Na: Veronica Kazimoto
Dodoma
18 Julai, 2017.
Utafiti wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Tanzania wa awamu ya pili unatarajia kufanyika mwezi Agosti mwaka huu.
Akizungumza wakati wa mafunzo ya wadadisi yanayoendelea kufanyika mkoani Dodoma Meneja wa Shughuli za Kitakwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu Wilfred Mwingira amesema lengo
kuu la utafiti huo ni kufuatilia viashiria vilivyowekwa kwenye utafiti
wa awamu ya kwanza ili kutathmini na kujua kama kuna athari yoyote
iliyotokea.
"Utafiti huu ni wa
kitaifa na utafanyika Tanzania Bara na Zanzibar kwa lengo la kutathmini
na kujua kama kuna athari yoyote iliyojitokeza kwenye viashiria
vilivyowekwa kwenye utafiti wa awamu ya kwanza", amesema Mwingira.
Nae Mratibu wa utafiti
huo Rainer Kiama amesema kuwa utafiti huu unafanyika ili kutathmini kama
mpango unaleta manufaa yaliyokusudiwa katika ngazi ya kaya kwa kutumia
viashiria kama vile elimu, afya, kazi na matumizi ya muda, shughuli za
kaya zisizo za kilimo, mapato, mikopo, akiba na uhamishaji fedha.
Viashiria vingine ni shughuli za kilimo, makazi ya kaya na upatikanaji wa maji, matumizi na usalama wa chakula katika kaya,
maamuzi katika kaya, ukatili kwa wanawake na matarajio ya vijana,
mahusiano ya kaya na jamii pamoja na mtazamo wa kaya kuhusu Mpango wa
Kunusuru Kaya Maskini.
Utafiti wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Tanzania wa awamu ya pili utahusisha kaya takribani elfu saba (7,000) ambazo zilihojiwa katika utafiti wa awamu wa kwanza uliofanyika mwezi Juni, 2015.
0 comments:
Post a Comment