Home » » WANG’OLEWA UBADHIRIFU WA FEDHA ZA USHIRIKA

WANG’OLEWA UBADHIRIFU WA FEDHA ZA USHIRIKA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

 
VIONGOZI wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Akiba na Mikopo (SCCULT), akiwamo Mtendaji Mkuu Habib Mhezi, wameondolewa madarakani kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha.
Uamuzi huo ulitangazwa jana na Kaimu Mrajisi wa Vyama vya Ushirika nchini Tito Haule katika Mkutano Mkuu Maalum wa Chama hicho, mjini Dodoma, baada ya taarifa ya ukaguzi kubaini kuwapo matumizi mabaya ya fedha za mikopo ya wanachama kutoka katika taasisi mbalimbali za fedha.
Awali, akisoma taarifa ya ukaguzi, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ukaguzi wa Hesabu za Vyama vya Ushirika (Coasco), Goldeni Kajaba, alisema kwa miaka minne mfululizo kumekuwapo na hasara ndani ya chama hicho.

Alibainisha ubadhirifu huo ni katika fedha kutoka mifuko mbalimbali ukiwamo Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (JK Fund), Mfuko wa Kukopeshana (Central Financial Programme-CFP), fedha za mikopo ya Mfuko wa Pembejeo wa Taifa (AGITF) ambayo ilikuwa inasimamiwa na chama hicho.

Kutokana na taarifa hiyo, baadhi ya wajumbe wa mkutano huo waliibuka na kuhoji huku wengine wakitaka chama hicho kifutwe kutokana na kukosa imani juu ya utendaji wake.

Walisema ukosefu wa uadilifu kwa viongozi ndio umekifikisha chama katika changamoto hiyo.

“Fedha zetu zitarudi, vipi hasa tulizowekeza kwa CFP,” walihoji baadhi ya wanachama hao.

Akizungumza baada ya mkutano kumalizika, Mrajisi huyo alisema katika mkutano huo wameamua kuwaondoa madarakani viongozi wa chama hicho na ataunda timu itakayoenda kufanya uchunguzi dhidi ya ubadhirifu huo.

“Timu hii itaenda kufanya uchunguzi wa taarifa mbili zilizojadiliwa na wanachama. Tumewaondoa madarakani Mtendaji Mkuu na viongozi wengine wa chama,” alisema Haule.

Alibainisha kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Ushirika, fedha zinatakiwa kurudishwa na wahusika lazima wachukuliwe sheria za kijinai.

Aidha, Haule alisema kumekuwa na utendaji usioridhisha wa chama hicho na kusababisha kuwapo malalamiko mengi kutoka kwa wanachama.


Alisema tangu mwaka 2008, uendeshaji wake umekuwa si wa kuridhisha na kusababisha wanachama kushindwa kupata huduma.

“Nimepokea barua za SACCOS zenye malalamiko mbalimbali juu ya SCCULT. Baadhi ya malalamiko yaliyoelezwa kwenye barua hizo ni pamoja na suala la akiba na hisa za vyama hivyo zilizowekezwa SCCULT kutojulikana zilipo pamoja na baadhi ya vyama kila mara vinapotaka kujitoa SCCULT Ltd huwa hawapati fedha zao zilizowekezwa huko,” alisema.

Hata hivyo, alisema baadhi ya vyama vilikuwa vikilalamikia kutofanyika kwa mikutano mikuu pamoja na kutojulikana kwa taarifa za hesabu za chama chao kwa muda wa miaka minne sasa.

Chanzo:Nipashe

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa