Home » » MBINU MPYA ZA WIZI ZALIZA DODOMA

MBINU MPYA ZA WIZI ZALIZA DODOMA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
 
WAKATI Mkoa wa Dodoma ukiendelea kupokea watumishi wanaohamia makao makuu ya nchi, vitendo vya uhalifu vikiwamo vya kuvunja nyumba za watu vilivyokuwa vikisikika jijini Dar es Salaam, sasa vimeanza kushamiri mkoani humo.
Mbali na kuvunja nyumba za watu kwa kutumia njia mbalimbali zikiwamo za kupuliza dawa za usingizi, wahalifu wamebuni mbinu mpya ya kufungua maji kwenye nyumba zenye mabomba ya maji nje, ili kupata urahisi wa kuingia ndani.
Vitendo hivyo vimetajwa kushamiri katika mitaa ya Nkuhungu, Ndachi, Area A, Chang’ombe, Kizota na Mbwanga.
Kadhalika, vitendo vya kinamama kukabwa na kuporwa mikopa kwa kutumia pikipiki navyo vimeongezeka huku maeneo ya Chinangali, Maluwe, Swai na katikati ya mji yakishamiri kwa matukio ya aina hiyo.
Nipashe ilipita katika maeneo hayo mwishoni mwa wiki na kuzungumza na baadhi ya wananchi kuhusu vitendo hivyo, ambapo walisema uhalifu huo umekuwa ukiwarudisha nyuma kimaendeleo.
Elizabeth Daniel, mkazi wa Nkuhungu, alisema vitendo hivyo vimeonekana kuongezeka kwa kasi kwa siku za hivi karibuni na kuwafanya walale wakiwa na hofu ya kuibiwa.
Alisema wahalifu hao wamekuwa wakivunja nyumba za watu kwa kuchomoa vioo vya madirisha na kuingia ndani kuchukua vitu mbalimbali hasa viambaza vya kisasa (flat screens), redio na wakati mwingine ving’amuzi.
"Juzi nyumba ya jirani yangu aliamka asubuhi akakutana na mwanga mkali unatoka dirishani, kuangalia sebuleni kwake akakuta wameshabeba Tv, redio na king’amuzi,” alisema.
Alibainisha kuwa uhalifu unaojitokeza katika mitaa hiyo kwa asilimia kubwa ni wa kuibiwa vitu hivyo.“Kinachostaajabisha sasa hivi kama una bomba lako la maji nje, kuwa makini usije ukasikia maji yanamwagika usiku ukatoka, wenzako wanaingia ndani kirahisi na kufanya yao," alisema.
Mkazi wa Chang’ombe, Majaliwa Rajab, alidai mtaa huo umekuwa na vibaka wengi ambao wamekuwa wakifanya uhalifu mitaa mingine.
Alisema mitaa hiyo kutembea usiku ni hatari kwa kuwa vibaka wamekuwa wakipora watu na kuwapiga kwa nondo na kuwachoma bisibisi.
"Yaani haya matukio ya mtu kuvunjiwa nyumba mpaka sasa tunayaona yamekuwa mengi hadi watu wameyazoea, wakati mwingine tunawakurupusha na kukimbizana nao, wengine tunawakamata na kuwapeleka polisi, lakini wengine hatuwapati,” alisema Rajab.Alisema mbinu ya wahalifu kufungua maji kwenye mabomba wanaitumia sana kwa sasa kupata urahisi wa kuingia ndani ya nyumba husika.
“Yaani wenye mabomba ya maji nje ya nyumba wachukue tahadhari maana sasa hivi wanafungua maji yanamwagika, ukitoka tu kwenda kuangalia maji yanayomwagika huku wenzako wanaingia ndani kuchukua kila wanachokitaka," alisema.
Frank Mhagama, Mkazi wa Mbwanga, alisema wananchi sasa wanaishi roho juu wakiogopa kuibiwa.
"Sijui ni ugumu wa maisha maana vibaka wamezidi jamani, tunaomba tu Jeshi la Polisi liongeze doria mitaani," alisema.Aliongeza kuwa imefika wakati watu wanalazimika kufua nguo na kuzilinda kwa kuwa wakiingia ndani tu, nje zinaibiwa hata kama bado hazijakauka.
Mmoja wa wadada waliokumbana na mkasa wa kukwapuliwa pochi, Halima Awadh, alisema mwanzoni mwa mwezi huu, majira ya saa 12 jioni, akiwa njiani kurudi nyumbani, alikwapuliwa pochi yake na watu waliokuwa wamepakiana kwenye bodaboda.
“Pochi yangu ilikuwa na vitambulisho vya kazi na pesa Sh. 50,000, walikwapua na kukimbia nayo na nilipojaribu kupiga kelele walikuwa tayari wameshatokomea, nilikuwa tu nasikia haya matukio Dar kumbe na Dodoma ndio yameshapiga hodi,"alisema.
Aliongeza kuwa matukio ya watu kukabwa na kupigwa nondo kichwani au bisibisi yameanza kushamiri mkoani humo.“Hii hamiahamia ya Dodoma jamani sasa imeleta na wahalifu, maana haya tulikuwa tunasikia tu Dar es Salaam, sasa ni Dodoma. Polisi tunawaomba watusaidie kukabiliana na vitendo hivi," alisema.

POLISI YAFUNGUKAKamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa, alikiri kuwapo kwa uhalifu wa aina hiyo alipotafutwa na Nipashe jana.
Alisema Jeshi la Polisi limeshachukua hatua kukabiliana na uhalifu huo na tayari vijana wake wako kazini."Huo uhalifu upo na tumeshabaini wahusika na kuna vitu mbalimbali tumeendelea kukamata na mitandao yao mbalimbali. Sisi kama Jeshi la Polisi tumejipanga kuhakikisha hakuna (mhalifu) anayepona," alisema.
Aidha, alisema tayari baadhi ya watu wanaofanya uhalifu huo wamekamatwa na kesi zao zipo katika hatua mbalimbali mahakamani.
“Wengine wametupeleka hadi Mwanza. Unajua serikali ilipotamka kuhamia Dodoma nao wakajivuta kuja kwa hiyo, tumekwenda hadi Mwanza kuna watu wamekamatwa na kurudishwa hapa kwa ajili ya hatua za kisheria," alisema Mambosasa.
Mambosasa alisema mtu anayefanya uhalifu wa aina hiyo ajue hayupo salama kwa sababu tayari Jeshi hilo limejipanga kuhakikisha wananchi wanaendelea kuwa salama kwenye maeneo yao.
"Tunafanya doria sana, siyo tu doria ya polisi, lakini pia tunatumia polisi wa pikipiki, magari na mbwa na pia tunashirikisha na wenzetu wa kampuni za ulinzi binafsi na vikundi vya ulinzi shirikishi, ili kuhakikisha mambo yanakuwa sawa," alisema.
Kamanda Mambosasa aliwatoa hofu wakazi wa Dodoma akiahidi kuwa jeshi hilo litakabiliana na uhalifu wa kila aina huku akiwataka kutoa ushirikiano kwao kuwabaini wahalifu hao.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa