa kuna
gari linamsubiri nje ya mahakama kupelekwa Dar es Salaam. Katika
mazingira ya mahakama kulikuwa na watu walioonekana kusubiri wakiwa
katika mavazi ya kiraia huku gari la Polisi likiwa limeegshwa jirani na
lango la kuingilia viwanja vya Mahakama hiyo.
Alipoulizwa anahisi nini chanzo cha kutaka kukamatwa kwake, Lissu
alisema anahisi kauli zake za karibuni dhidi ya Rais John Magufuli
kuhusu utendaji wake. Kutokana na Lissu kugomea kutoka mahakamani,
alizua taharuki na kusababisha watu kurundikana mahakamani hapo huku
gari linalodhaniwa ndilo limeegeshwa kumsubiri likiondolewa mahali
lilipokuwepo.
Lissu hadi saa kumi kasoro jioni alikuwa bado ndani ya mahakama hiyo
huku akidai kuwa anaandika ujumbe mfupi wa kuwajulisha watu wengine.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa alisema anamshangaa
Lissu na kwamba Polisi hawana mpango wa kumkamata na wakitaka kumkamata
hata mahakamani ndani, wana uwezo wa kumtoa.
“Kama anaogopa polisi, kwanini anazungumza maneno yasiyofaa mbele ya
jamii?,” alihoji Mambosasa. Kamanda Mambosasa alimtaka Lissu kutoka,
kwani hawana mpango naye na wanashangaa alipozitoa hizo taarifa.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment